The House of Favourite Newspapers

Mchungaji Mkanyaga Watu Yamkuta Dar

DAR ES SALAAM: Yawezekana wewe ni kati ya wale waliowahi kuona picha za mchungaji ambaye anaonekana akiwa amewakanyaga waumini wake pamoja na kubebwa mgongoni na ukaamini si habari ya Tanzania bali Nigeria au Afrika Kusini.

 

Kama jibu ni ndiyo, habari mpya ikufikie kwamba, mchungaji huyo aliyeibua taharuki anayefahamika kwa jina la Bethania Simon anafanya shughuli zake za kitumishi katika Kanisa la Neema ya Kitume (AMG) lililopo Mbezi Luis jijini Dar.

AINA YAKE YA MAHUBIRI YASHANGAZA

Mchungaji huyo ambaye picha nyingi mitandaoni zinamuonesha akiwa anahubiri huku akiwa amewakanyaga waumini migongoni na nyingine akiwa amebebwa mithili ya mtoto mdogo, amekuwa gumzo na kuzua kasheshe mtaani huku baadhi ya watu wakimtuhumu kwa kuwadhalilisha waumini wake.

Baadhi ya watu walioziona picha zake mtandaoni walikomenti wakisema kuwa, anachokifanya ni kinyume na haki za binadamu kwani hakuna maandiko yanayoeleza aina hiyo ya kuhubiri neno la Mungu.

“Hii siyo sawa kabisa, hivi mimi kweli naweza kwenda kuabudu kwenye kanisa hili? Anachokifanya mchungaji huyu ni kuwadhalilisha watu wa Mungu, nadhani viongozi wakubwa wa dini wanatakiwa kuingilia kati,” aliandika mmoja wa waumini aliyejitambulisha kwa jina la Janeth E.

Mwingine akaandika: “Mimi nadhani hii siyo Tanzania, anaweza kuwa mchungaji wa nje, ila hii ni kali.”

Hata hivyo baada ya mchungaji huyo kuzua kasheshe mtaani, waandishi wetu walifanya uchunguzi na kubaini kuwa kumbe si mchungaji wa nje ya nchi kama baadhi walivyodhani bali anapatikana Mbezi Luis jijini Dar.

SAFARI YA KUMSAKA

Baada ya taarifa kuwa mtumishi huyo anapatikana Mbezi, jitihada za kumsaka zilianza na alipopatikana alifunguka mambo ya kushangaza ikiwa ni pamoja na mazito yaliyomkuta baada ya picha zake kusambaa mitandaoni.

“Kwanza niseme tu kwamba, niliyokutana nayo baada ya picha hizo kuvuja ni mazito, hakuna watu wa haki za binadamu walionifuata wala taasisi yoyote iliyonifuatilia kuhusiana na picha hizo ila nimekejeliwa sana, nimetukanwa sana na kuambiwa kila aina ya neno baya.

“Ukweli ni kwamba, wengi waliona picha tu na bila kujua nilikuwa nafanya nini waliamini kuwa ile ndiyo staili yangu ya kutoa mahubiri wakati siyo hivyo.

“Picha zote zilizosababisha watu wanione sifai zilikuwa ni kwenye mafundisho, sasa kwenye yale mafundisho inapofika kwa mfano sehemu nazungumzia watu kubebana, naonesha kwa mifano, namchukua muumini, ananibeba au nasimama juu ya migongo ya watu kisha nashuka na kuendelea na kazi ya Mungu.

“Siyo kwamba hivyo ndivyo ninavyoendesha ibada zangu, naomba watu wanielewe hivyo,” anasema mchungaji huyo.

Mchungaji huyo anaongeza kuwa, uzuri waumini wake wanajua anachokifanya na kwamba siyo kuwadhalilisha, wanajua ni sehemu ya mafundisho.

MAHOJIANO ZAIDI NA MCHUNGAJI HUYO

Risasi Jumamosi: Watu wanasema ilikuwa ni kiki ya kulitangaza kanisa lako, unasemaje kuhusu hilo?

Mchungaji: Hapana, wala haikuwa kiki na huwezi amini baada ya siku ile nilipata misukosuko ya kutukanwa sana, nilipigiwa simu nyingi watu wakiniita mchungaji wa uongo lakini ni kwa sababu ya picha kwani ingekuwa video wangeelewa nilikuwa namaanisha nini.

Risasi Jumamosi: Kwa nini sasa ulipiga picha wakati ulijua lile ni somo ulikuwa ukifundisha?

Mchungaji: Pale kanisani nikitoa mafunzo watu huwa wanapiga picha kwa simu zao tu na sikuwahi kuwakataza na mimi kila nikitoa somo huwa natoa na mifano mara nyingi tu lakini nilishangaa la siku hiyo lilinizulia mambo makubwa hadi najuta sasa.

Risasi Jumamosi: Je, baada ya kuonekana umekanyaga watu, maafisa wa haki za binadamu hawakukutafuta?

Mchungaji: Hakuna aliyenitafuta halafu ieleweke kuwa mimi pia ni mtu wa haki za binadamu kwa maana ya uchungaji wangu. Ila kwa shida niliyoipata siwezi kuutoa tena mfano huo, kwa kifupi nimekoma.

Risasi Jumamosi: Je tukio hilo halijakuondolea waumini kanisani?

Mchungaji: Halijaniathiri kivyovyote bali liliniongezea watu kwa sababu wengi walikuja kanisani kuona ninavyopandia watu, wengine walikuja kwa nia ya kunisema kwa kile nilichokifanya lakini mwisho wa siku walibaki na kuwa waumini wangu.

Risasi Jumamosi: Wapo wanaosema kanisa lako liko kimagumashi, halijasajiliwa na serikali, unasemaje kuhusu hilo?

Mchungaji: Kanisa langu liko kihalali kabisa na mimi si mchungaji wa jina bali nimesomea nchini Zambia.

Kanisa hilo la mchungaji Bethania ni moja ya makanisa ambayo kila kukicha watu wanayatolea macho kwa vitendo visivyokubalika lakini mwenyewe anadai kuwa ni kwa sababu hawahudhurii ibada na wengi wanapenda kuchafuliana majina.

STORI: HAMIDA HASSAN NA GLADNESS MALLYA, RISASI JUMAMOSI

Comments are closed.