The House of Favourite Newspapers

Mchungaji wa Mainda akamatwa

0

mchungajiMchungaji Boniface Godwin Mwamposa.

Makongoro Oging’ na Mayasa Mariwata
VIBALI noma! Mchungaji Boniface Godwin Mwamposa anayeendesha huduma ya Neno la Mungu kwenye ukumbi wa baa iliyosimama kufanya kazi, Vatican Hotel, Sinza Kijiweni, Dar amekamatwa na msajili wa vyama vya kijamii (yakiwemo makanisa) kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani na kufikishwa Kituo cha Polisi Kijitonyama ‘Mabatini’ jijini Dar kwa madai ya kutokuwa na vibali cha kufanya kazi hiyo.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, Desemba 8, mwaka huu, saa 12 jioni, mchungaji huyo alikamatwa akiwa katika eneo hilo akitoa mahubiri muda wa kazi, tena bila vibali kazi katika eneo hilo la baa. Msanii wa sinema za Bongo, Ruth Suka ‘Mainda’ anaabudu katika kanisa hilo.

1mainda Msanii wa sinema za Bongo, Ruth Suka ‘Mainda’.

Waandishi wetu walimtafuta mchungaji huyo ili kuonana naye laivu bila mafanikio, akapatikana kwenye simu na kuulizwa kuwepo kwa madai hayo ambapo alijibu kwa ukali:

“Sasa nikikwambia utapata faida gani? Achana na hayo mambo yameshapita, sioni haja ya kuyaongelea kwani lazima kila kitu kwenu kiwe habari?”

Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Kijamii Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Maurine Komba alipoulizwa, alisema mchungaji huyo alikuwa akifanya makosa makubwa kuendesha mahubiri katika eneo hilo tena muda wa kazi na kuwafanya watu washindwe kuwajibika ipasavyo katika majukumu mengine ya kujenga taifa.

“Huyo ni mfano kwa wengine kwani wapo wengi tu ambao wanaendesha huduma hizi pasipo kuwa na vibali, wajiandae tunawafungia kazi.

Huyo Mchungaji Boniface kanisa lake halina vibali wala yeye mwenyewe hana kibali na lile eneo si kanisa ni baa,” alisema Komba.

Alipoelezwa na mwandishi kuwa ibada inaweza kufanyika popote, alijibu:
“Hata kama ibada inaweza kufanyika popote lakini suala la kibali ni muhimu, lazima utambulike na serikali. Katika ukaguzi wetu tulipobaini hayo hatukuwa na muda wa kupoteza zaidi ya kumfungulia mashitaka. Atapanda kortini.”

Kutokana na sekeseke hilo, jalada la kesi limefunguliwa katika Kituo cha Polisi Mabatini kwa kumbukumbu namba KJN/RB/12684/15 KUFANYA MAHUBIRI BILA KIBALI.
Uwazi juzi, lilimtafuta Mainda kwa simu yake ya mkononi ili kutaka kusikia lolote kutoka kwake, lakini simu hiyo iliita bila kupokelewa.

Tangu aokoke miaka mitano iliyopita, Mainda ambaye zamani alijulikana kwa jina la Mwanaidi kabla ya Ruth, amekuwa akiabudu kwa mchungaji huyo huku kanisa hilo likizidi kuvuna kondoo (waumini) siku hadi siku.

Leave A Reply