The House of Favourite Newspapers

Mechi 1 Tu Simba Kimataifa, Wakiomba Yanga washinde Jumapili

1

NA MWANDISHI WETU | CHAMPIONI JUMATANO | HABARI

NI sahihi kusema kuwa Simba wataishangilia Yanga Jumapili kama wenyewe watakuwa wameshinda mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Azam.

Simba wanacheza na Azam Jumamosi kwenye mchezo wa Kombe la FA, hatua ya nusu fainali na kama wakipata ushindi hapo basi watakuwa wanawaomba Yanga washinde dhidi ya Mbao ili wawe na uhakika wa kucheza michuano ya kimataifa mwakani.

Kikosi cha Azam SC.

Simba hawajashiriki michuano ya kimataifa kwa miaka minne na hii itakuwa nafasi yao ya pekee kukwea pipa msimu ujao. Itakuwa hivi! Kama Simba wakiibuka na ushindi na kutinga kwenye hatua ya fainali ya michuano ya Kombe la FA, watakuwa wanasubiri Yanga wacheze na Mbao Jumapili, lakini wakiomba Yanga wapate ushindi kwa kuwa ndiyo timu ambayo wanawania nayo ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu na mojawapo kati ya timu hizo itatwaa ubingwa mwishoni mwa msimu.

Kikosi cha timu ya Mbao.

Endapo Yanga watashinda kwa Mbao watakwenda fainali kuvaana na Simba, lakini wote watakuwa hawana presha kwa kuwa watakwenda kwenye fainali ambayo timu zote zinapata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu unaofuata.

Kikosi cha timu ya Simba.

Kama Yanga wataifunga Simba kwenye mchezo huo, lakini Yanga haohao wakaja wakatwaa ubingwa wa Tanzania Bara, basi watawaachia Simba nafasi ya Kombe la Shirikisho kama walivyofanya msimu uliopita walipoifunga Azam, huku pia wakitwaa ubingwa wa Tanzania Bara.

Lakini kama Simba watashinda kwenye mchezo wa fainali, kisha wakatwaa ubingwa wa Kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara, basi hao wa Jangwani nafasi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Hii inaonyesha kuwa pia Yanga nao watakuwa wanaomba kwa nguvu zote Simba waifunge Azam Jumamosi, ili wakishinda wao Jumapili wakutane na Simba kwenye fainali baada ya mmoja wao kuwa ameshatwaa ubingwa wa ligi.

Kama Azam watatinga fainali na Yanga, halafu Yanga wakakosa ubingwa wa Bara, basi fainali hiyo itakuwa hatari kuliko nyingine zote za michuano ya FA tangu imeanzishwa kwa kuwa timu zote zitakuwa zinatafuta nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa kwa kuwa Azam kwa sasa hawana uwezo wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Simba kwa sasa ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 59 huku  ikiwa na michezo miwili mbele ya Yanga ambao wapo nafasi ya pili na pointi 56.

Leave A Reply