Mechi ya Kihistoria: Simba na Stellenbosch Vita Ya Fainali
Kikosi cha Simba SC kinatarajiwa kuwakaribisha wageni kutoka Afrika Kusini, Stellenbosch FC, katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar, leo majira ya saa 10:00 jioni. Mchezo huu ni sehemu ya hatua ya mtoano ya mashindano yanayoendelea kwa kasi barani Afrika.
Timu zote mbili zinaingia uwanjani zikiwa na rekodi nzuri na vikosi vyenye nyota mahiri wanaotarajiwa kuamua matokeo ya mchezo huo.
Kwa upande wa Simba SC, macho yote yataelekezwa kwa Elie Mpanzu, ambaye aliweka bao muhimu kwenye mchezo wa robo fainali dhidi ya Al Masry, akifungua dimba kwa goli maridadi. Aidha, Kibu Denis naye anasifiwa kwa mchango wake mkubwa katika michuano hii, hasa baada ya kuiwezesha Simba kutinga hatua ya robo fainali kwa goli la dakika za lala salama dhidi ya SC Faxien FC.
Stellenbosch FC nao hawako nyuma. Wanajivunia kuwa na mshambuliaji Andre De Jong, aliyetikisa nyavu mara mbili katika mchezo wa hatua ya makundi dhidi ya Lunda Sul, na kuwapa alama tatu muhimu. Nyota mwingine wa kuangaliwa ni Devin Titus, aliyefunga dhidi ya Stade Malien na ambaye pia amewahi kuichezea timu ya taifa ya Afrika Kusini, Bafana Bafana.
Timu zote zinaingia katika mchezo huu zikiwa na motisha kubwa. Stellenbosch walipata ushindi wa kuvutia wa bao 1-0 dhidi ya Zamalek FC kule nchini Misri katika hatua ya robo fainali – ushindi unaowapa morali ya hali ya juu.