The House of Favourite Newspapers

Meja Jenerali Mstaafu January Kisanko afariki

0

KISANKO

Meja Jenerali January Claudio Kisanko (mstaafu) enzi za uhai wake.

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linasikitika kutangaza kifo cha Meja Jenerali January Claudio Kisanko (mstaafu) kilichotokea tarehe 21 Machi 2016.

Meja Jenerali January Kisanko (mstaafu) alizaliwa mwaka 1945 katika kijiji cha Mkima, Tarafa ya Lyangalile, Wilaya ya Sumbawanga. Alipata Elimu ya Msingi Mkoani Rukwa na baadaye elimu ya Sekondari katika Shule ya Sekondari ya wavulana Agakhan ambayo kwa sasa ni shule ya Sekondari Tambaza, hadi alipohitimu kidato cha Sita mwaka 1966.

Marehemu Meja Jenerali January Claudio Kisanko (Mstaafu) alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania tarehe 31 Mei, 1967 na kutunukiwa Kamisheni tarehe 24 Julai, 1969. Marehemu alilitumikia Jeshi kwa muda wa miaka 35 na mwezi 1 hadi alipostaafu utumishi Jeshini tarehe 30 Juni 2002.

Katika utumishi wake marehemu alishika Madaraka mbalimbali Ikiwemo Kamanda wa patuni Nachingwea 1969 hadi 1970, Kamishina wa Mipango na Sera katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa 2001, madaraka ambayo alikuwa nayo hadi alipostaafu tarehe 30 Juni 2002.

Marehemu Meja Jenerali January Kisanko (Mstaafu) alifariki dunia tarehe 21 Machi, 2016 katika Hospitali ya TMJ Dar es salaam. Ameacha Mke na Watoto. Mwili wa marehemu unatarajiwa kuagwa rasmi tarehe 28 Machi, 2016 kuanzia saa 3:00 asubuhi katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo na mazishi yatafanyika katika makaburi ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam, saa 10:00 jioni.

MUNGU AILAZE MAHALI PEMA PEPONI ROHO YA MAREHEMU MEJA JENERALI JANUARY KISANKO (MSTAAFU) AMINA

Imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Mahusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
S.L.P 9203, Dar es Salaam, Tanzania.
Kwa Mawasiliano zaidi: 0784-477638

Leave A Reply