The House of Favourite Newspapers

Meja Jenerali Msuya; alivyokufa na kufufuka-10

0

ILIPOISHIA…
Nikiwa bado nahangaika kujua kilichokuwa kinanitokea, mkono wenye nguvu kubwa ulinikamata na kunipeleka upande mmoja. Mara nilijikuta nikiwa katika ukumbi mkubwa uliokuwa umemulikwa na taa za aina mbalimbali. ENDELEA…
Sehemu hii ilikuwa inapendeza kuliko maelezo na yenye utulivu mkubwa. Ukumbi ulikuwa umejaa watu waliokuwa wanaonekana wazi lakini sura zao zilikuwa hazionekani. Niliweza kumwona mtu aliyenivuta kunipeleka katika ukumbi huo. Alikuwa pia hana taswira ya uso lakini alikuwa na umbo kubwa.

Kwa haraka nilitambua kwamba eneo nililokuwepo lilikuwa mbinguni; hivyo nilitazama kila upande wangu kuona iwapo kulikuwa na mtu ambaye ningemtambua au kukikuta Kiti cha Huruma (Mercy Seat) lakini sikufanikiwa.
Mtu huyu aliyekuwa amesimama kando yangu alisema ‘njoo.  Nataka kukuonesha kitu fulani’. Tukiwa tumeshikana mikono, tulipanda ngazi kadhaa ambapo huko juu magogo ambayo yalikuwa mihimili iliosimama yakiwa yameunganishwa kwa komeo kubwa. Aliniambia ‘hiki ndicho kituo kikuu cha banda la Mungu’.

Kituo hiki kinajulikana kwangu kama kituo cha Benjamin na kwa vile umefika hapa ni hakika hutakufa sasa,  kisha akaushika  mkono wangu tena na kunirudisha kwenye ukumbi.  Sauti nyingine ikaniita kwa jina langu. Sauti hii ilikuwa ya nguvu na mamlaka zaidi. Ilisema ‘unaliona geti lile?’
Nilijibu ‘ndiyo’.  Kisha aliendelea kusema kwamba ‘lile ni geti la kuelekea kuzimuni. Kila anayesimama mbele ya kiti cha huruma na kuhukumiwa kuwa hakuwa mwadilifu, au kama aliendesha maisha ya dhambi hutupwa kupitia geti hilo na kutumbukia kuzimuni.

Nikiwa naendelea kuyashangalia maajabu ya mbinguni, sauti ile yenye nguvu iliniita kwa jina langu tena na kuniamuru kwenda kuliunga geti lile. Nilijibu kwa kusema kwamba nilikuwa sina ufundi wa kutia weko (welding).    Alisema  ‘nitakupa watu wa kukusaidia kutekeleza jukumu hilo’; kisha mtu huyo aliyekuwa karibu yangu aliubeba mkono wangu na kuniongoza kuelekea katika geti hili. Lilikuwa na umbo la yai ambapo sehemu yake ya chini ilikuwa imekatwa kuonekana kama jukwaa.

Kwangu lilinipa taswira kama ile ambayo huwa ya nyuma ya ndege kubwa.  Kama vile bomba la kutolela moshi. Kwa upande wa kulia, kulikuwa na rundo la mabamba manene ya chuma na kwa upande wa kushoto kulikuwa na watu sita kama nilivyokuwa nimeahidiwa kuwaona.

Niliwaamuru kuyakata mabamba ya chuma ili yaweze kuingia kwenye upenyo uliokuwepo. Taratibu tuliyakata kwa kutumia chombo maalum, kisha tukayaunganisha kwa weko (welding) ili kuliziba geti hilo. Tulipopita, niligeuka kuona nilipokuwa  ili kumwona yule mtu aliyenipa jukumu hilo ili nimjulishe kuimaliza kazi hiyo.

Kwa bahati mbaya sikutazama mbali sana kwani mtu huyo alikuwa palepale nyuma yangu. Alisema ‘umefanya kazi nzuri’ na akaukamata mkono wangu na kunirudisha katikati ya ukumbi.

Nikiwa nimesimama pale na yule kibonge cha mtu akiwa bado karibu yangu, sauti yenye mamlaka iliita jina langu: ‘Benjamin!  Ninataka urejee duniani na kuwaambia watu wangu kwamba nimeridhika na ufahamu wao wa Biblia; ufahamu wa mema na mabaya na tofauti ya uadilifu na dhambi; na kwamba wanazifahamu vyema amri zangu.

‘Neno langu sasa limemfikia kila mtu katika kona zote za dunia.  Wanaopinga au kukataa maelekezo yangu na kumkataa Mwanangu Yesu Kristo wanafanya hivyo wakati wanafahamu vyema kutoka ndani ya mioyo yao UKWELI kwamba Yesu ni Masiha. Watakumbana na yale yatakayowapata.  Waambie kwamba tangu na kuendelea hapatakuwa na hukumu tena mbinguni. Watu watajihukumu wenyewe kufuatana na uchaguzi wanaoufanya maishani.  ‘Anayetaka kuja mbinguni lazima aishi maisha ya uadilifu, aheshimu na kufuata amri zangu na maagizo yangu.

‘Anayenikataa na kupuuza maelekezo yangu akafanya dhambi na kufuata matakwa ya miungu wengine, ni dhahiri atakwenda moja kwa moja jehanamu wakati wa mwisho ukifika; lakini wale ambao watafuata neno langu na kuishi kwa unyenyekevu wataingia katika ufalme wangu wa milele; hawatakiona kifo.’

Kisha akaniamuru kwa kusema ‘nenda!  Nenda sasa na ufanye kama nilivyokueleza’.  Upepo wenye baridi kali ukanipiga na ghafla, nilifungua macho yangu na kumwona Jenerali Sarakikya akiwa amesimama kando ya kitanda changu na mwanangu Bis akiwa amesimama upande wa miguuni kwangu.

Kila mtu, madaktari, manesi na mke wangu na wanangu, wakashangaa.  Ulikuwa ni muujiza uliofunguka mbele yao. Kwa mtu aliyekuwa amekufa kwa siku nne na nusu, huo ulikuwa ni muujiza wa Mungu. Madaktari walinipeleka haraka kwenye sehemu ya kusafishia damu na wakati wakisafisha damu yangu, waliirudisha pia mipira yote waliyoitoa baada ya kukata tamaa.

Nilirejeshwa katika matibabu kamili na habari ikaenea hospitalini hapo kwamba nilikuwa nimerejewa na uhai kimiujiza. Mara moja nikawa mgonjwa maarufu zaidi katika hospitali hiyo. Wakati napitishwa katika sehemu mbalimbali za hospitali hiyo ya Heartland, manesi walinikimbilia na kunisalimia, wakishangazwa na muujiza huo.

Ni vizuri kufahamu kwamba binadamu kwanza kabisa ni kiumbe kwa maana kwamba ni roho. Pili, ni mtu, kwa maana kwamba ana mwili uliotengenezwa kwa ‘mboji’, udongo wa mfinyanzi au uchafu.  Ni roho ndiyo huweka uhai katika mwili.  Roho inapoondoka, mwili hufa.

Je, kilijiri nini baada ya Meja Jenerali Msuya kufufuka? Usikose mwendelezo wake katika Gazeti la Risasi Jumamosi siku ya Jumamosi.

SOCIAL MEDIA ZETU:

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz

Leave A Reply