The House of Favourite Newspapers

Merciless Billionaires – 59

0

INSPEKTA Masala amefanikiwa kuwaokoa wapelelezi waliokuja kutoka Marekani kwa lengo la kumsaidia kuwakamata Dk Viola na nduguye Vanessa, wauaji hatari ambao kwa muda mrefu wametafutwa bila mafanikio kumbe walikuwa wakiishi nchini Tanzania ambako walinunua kisiwa na kuwekeza fedha nyingi kwa kujenga mji wa kisasa wenye kila aina ya starehe.

Serikali ya Tanzania haikuwahi kabisa kugundua kwamba watu hao ni wauaji waliokuwa wakisakwa, bali iliwachukulia kama wawekezaji na kuwapa kila aina ya upendeleo ikiwa ni pamoja na uraia wa nchi hiyo wakiamini walikuwa ni Wajapan kumbe wameshabadili sura zao nchini Thailand na kuonekana hivyo kwa lengo la kukimbia mkono wa sheria.

Inspekta Masala kaanika kila kitu, hakuna anayeonekana kuamini kwamba Dk Viola na nduguye Vanessa wamekamatwa wakitumia  majina bandia ya Jonathan na Andrew. Dunia nzima imepatwa na mshtuko baada ya habari hizo kusambaa kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

Je, nini kitaendelea? SONGA NAYO…

MIILI yote ya wauaji wa kukodiwa na Dk Viola na Vanessa ilizikwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwenye makaburi ya Kigogo, Dk Viola na Vanessa walihojiwa Kituo cha Kati cha Polisi lakini hawakutaka kuongea chochote, wakishinikiza ni lazima mwanasheria wa kampuni yao awepo wakati wakitoa maelezo yao.

Bahati mbaya mwanasheria wao alikuwa amesafiri nje ya nchi, hivyo wakalazimika kutupwa mahabusu hivyohivyo bila kutoa maelezo yoyote, tukio hili lilikuwa tayari limeshakua maarufu dunia nzima ndani ya muda mfupi, watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia ambao ndugu zao walikufa katika ajali ya ndege iliyowapatia Dk Viola na nduguye Vanessa utajiri haramu wa dola milioni 620 walimiminika nchini Tanzania kila siku kuja kuwaona wauaji hao hatari.

Kila mtu alitaka watu hao wafikishwe haraka mahakamani na kesi yao ipelekwe kwa kasi ili wahukumiwe kifo haraka iwezekanavyo, baadhi ya Wazungu walipendekeza kesi hiyo ihamishwe Tanzania na kupelekwa katika nchi iliyokuwa na sheria kali lilipokuja suala la mauaji kama vile Uingereza, lakini pendekezo hilo halikupokewa, Serikali ya Tanzania ilikubali kubeba mzigo wa kuiendesha kesi hiyo mpaka mwisho hasa baada ya kugundulika kuwa Dk Viola na Vanessa walikuwa ni Watanzania waliobadilisha sura zao kuonekana Wajapan kwa lengo la kuukimbia mkono wa sheria.

John Mbwambo, mwanasheria maarufu nchini Tanzania, akifanya kazi na kampuni binafsi ya Uwakili ya Mbwambo Advocates and Co, ndiye alikuwa mwanasheria wa Dk Viola na Vanessa katika kampuni yao iliyofanya uwekezaji kwenye Kisiwa cha Bongoyo, aliposoma habari hiyo mtandaoni aliamua kukatisha safari yake katika Jiji la CapeTown huko Afrika Kusini alikokuwa amekwenda kwenye mkutano na kurejea Tanzania haraka iwezekanavyo.

Kitu cha kwanza alipowasili Tanzania ni kwenda moja kwa moja ofisini kwake ambako alipewa taarifa za tukio hilo kisha kuondoka kwenda moja kwa moja Gereza la Segerea ambako Dk Viola na Vanessa walikuwa wamewekwa mahabusu, alijitambulisha na kuomba kuwaona, watu wengi walikuwa nje ya gereza na walifika kwa lengo la kuwaona watu hao lakini hawakuruhusiwa, alipojitambulisha kama mwanasheria wao, bwana Mbwambo aliruhusiwa bila kizuizi chochote na kupelekwa kwenye chumba maalum baada ya kupekuliwa ambako Dk Viola na Vanessa waliungana naye muda mfupi baadaye.

“Poleni!”

“Hakuna sababu ya kutupa pole, tulijua jambo hili lingetokea maishani mwetu, tumejitahidi sana kulizuia lakini imeshindikana!”

“Ni kweli ninyi ni Dk Viola na Vanessa?”

“Ni kweli, wewe lazima tukuambie ukweli, maana ni mwanasheria wetu, tukikudanganya wewe tutakuwa tunajidanganya wenyewe.”

“Ni kweli ninyi ni wanawake?”

“Kabisa.”

“Ilikuwaje mkawa hivyo?”

“Tulibadili sura na muonekano kwa lengo la kujificha!”

“Mliua watu wote mnaodaiwa kuwaua?”

“Hakuna uongo hata mmoja,” alijibu Dk Viola, vinyweleo vikamsimama mwanasheria wao, alishasoma sana juu ya Dk Viola na Vanessa lakini hakujua kwamba watu hao kumbe walikuwa ni wateja wake, hakika hofu ilimwingia.

“Mh!” akaguna.

“Mbona umeguna?”

“Siwafichi, nimeshangaa.”

“Wala usishangae, unachotakiwa kufanya ni kutuokoa na hili janga kama unaweza, iwapo ni kubwa sana kwako, utueleze sisi tutafute mawakili wengine duniani, maana fedha za kutosha tunazo, hatuko tayari kufa na kuacha utajiri wetu nyuma, tumetafuta fedha kwa muda mrefu, kazi yake ni kutusaidia na wakati wa kuzitumia ndiyo sasa!”

“Mh!”

“Kama huna uwezo sema!”

“Nipeni muda nikafikirie.”

“Mpaka lini?”

“Kesho saa nne asubuhi nitakuwa hapa.”

“Hakuna shida, unaweza kuondoka,” Vanessa aliongea huku akisimama, uso wake ukiwa umebadilika na alionekana mwenye hasira.

“Lakini kwa nini mlifanya mambo haya?”

“Ni shetani tu, tamaa! Maana tulizaliwa kwenye umaskini mkubwa na tukaapa kwamba maishani mwetu ni lazima tuwe mabilionea kwa gharama yoyote, tukafanya dhambi kubwa ya kuua watu, hatukuwa na hekima wakati tunachagua kufanya jambo hili, tunahitaji msaada wako kama mwanasheria wetu!”

“Acheni nikafikirie!”

“Kama ukifanikiwa kutuokoa na kifo, malipo yako yatakuwa nusu ya utajiri wetu.”

“Sasa hivi unafikia kiasi gani?”

“Dola bilioni moja!”

“Kwa hiyo mnaamanisha nitapata dola milioni mia tano?”

“Ndiyo.”

“Mko tayari kusaini?”

“Kabisa, wakati wowote!”

“Basi nitakuja kesho, tutaongea vizuri.”

Mwanasheria Mbwambo aliondoka gerezani akiwa mwenye mawazo mengi kichwani  mwake, tangu aifanye kazi ya uanasheria kwa miaka zaidi ya thelathini hakuwahi kukutana  na kesi mbaya kiasi hicho, alitakiwa kuwatetea watu ambao hakika waliua makumi ya watu, lakini kwa upande mwingine aliuhitaji utajiri wa dola milioni mia tano, fedha ambazo hata angefanya kazi usiku na mchana kwa miaka elfu moja asingezipata, kwake aliona tukio hilo kama bahati.

Kitu cha kwanza alichokifanya baada tu ya kuingia ofisini kwake ni kuingia mtandaoni na kutafuta kampuni za uanasheria zenye umaarufu duniani, akapata tatu lakini kati ya hizo akaona moja iliyoitwa American Law Barristers yenye makao yake makuu jijini New York lakini ikiwa na ofisi karibu katika nchi zote duniani isipokuwa Tanzania.

“Hawa watanifaa, najua baada ya kesi hii kwisha nitakuwa nimepata wabia!” aliwaza huku akiandika barua pepe kwa kampuni hiyo.

Jioni hiyohiyo alipata majibu kutoka New York, mkurugenzi wa kampuni hiyo, bwana Denis Crapton, akitaka kuzungumza naye kwa kutumia Mtandao wa Skype ambao wazungumzaji huonana moja kwa moja kupitia kompyuta, katika mazungumzo yao alielezea undani wa suala zima na malipo ambayo washtakiwa walikuwa tayari kuyalipa kama  mtu angewaepusha na kifo.

“Una uhakika watalipa dola milioni mia tano?”

“Ni matajiri wakubwa, hawatanii, najua wanamaanisha wanachokisema.”

“Kweli?”

“Kabisa.”

“Unaweza kuingia nao mkataba wa mwanzo ambao utanifanya mimi na wenzangu tuwe na uhakika kisha tusafiri kuja nchini Tanzania kuonana nao?”

“Haina shida, nakutana nao siku ya kesho.”

“Fanya hivyo halafu unijulishe.”

“Ahsante!”

Simu ikakatwa na bwana Mbwambo akajiegemeza kwenye kiti ofisini kwake, akitafakari juu ya tukio hilo, hakika alikuwa hafanyi kitu sahihi kwa watu wote ambao Dk Viola na Vanessa waliwaua lakini alijikuta hana jinsi zaidi ya kuwatetea watu hao hatari sababu tu alihitaji utajiri wao.

Siku iliyofuata kama alivyoahidi alifika gerezani na kukutana na wateja wake, kazi ilikuwa moja tu kusainisha nao mkataba wa mwanzo wa kukubaliana kuwatetea kwa malipo ya dola milioni mia tano, baada ya hapo ndipo mwanasheria akawaruhusu kuongea na polisi ambao walifika siku hiyohiyo na kufanya nao mahojiano, wakakanusha kushiriki katika mauaji yoyote.

“Lakini ninyi ni Watanzania?”

“Ndiyo.”

“Na wewe ulikuwa daktari uliyekuwa ukiishi kwenye nyumba ambayo baadaye uliibomoa na kupanda bustani uliyoikabidhi kwa jiji?”

“Afande maswali mengine nitakutana nayo mahakamani, wewe chukua maelezo yangu ya kwamba sikufanya mauaji yoyote,” Vanessa alimalizia.

“Tuliyokwisha kukueleza ndiyo maelezo yetu, hakuna zaidi, tukutane mahakamani,” Dk Viola akaongezea, baada ya hapo hawakutaka kuongea kitu kingine zaidi.

JE, nini kitaendelea katika kesi hii ambayo itaanza kuunguruma kuanzia Jumatatu? Fuatilia Gazeti la Championi Jumatatu.

Leave A Reply