The House of Favourite Newspapers

Merciless Billionaires – 63

0

DK Viola na pacha wake Vanessa wako katika wakati mgumu, kesi za mauaji zinazowakabili mahakamani zinaonekana kuwalemea kwani ushahidi uliotolewa dhidi yao ni mgumu mno na hauna namna ambayo upande wa utetezi unaweza kuitumia kuwaweka huru.

Wanawake hawa wawili ni mabilionea, walizaliwa masikini sana, wakaapa kutokufa masikini kama walivyozaliwa na kusema wangetafuta fedha kwa namna yoyote mpaka watajirike.

Kiapo hiki kilikuwa kibaya kwani kiliwafanya wajikute wakitumia elimu yao kwa njia haramu kujipatia utajiri, Viola akasoma na kuwa daktari bingwa wa figo, elimu ambayo badala ya kuitumia kuokoa maisha ya watu, aliitumia kuwaibia watu figo miilini mwao na kuziuza kwa matajiri waliokuwa wakiugua figo sehemu mbalimbali za dunia, bei ya figo moja ikifika mpaka dola milioni moja.

Biashara hii haramu ilimpa Viola fedha nyingi huku akiua makumi ya watu na kuwafukia chini ya jumba lake kubwa.

Vanessa alisoma na kuwa mhandisi wa ndege, akaajiriwa na Shirika la Ndege la Brito Africa Airline kama mhandisi mkuu, yeye na nduguye kwa tamaa ya fedha wakapanga kuiangusha ndege, ndani yake wakiwa wamewapakia watoto yatima 62 kutoka Tanzania ambao wiki mbili kabla ya safari hiyo waliwawekea bima na Viola kujitaja kama mrithi wa fidia yao, ndege ilipoanguka na watoto hao kufa, Viola alilipwa dola milioni 620, kwani  fidia kwa kila mtoto ilikuwa dola milioni kumi, wakawa mabilionea.

Ili kuikimbia dhambi yao, walitoroka kwenda Thailand ambako walibadili sura zao na kufanana na wazee wa Kijapan, ndipo wakarejea Tanzania na hati za kusafiri za Thailand kama wawekezaji bila mtu yeyote kuwagundua na kununua Kisiwa cha Bongoyo ambako waliwekeza fedha nyingi kwa kujenga mji wa kisasa uliopewa jina la New Dar es Salaam City.

Inspekta Masala, mpelelezi wa kimataifa, raia wa Tanzania ndiye aliyewagundua watu hao, akawakamata na sasa wapo mahakamani, kesi yao ikiendelea!

Je, nini kitaendelea? SONGA NAYO…

MWILI wa Vanessa ulikuwa ukitikisika kama vile awavyo mtu mwenye homa kali, hofu ilikuwa imemgubika, hapakuwa tena na nafasi ya yeye na ndugu yake kukiepuka kitanzi! Mambo yalikwenda tofauti kabisa na walivyotarajia, kwa ushahidi uliokuwepo, lazima wangenyongwa, ulikuwa mzigo mzito mno usiopingika.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Dk Viola, alikiona kitanzi kikining’inia mbele ya kichwa chake, lazima yeye na nduguye wangenyongwa kwa mauaji ya mtungo waliyoyafanya! Kila walipowaangalia watu ndani ya chumba cha mahakama walionekana kama wanasema, “Wanyonge wauaji hao” nyuso zao hazikuonyesha huruma hata kidogo.

“Kama hakuna swali la ziada naahirisha kesi hii mpaka siku ya tarehe 26 Agosti, wiki mbili kuanzia sasa, ambapo upande wa mashtaka utakamilisha kuwahoji mashahidi wake kabla upande wa utetezi haujaanza kuwatetea washtakiwa!” Jaji aliongea kwa sauti ya chini akikusanya makabrasha yake mezani, alipomaliza alinyanyuka na watu wote mahakamani wakanyanyuka, akatembea taratibu kwenda nje ya chumba cha mahakama.

Nyuma yake, Dk Viola na Vanessa waliondolewa pia chini ya ulinzi mkali, mawakili wao wakiwafuata kwa nyuma hadi kwenye chumba maalum ambamo waliomba kuongea nao juu ya kilichojitokeza mahakamani, kweli vichwani mwa mawakili walifikiria sana dola milioni mia tano walizokuwa wameahidiwa lakini kwa hali ilivyokuwa, walionekana kukata tamaa, kesi kwao ilionekana ngumu.

“Fanyeni chochote kinachowezekana kuweza kutusaidia, vinginevyo tutanyongwa, kesi hii ni ngumu sana, tuna fedha nyingi na utajiri mkubwa ambao tumeutafuta kwa miaka mingi na hatujaufaidi, hatutaki kufa na kuacha utajiri wetu nyuma, maana hatuna hata mtoto wa kurithi!”

“Kweli kesi ni ngumu, hata mimi nashindwa kuelewa ni kitu gani tunaweza kufanya!”

“Fedha tunazitaka, lakini kwa ushahidi mzito uliotolewa ninashindwa kuelewa tutatumia maneno gani kwenye utetezi ili tuweze kuwaweka huru!”

“Vinginevyo tulazimike kutumia sehemu ya fedha zenu kurubuni watu ili haki ipindishwe!”

“Hiyo haina tatizo, tuko tayari kutumia kiasi chochote cha fedha ili mradi tu tuwe huru!”

“Mambo mawili yanaweza kufanyika tukiwa na fedha za kutosha, la kwanza ni kuhakikisha vielelezo vyote vinapotea, la pili ni kuwahonga watendaji wote wa mahakama na la tatu ni kuwatorosha kabla ya kunyongwa maana kwa inavyoonekana hukumu ya kifo haikwepeki!”

“Hatutaki kutoroshwa, maana mwisho wa siku tutaishi maisha ya kukimbiakimbia bila kufaidi utajiri wetu, kinachotakiwa hapa ni kutumia fedha ili kesi imalizike!”

“Basi tufanye aidha kupoteza ushahidi au kuhonga watumishi wa mahakama au mambo yote mawili.”

“Tufanye yote mawili!”

“Mnahitaji fedha kiasi gani?”

“Dola laki moja hivi kwa kuanzia.”

“Akaunti yetu inaweza kutoa dola elfu kumi kwa siku, bahati mbaya tuko gerezani hatuwezi kuwatolea hizo fedha, mnachoweza kufanya ni kwenda hadi Bongoyo kisiwani, kwenye Benki ya Wezesha Mzawa Commercial, mkiwa hapo mtatumia kadi ya benki mtakayoichukua ofisini kwangu kwenye droo, kisha mtakuwa mnachukua dola elfu kumi kila siku kwa siku kumi kwenye akaunti yangu!”

“Namba yako ya siri?”

“4142!”

“Ni hiyo tu?”

“Kabisa, tafadhali fanyeni kila kinachowezekana ili tunusurike na mdomo wa kaburi,” Dk Viola aliongea na mwisho wakaagana na askari wakawachukua kuwapakia kwenye karandinga huku watu wakiwazomea bila kujali walikuwa mahakamani.
Walikuwa wamekata tamaa kabisa, fedha na utajiri walioutafuta kwa njia haramu ulionekana kutowapa faida yoyote, kweli walifanikiwa kutimiza ndoto ya kuwa mabilionea kama walivyoapa wakiwa watoto wadogo, lakini mwisho wa siku walikuwa mikononi mwa sheria wakikabiliana na kesi ya mauaji. Kila kitu kilikuwa kimebadilika, ndoto yao ya kufaidi utajiri ilikuwa imeyeyuka, sasa walikuwa wakihangaika kukwepa kitanzi.

***

Mawakili Denis Crapton na Mbwambo waliondoka moja kwa moja mahakamani na kwenda hadi kivukoni, wakiwa ndani ya gari aina ya SUV, Anganile akiendesha, njia nzima walipanga jinsi ya kuzipata dola milioni mia tano, hawakuona njia nyingine ya kuwafanya wawe mamilionea zaidi ya kuteketeza vielelezo ama kuhonga watumishi wa mahakama katika taifa kama Tanzania ambalo rushwa ilitawala na haki mahakamani mara nyingi ilipindishwa ili mradi mtu alikuwa na fedha.

“Lakini macho ya mataifa mengi duniani yanaifuatilia sana kesi hii!”

“Ni kweli!”

“Itawezekana kweli kupindisha sheria wakati wapo na raia wa Marekani waliokufa kwenye ajali ya ndege, Marekani haitakubali.”

“Tufanye kinachowezekana, tusikubali kushindwa kabla ya kufanya.”

“Sawa!”

Tayari walishafika kivukoni, boti ilikuwepo, wakapanda pamoja na magari ya watu wengine na nusu saa tu baadaye walishafika kisiwani Bongoyo wakaendesha hadi kwenye jengo la ofisi ya Dk Viola na Vanessa, ambako waliegesha na kupandisha kwa kutumia lifti hadi kwenye ghorofa ambalo ofisi hiyo ilikuwepo, Katibu Muhtasi aliwakaribisha na walipojitambulisha, akawaeleza kwamba alipokea simu kutoka kwa mkuu wa gereza kwamba wangefika na awaruhusu waingie ofisini kwa mabosi wake.

“Ahsante sana.”

“Karibuni ingieni.”

Walizama moja kwa moja ofisini na kuanza kupekua kwenye droo ya meza kubwa, hawakuchukua muda mrefu sana wakaiona kadi ya benki na kuichukua, wakatoka mara moja hadi kwa Katibu Muhtasi ambaye walimuaga na kuondoka zao kutumia lifti hadi chini ambako walichukua gari na kuanza safari kuelekea benki ya Wezesha Mzawa, huko waliingia moja kwa moja kwenye mashine ya kutolea fedha na kuingiza kadi.

“Ile namba alisema ni ngapi kweli?” Wakili Mbwambo alimuuliza mwenzake.

“4142!”

“Ahsante ilitaka kunitoka kidogo.”

Haraka akaingiza namba hiyo na haukupita muda mrefu sana fedha za Kitanzania zenye thamani ya dola elfu kumi zikaanza kutoka baada ya kuandika kiasi kilichohitajika, zoezi hilo lilipokamilika waliondoka moja kwa moja hadi ofisini ambako walianza kupanga mikakati ya kupoteza vielelezo, wakagundua walihitaji zaidi ya dola elfu kumi na tano kwa  kazi ya siku ya kwanza na walizokuwa nazo zilikuwa sawa na dola elfu kumi.

“Tunaweza kuchukua kwenye akaunti yangu halafu kesho tukichukua kwenye akaunti yao tukazirejesha,” Wakili Mbwambo alisema.

“Kwani siku huwa inaanza saa ngapi?”

“Saa sita.”

“Hivi sasa ni saa ngapi?”

“Saa moja usiku.”

“Kuna saa tano tu kabla siku nyingine mpya haijaanza ili tuweze kuchukua dola elfu kumi nyingine, kwani hatuwezi kusubiri?”

“Tunaweza.”

Wakakubaliana na kubaki ofisini wakiandika mambo mbalimbali juu ya utetezi wa kesi hiyo kama wangefanikiwa kupoteza vielelezo na kuwahonga watumishi wa mahakama, ilionekana ni kazi ngumu kupata maneno ya kutosha ambayo yangesaidia kuwaweka Dk  Viola na nduguye Vanessa huru.

“Tunachoweza kufanya baada ya vielelezo vyote kupotea ni kuvikana, pia kuwakataa wale watoto yatima waliotoa ushahidi wakiwa hawana figo moja!”

“Na kuhusu suala la fedha zilizoingia kwenye akaunti yao kutoka Kampuni ya Bima kama fidia kwa watoto 62?” wakili Mbwambo aliuliza.

“Pia tutazikana, kwa sababu hata wateja wetu hawakujibu hayo maswali, walibaki kimya, tutakachofanya ni kwenda kwenye mifumo ya benki na kupoteza hizo kumbukumbu, hayo yakifanyika tutakuwa tumepunguza ugumu wa kesi!”

“Kwa upande wa ndege kuanguka maana Vanessa alionekana kabisa akiwa na boksi la Xplo-Corrosive ambayo ni kemikali ya kulipuka akiingia nayo kwenye ndege!”

“Tukishaipoteza ile video, hapatakuwa tena na ushahidi mwingine wa kuthibitisha kwamba aliingia na kemikali hiyo kwenye ndege, tutakanusha tu!” Wakili Denis Crapton alisema.

Mwisho wa maongezi yao ikiwa imefika saa sita na dakika ishirini usiku, walikubaliana kuchukua hatua hiyo, wakaondoka ofisini kwenda tena kwenye Tawi la Benki la Wezesha Mzawa ambako walifanikiwa kuchukua dola elfu kumi nyingine lakini katika shilingi, fedha ya kufanyia kazi ya mwanzo ya kupoteza vielelezo ikawa imekamilika.

***

Hakuna mtu aliyeamini, watu walipomiminika mahakamani asubuhi hiyo na kukuta jengo la mahakama kuu likiwa limeteketea kwa moto, walinzi walidai ulianzia kwenye chumba cha kuhifadhia vielelezo na watalaam wa moto walipofika walidai ilikuwa ni shoti ya umeme! Uongozi wote wa mahakama ulipagawa kwani kulikuwa na vielelezo muhimu mno vya kesi vya wauaji ambao dunia nzima ilikuwa ikiwafuatilia!

“Mungu wangu tutafanya nini?” Jaji Kabengwe Lupilia alisema akiwa ameshika mikono kichwani.

JE, nini kitaendelea? Mipango hii itafanikiwa? Fuatilia wiki ijayo siku ya Jumatatu katika Gazeti la Championi Jumatatu.

Leave A Reply