Messi Ashinda Ubingwa wa 46 Akiwa na Inter Miami
Mshambuliaji wa Inter Miami ya Marekani na Timu ya Taifa ya Argentina, Lionel Messi (37) usiku wa kuamkia leo Alhamisi aliiwezesha timu yake kupata ushindi dhidi ya Columbus Crew uliowawezesha kutwaa kombe la Ngao ya Mashabiki.
Katika mchezo huo, Messi alifunga magoli mawili katika ushindi wa mabao 3-2 huku bao lingine la Inter Miami likiwekwa kimiani na mshambuliaji raia wa Uruguay, Luis Suarez, huku magoli ya Columbus crew waliokuwa nyumbani yakifungwa na Diego Rossi pamoja na Cucho Hernandez.
Ubingwa huo unakuwa ni taji la 46 kwa nyota wa timu hio, Lionel Messi ambae amewahi kutamba na klabu ya Barcelona na kushinda mataji mengi pamoja na tuzo binafsi kabla ya kuhamia PSG ya Ufaransa kisha Inter Miami alipo hadi sasa.
“Ukweli ni kwamba tuna furaha kufanikisha lengo la kwanza na sasa tunafikiria kuhusu kitakachokuja” Alisema Lionel Messi katika mahojiano baada ya mchezo na Apple TV.
Kwa ubingwa huo, Messi anaendelea kuwa kinara kwa mchezaji mwenye makombe mengi zaidi akifuatiwa na Dani Alves mwenye mataji 43.
Messi hadi sasa katika Ligi Kuu ya Marekani, MLS, amepachika mabao 17 na pasi za magoli 15 katika michezo 17 aliyoshuka dimbani msimu huu na kuiwezesha timu yake kuendelea kusalia kileleni mwa Ligi hio wakiwa na alama 68 katika michezo 32 hadi sasa.