Kartra

Metacha Wa Yanga Atajwa Kuingia Anga Za Simba

IMEELEZWA kuwa kipa namba moja wa Klabu ya Yanga, Metacha Mnata yupo kwenye rada za mabosi wa mtaa wa Msimbazi, Simba ili kuongeza nguvu ndani ya kikosi hicho kinachoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Tetesi zimeeleza kuwa Mnata amekuwa akihusishwa kujiunga na watani hao wa jadi jambo ambalo viongozi wake wameshtukia na kumpiga mkwara mzito.

 

Machi 7 alipofungwa bao moja na Pius Buswita, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, ilielezwa kuwa mabosi wa Yanga walimpigia simu nyota huyo na kumpa lawama nzito jambo ambalo lilimfanya Mnata achukue maamuzi ya kuwaaga mabosi hao kupitia mitandao ya kijamii.

 

Ujumbe huo haukudumu muda mrefu aliufuta na kufanya mdahalo uwe mkubwa kuhusu hatma yake ndani ya Yanga.

Alipotafutwa Mnata ili atolee ufafanuzi suala hilo hakuwa tayari kulizungumzia.

 

Ufafanuzi ambao ulitolewa na Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Mshindo Msolla aliweka wazi kwamba hakuna tatizo kati ya Yanga na Mnata bado ni mchezaji wa timu hiyo.

 

Kwa sasa Mnata yupo na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ambayo Machi 18 itakuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Kenya.

 

Mchezo wa kwanza uliochezwa jana, Machi 15, Stars ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-1 hivyo Machi 18 utakuwa ni wa marudio.


Toa comment