The House of Favourite Newspapers

Meya Kinondoni: Tutaondoa makazi yote holela (Video)

meya-sitta-3

Makala: Elvan Stambuli na Sifael Paul | Gazeti la Uwazi, Toleo la Jumanne Januari 10, 2017

Dar es Salaam: Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Samuel Sitta alifanya ziara katika ofisi za gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo alipata fursa ya kuhojiwa na waandishi wetu.

Katika mahojiano hayo, Ben Sitta alieleza mambo mengi ikiwa ni pamoja na mikakati ya manispaa yake ya kuondoa makazi holela yasiyopimwa. Fuatana nasi katika mahojiano hayo…

meya-sitta-5

Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Samuel Sitta.

Swali: Baba yako, marehemu mzee Samuel Sitta na mama yako, Magreth Sitta wametumikia ubunge kwa miaka mingi, kwa nini wewe uliamua kugombea udiwani wa Msasani jijini Dar badala ya ubunge?

JIBU: Ni uchaguzi tu, mimi niliamua kugombea udiwani kwani ni njia nyingine ya kuwatumikia wananchi, kwenye halmashauri ndipo kuna wananchi wengi na lengo hasa lilikuwa ni hilo na hakika tunajitahidi kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kijamii.

meya-sitta-4Swali: Katika kazi yako ya udiwani umekumbana na changamoto gani?

JIBU: Changamoto kubwa kwenye halmashauri yangu ni bajeti finyu. Mwaka huu peke yake wanafunzi waliokosa nafasi ya kwenda sekondari ni 3,000, wamebaki kwa sababu nafasi za madarasa hazitoshi. Vyumba vya madarasa bado ni changamoto, barabara tunataka ziwe za lami, bado ni changamoto, migogoro ya ardhi ni mingi, watu wanakaa kwenye maeneo ambayo hayajapimwa. Tunataka kuondoa tatizo hili ili maeneo mengi yapimwe, tunataka kupima maeneo ambayo hayajapimwa, squatter upgrading, tuna lengo la kuboresha maisha, maeneo kama Tandale, Mwananyamala na Bonde la Mpunga yapangiliwe na tuboreshe miundombinu. Au wenye nyumba maeneo hayo wauze au wapewe fedha au tujenge flati na wale watu wapewe nyumba za kukaa pale. Mazingira ya maeneo hayo hayafai kwa watoto wanaokua. Huo mpango upo na tutatekeleza ndani ya miaka mitano.

Swali: Kuna malalamiko mengi juu ya ucheleweshwaji wa huduma kama kukata leseni za biashara na kadhalika, hilo likoje?

JIBU: Mimi nimesomea masomo ya IT (Information Technology). Kwa upande wa huduma kwa wananchi wetu, tunaleta utaratibu wa kupokea maombi na kuyafanyia kazi kwa njia ya mtandao kama vile leseni ya biashara, vibali vya ujenzi, hiyo ni njia ya kupunguza msongamano kwenye ofisi za halmashauri yetu.

 meya-sitta-2

Swali: Elimu ina changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa maabara, vipi katika manispaa yako?

JIBU: Ni kweli. Tuna shule za sekondari 22, sita tayari zina maabara ya kompyuta, tunataka mwisho wa mwaka huu shule zote ziwe na maabara za kompyuta. Wenye vipaji watajengewa viwanja, kutakuwa na academy kwa ajili ya kusaka vipaji.

Swali: Je, kuna mpango wowote wa kupunguza umaskini katika manispaa yako?

JIBU: Tumeandaa mpango wa kukopesha vikundi vya wanawake na vijana na watakopeshwa kati ya shilingi milioni moja hadi tatu. Dhamana ya mkopeshwaji ni kikundi hasa kwa vijana wajasiriamali, fedha zipo na kuna mabenki tumeshaongea nayo. Sikufurahishwa na fedha ambazo zilitolewa kipindi cha nyuma. Kuhusu elimu, ni bure lakini kuna changamoto nyingi na watoto wa mtaani hatujaweka ajenda za kuweza kuwasaidia.

 meya-sitta-6

Benjamin Samuel Sitta (katikati) akiwa na Mhariri wa Gazeti la Ijumaa Wikienda Sifael Paul pamoja na Mhariri wa Gzeti la Uwazi, Elvan Stambuli.

Swali: Katika manispaa yako kuna wabunge wa Chadema na madiwani wao, pia wapo wa CUF, je, kuna upinzani wakati wa mijadala yenu?

JIBU: Manispaa inaendeshwa na Baraza la Madiwani, wabunge na madiwani ni wajumbe na ndani kuna mawaziri. Lakini tangu niingie sijapata upingamizi wowote katika kuendesha shughuli za manispaa na hatuhitaji chama kwenye Baraza la Madiwani. Hakuna hata sehemu moja ninaingiliana na kazi za mbunge. Miradi inayotekelezwa ni ile iliyoingizwa kwenye bajeti, hivyo hakuna mtu anayeweza kupindisha hilo. Pili, waheshimiwa wabunge naheshimiana nao na wote nafanya nao kazi. Mimi kwenye baraza ni mwenyekiti. Kinachotekelezwa pale ni ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hata wangeshinda Chadema, ningetekeleza ilani yao. Kinachoangaliwa sasa ni CCM iliahidi nini na tunatekeleza. Diwani anapoingia kwenye kikao anapigania maendeleo ya eneo lake na siyo itikadi za vyama.

Swali: Manispaa ya Kinondoni inaongoza kwa ujambazi, hilo mmeliona na mnakabiliana nalo kivipi?

JIBU: Hilo suala ni la kamati ya ulinzi na usalama lakini tuna mpango wa kufunga kamera kwenye mitaa, tunadhani itasaidia kupunguza majambazi. Kinondoni, Masaki na Oysterbay ni maeneo yetu yaliyoongoza kwa ukabaji lakini tumeweka vituo vya polisi kama kile cha Coco Beach na Masaki na sasa hali ni shwari.

Swali: Vipi tatizo la madawa ya kulevya kwenye manispaa yako?

JIBU: Hilo tatizo lipo. Wanaoendekeza biashara hiyo ni watu wenye fedha na vita yake siyo ndogo, lakini tutapambana nao kwa kushirikiana na vyombo vya dola na wananchi. Wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama ni DC (Mkuu wa Wilaya) na RC (Mkuu wa Mkoa) na kwa upande wangu anakwenda mkurugenzi wa wilaya, hao ndiyo wanajua zaidi kuhusu ulinzi na usalama.

Swali: Vipi kuhusu mchakato wa kiwanda cha kuchakata takataka?

JIBU: Mpango huo upo, tumeshalipa fidia pale Mabwepande tutakapojenga kiwanda, tumeshakubaliana na watu wa Jiji la Hamburg, Ujerumani watatujengea. Takataka kitakuwa kitu cha thamani na kutakuwa na magari maalum ya kukusanya takataka na kiwanda kitatoa ajira na kufanya jiji safi.

Swali: Kuna watu maeneo ya Kunduchi-Maweni wanatishiwa kubomolewa nyumba zao, manispaa mna mpango gani na maeneo hayo?

JIBU: Kunduchi-Maweni ni eneo la manispaa lililovamiwa na watu. Manispaa ilitaka kujenga mji wa kisasa. Kuna watu naambiwa 3,000, wameshindwa kesi, manispaa imeshinda. Kuna watu wamejenga nyumba nzuri kwelikweli. Nashangaa unajengaje pale huna hata ofa? Ni sehemu nzuri lakini haipo kwenye mpango mji. Ni suala ambalo linahitaji busara maana baada ya kushinda kesi ilitakiwa pale tukapasawazishe, tutatumia busara kuona la kufanya lakini lazima manispaa ipate chochote pale kwa sababu ni eneo lake na lina thamani. Lile eneo lazima lipangwe, liwe na huduma za kijamii na kwenye kupanga lazima kuna watu wataathirika. Ni kitu kinahitaji mjadala mpana na lazima Baraza la Madiwani liamue. Tungefuata sheria ilitakiwa pale pawe na buldoza nane za kusawazisha. Kuna uzembe ulifanyika huko nyuma.

Swali: Kuna taarifa kuwa wageni wanapewa kazi ambazo wangeweza kufanya wazawa kama vile makusanyo ya maegesho ya magari jijini Dar inafanywa kampuni ya viwanja vya ndege ya Kenya, nini maoni yako kuhusu hilo?

JIBU: Naamini wazawa wanaweza kufanya makubwa mazuri. Kiutaratibu parking (maegesho) zinatakiwa kukusanywa na jiji na inatakiwa itolewe tenda. Sina uhakika na taratibu zetu za Afrika Mashariki, sijui kama walitangaza tenda kimataifa kuwapa kazi hizo. Kuna mambo mengi ndani yake ya mimi kujiridhisha.

Comments are closed.