The House of Favourite Newspapers

Meya: Mradi Wa Mabasi Ya Mwendo Kasi Waja Mbagala (Video)

meya-temeke-2  Wahariri wetu Elvan Stambuli (kushoto) na Sifael Paul (kulia) wakihojiana na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya ya Temeke, Abdallah Jaffar Chaurembo ambaye ni Diwani wa Kata ya Charambe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCC).

Sifael Paul na Elvan Stambuli
Meya wa Manispaa ya Temeke, Msitahiki Abdallah Jaffar Chaurembo anaelezea mipango ya manispaa yake katika sehemu hii ya pili ya mahojiano na wahariri wetu yaliyofanyika ofisini kwake akianzia kueleza mgawanyo wa mali kati ya halmashauri yake na mpya ya Kigamboni pia mradi wa mabasi ya mwendokasi ambao anasema unakuja, ungana nasi:

Swali: Halmashauri yako imegawanywa mara mbili, Temeke na Kigamboni, je, mgawanyo wa mali ukoje?

meya-temeke-1

Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya ya Temeke, Abdallah Jaffar Chaurembo akiendelea kufunguka.

Jibu: Kwa mujibu wa tangazo la serikali, Temeke imegawanywa na kupata wilaya mbili za Temeke na Kigamboni. Baraza letu la madiwani tulikubaliana kwamba mali za Kigamboni zibaki Kigamboni. Pia mali za Temeke zilibaki Temeke ikiwa ni sambamba na watumishi.

Kigamboni kuna maeneo mengi ya uwekezaji. Kigamboni ni mtoto wetu hivyo kuna mali nyingine ambazo ni uwekezaji wa Temeke tumeamua kuwapa Kigamboni ikiwemo jengo la kitega uchumi la Mkuki House ambalo tumewapa Kigamboni.

Ni mali ya Halmashauri ya Temeke lakini tumeamua liende Kigamboni sisi tukabaki na viwanja vya Temeke-Mwisho. Pia tumegawana nyumba zetu za vitega uchumi zilizopo kule Masaki. Pia pale Mtoni-Mtongani tumewagawia nyumba za kupanga.
Kigamboni wana vyanzo vichache vya mapato ya shilingi bilioni 8 wakati bajeti yao ni shilingi bilioni 50 hivyo wana upungufu wa shilingi bilioni 42 ndiyo maana tukajitoa kuwasaidia.

Pia tumewapa greda moja la kukwangulia barabara na kijiko kimoja kwa ajili ya kuzoa taka. Ukweli ni kwamba kwenye baraza letu hakukuwa na mvutano kwani tulitumia nusu saa tu kugawa mali tukiamini Kigamboni ni mtoto wetu anayetutegemea.

TEMEKE IPO VIZURI KWA USAFI
Swali: Tatizo kubwa la Temeke ni mlipuko wa kipindupindu hasa kwa serikali zilizotangulia, je, nini mkakati wa kulimaliza tatizo hilo?

Jibu: Temeke ipo vizuri kwa usafi na si kweli kwamba inaongoza kwa magonjwa ya mlipuko. Tumeweka mikakati thabiti ya kuweka mazingira yetu safi. Tunatumia vikundi mbalimbali vikiwemo vya jogging.

Pia tumenunua kijiko kipya cha kisasa cha kukusanya na kuzoa taka na sasa tumeelekeza nguvu kwenye kununua malori ya kuzoa taka.

Tunatoa elimu kwa watu wetu juu ya magonjwa ya milipuko kama kipindupindu kwa kuwataka wawe wasafi kwenye maeneo yao.

Pia tumenunua mitambo kwa ajili ya maji safi. Kimsingi hata ukitazama kwenye makao makuu ya halmashauri yetu mazingira ni safi na yanavutia ukilinganisha na halmashauri nyingine za jiji.
Kinachofuata sasa ni kupanda miti ya kutosha kwenye halmashauri yetu na tayari zoezi limeanza kwa kuwataka wananchi kufanya hivyo kwenye maeneo yao.

TATIZO LA MADAWATI TEMEKE NI HISTORIA
Swali: Je, kwenye halmashauri yako mmemaliza tatizo la madawati na limefanikiwa kwa kiasi gani?

Jibu: Kwanza tulimuunga mkono Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa asilimia zote kwa kufuta safari za nje na kubana matumizi ili fedha hizo ziende kwenye kuwahudumia wananchi. Kwenye halmashauri yetu tulitenga shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya miundo mbinu ya shule zetu na madawati.

Tunawashukuru wadau mmojammoja, kampuni na benki zilizotuunga mkono na kutupatia madawati na sasa tatizo la madawati limekwisha kabisa. Pia tunamshukuru Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) na Mkuu wa Mkoa (Paul Makonda), wabunge na wote waliotusaidia. Sasa tumeanza ujenzi wa madarasa ili kukamilisha ahadi yetu ya Elimu Bure lakini isiwe elimu tu bali elimu bora inayoendana na mazingira rafiki ya kusomea.

NEEMA YAJA CHARAMBE
Swali: Wewe pia ni Diwani wa Charambe na wananchi wako wana kero mbalimbali zikiwemo za maji na mitaji au mikopo, je, hili umeliwekea mikakati gani?

Jibu: Kwanza nipo karibu sana na wananchi wangu wa Charambe, nimezaliwa pale na kukulia pale ndiyo maana sina bodigadi kama wengine kwani itifaki hainirusu kuwa na bodigadi, nafanya hivyo ili kila mwananchi anifikie bila woga. Makaburi ya wazee wangu yapo Charambe hivyo matatizo ya watu wa Charambe nayajua mtaa kwa mtaa. Changamoto zipo lakini kwa kuanzia, kuna Hospitali ya Nzasa B ambayo tumejenga kwa gharama ya shilingi milioni 300.
Kuna mfereji korofi wa Kwa Shegu ambapo hatua za ujenzi wake zimeanza kuanzia Msikiti Mweupe na kwa Mama Tembo.

Pia kuna ujenzi wa Barabara ya Kwa Pazi unaoendelea kwa ufadhili wa Benki ya Dunia. Pia tunaendelea na zoezi la kubaini nyumba na viwanja hewa. Pia tunahakikisha hela za serikali zinakwenda kwa wanaohusika. Barabara, elimu na tatizo la madawati tumelimaliza. Kuhusu mikopo tumeingia kwenye makubaliano na Benki ya Wananchi wa Dar-DCB ambayo inatoa mikopo kwa akina mama na vijana.

TATIZO LA USAFIRI
Swali: Mbagala kuna tatizo kubwa la usafiri kutokana na kuwa na watu wengi, utatatuaje tatizo hilo?

Jibu: Ni kweli Mbagala ina watu wengi. Kuna mradi wa mabasi yaendayo haraka ambapo awamu ya pili itakuwa ni kutoka Kariakoo hadi Mbagala hivyo wakazi wa Charambe nao watapata ahueni kwenye suala la usafiri na hata ukiangalia pale Kariakoo kuna matoleo yake ya kuelekea Mbagala na kuna baadhi ya watu tumezuia wasijenge kwani barabara ya mabasi hayo itapita kwenye maeneo husika.
-MWISHO-

Meya: Temeke Inakabiliwa Na Ongezeko La Watu (Video) ==>www. globalpublishers.co.tz/meya-temeke-inakabiliwa-na-ongezeko-la-watu/

Comments are closed.