The House of Favourite Newspapers

Mfalme Mswati III Abadili Jina la Nchi Yake

MFALME Mswati wa III wa Swaziland amebadilisha jina rasmi la taifa hilo kutoka Swaziland na kuliita Ufalme wa eSwatini (The Kingdom of Swaziland) wakati wa maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa ambapo ametimiza miaka 50 na wakati huo huo taifa hilo likiadhimisha miaka 50 ya uhuru wake.

 

Jina hilo jipya, eSwatini, lina maana ya ardhi ya Waswaz na limetumiwa rasmi na Mfalme Mswati wa III kwa miaka mingi. eSwati ni jina ambalo mfalme alilitumia alipokuwa akihutubia katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa mwaka 2017 na katika ufunguzi wa bunge la nchini mwake mwaka 2014.

 

Mfalme Mswati ni miongoni mwa wafalme wa mwisho wa duniani waliobaki na ametawala tangu mwaka 1986. 

Mswati III kwa sasa ana wake 15 akiwa anaifuata rekodi ya Baba yake aliyekuwa na wake 125. Wanaharakati wa kutetea usawa wa jinsia wanasema mfumo wa utawala wa nchi hiyo ni wa kushangaza na unawabagua wanawake.

 

Mswati III ametoa sababu kuu ya kubadilishwa kwa jina la nchi yake kuwa kila aendapo katika mikutano ya kimataifa, mataifa mengine wamekuwa wakilichanganya taifa lake na nchi ya Switzerland.

Nao raia wametoa maoni yao juu ya hatua ya mfalme wao na kusema kuwa badala ya kushughulika na jina la nchi yake, badala yake alipaswa kupasua kichwa ni namna gani anaweza kuimarisha uchumi wa nchi hiyo unaodidimia siku hadi siku.

 

Kwa taarifa yako, Mfalme Mswati anajulikana pia kama Ngwenyama kwa lugha ya taifa hilo jina likiwa na maana ya ‘Simba’, lakini pia anajulikana ullimwenguni kwa tabia yake ya kuoa wake wengi na kwa kuzingatia mavazi ya jadi pamoja na kuthamini mila na desturi.

Comments are closed.