The House of Favourite Newspapers

MFANYABIASHARA ATEKWA, AJERUHIWA VIBAYA KICHWANI

MFANYABIASHARA maarufu nchini, Innocent Shirima (pichani), mkazi wa Salasala jijini Dar es Salaam, ametekwa na watu wasiojulikana kisha kutupwa kwenye kichaka kilicho kando ya barabara.  Innocent ambaye alikuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Vunjo mwaka 2015, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kushindwa kwa kura kiduchu na James Mbatia, aliliambia Uwazi kuwa, alifanyiwa unyama huo Septemba 4, mwaka huu.

TUKIO LILIVYOKUWA

Mfanyabiashara huyo mwenye maduka kadhaa jijini Dar ya bidhaa mbalimbali vikiwemo vifaa vya ujenzi alisema: “Baada ya kumaliza shughuli zangu majira ya saa nne usiku, niliwasha gari langu kwenda kwenye mgawaha uliopo karibu na moja ya sehemu yangu ya biashara.

“Si mbali na ninapoishi. Nilipomaliza kula wakati narudi nyumbani kwa mbele kidogo nilimuona kijana kama anahangaika kuwasha pikipiki yake. “Nilipokaribia alijitokeza kijana mwingine na kuwa kama ananiomba msaada; ikabidi nisimamishe gari nimsikilize.”

APIGWA NA KITU CHEPESI USONI

Innocent aliongeza kuwa kitendo cha kushusha kioo ili amsikilize kijana huyo, lilikuwa ni kosa kubwa kwake kwani alijikuta akipigwa na kitu chepesi mfano wa kitambaa usoni na kupoteza fahamu ghafla. “Nahisi kitambaa hicho kilikuwa na madawa ya kulevya, kwani baada ya kuzimia walinichukua na gari yangu na kunipeleka kusikojulika.

AZINDUKIA KICHAKANI

Innocent anaendelea kuliambia Uwazi kuwa matukio yaliyoendelea nyuma baada ya yeye kupoteza fahamu hayakumbuki; zaidi ya kuzinduka na kujikuta yuko kichakani eneo la Njia Panda ya Kawe, Ukwamani na Kawe Beach karibu na Hoteli ya Pikolo.

Mfanyabiashara huyo anaeleza kuwa, baada ya kutelekezwa katika mazingira tatanishi na watekaji wake kutoweka walipita vijana wawili wakiwa kwenye pikipiki ambao baadaye walimsaidia.

SIMULIZI YA WALIOMUOKOTA

Innocent anaeleza kuwa, baada ya kupata fahamu na kujikuta akiwa na majeraha ya kutisha kichwani na mwilini yanayosadikiwa kutokana na kukatwa mapanga na watekaji ndipo vijana waliomuokota walipoanza kumpa simulizi ya kusikitisha.

“Sikuwa katika ufahamu timamu lakini wale vijana wanasema mara ya kwanza walipopita kwenye barabara walikuta gari yangu ikiwa kando imefunguliwa milango yote minne, wakajua kutakuwa na tukio.

“Ikabidi wapite bila kusimama, waliporudi wakakuta hali iko hivyo, wakashauriana waje karibu ndiyo wakanikuta nimezimia huku nikiwa na majereha makubwa yaliyokuwa yakivuja damu nyingi.

“Mwanzo wale vijana walipanga waniache kwa kuhofia wakitoa taarifa watakamatwa wao, lakini Mungu mkubwa wakajipa moyo na kusema liwalo na lilwe ndiyo wakaanza kuita wapita njia wengine ambapo walifika na kuanza kunifunga majeraha yaliyokuwa yakivuja damu nyingi.”

APATA UFAHAMU KAMILI

“Huduma waliyonipa iliniwezesha kurejewa na fahamu ambapo niliona damu nyingi zikiwa zimetapakaa mahali hapo, jambo lililonifanya niamini kuwa nilikuwa nimecharangwa mapanga.

“Nikakumbuka wale vijana walivyoniteka wakati nikielekea nyumbani, basi niliwashukuru wale vijana walionikoa na kuwaambia kuwa ninaweza kuendesha gari kwenda Kituo cha Polisi Kawe kutoa taarifa; wale vijana walikubali kuongozana nami kama sehemu ya kuendelea kunipa msaada.”

AGUNDUA VITU VILIVYOIBWA

Katika hali ya kushangaza Innocent anaeleza kuwa vijana wale walomteka walichukua vitu vidogovigo ikiwemo fedha ya matumizi aliyokuwa nayo na kompyuta mpakato moja huku nyingine wakiicha.

“Kwenye gari kulikuwa na bastola na kompyuta nyingine lakini hawakuichukua, kitu kilichonifanya niamini kuwa wale hawakuwa majambazi bali watekaji waliotaka kunidhuru.

“Kama walikuwa wanahitaji taarifa zangu wasingechukua kompyuta moja na kuacha iliyokuwa na taarifa zangu binafsi,” alisema Innocent ambaye anamiliki pia viwanda vidogo vya kufyatua matofali.

AZIMIA KITUO CHA POLISI

Simulizi ya unyama aliofanyiwa mfanyabishara huyo inafika hadi Kituo cha Polisi Kawe ambako alikwenda kuandikisha maelezo pamoja na kupatiwa Fomu Namba 3 ya Polisi (PF3) kwa ajili ya kwenda kupatiwa matibabu.

Aidha, inaelezwa na wale waliokuwa wakimpa msaada kuwa, muda mfupi baada ya kufika kituoni alidondoka tena na kupoteza fahamu, jambo lililowafanya polisi wafanye mpango wa haraka wa kumkimbiza Hospitali ya TMJ kwa ajili ya tiba

HIZI HAPA HISIA ZA INNOCENT

Kufuatia tukio hilo baya kumtokea katika maisha mfanyabishara huyo ameingiwa na hisia kuwa kuna watu wabaya (hakuwajata wanatoka wapi na sababu gani) wanamfuatilia kwa muda mrefu tangu mwaka 2016 baada ya kutoka kwenye harakati za uchaguzi.

Anasema mwaka 2016 nyumbani kwao Marangu mkoani Kilimanjaro baba yake mdogo aliyekuwa pia mlinzi katika nyumba yake ya huko aliuawa kinyama na wasiojulikana kwa kukatwa shingo. “Mimi nilikuwa Dar, nilikapanga kurejea Marangu lakini kuna rafiki yangu ambaye ni jaji alikuwa na sherehe ya kumuaga binti yake aliyekuwa anaolewa; akaniomba niwepo kwenye shughuli.

“Naweza kusema kitendo cha kuahirisha safari ndicho kilichookoa maisha yangu; kwani siku baba yangu mdogo anauawa watu hao walidhani nilikuwepo, waliponikosa ndiyo wakamdhuru baba yangu mdogo,” alisema.

AKUMBUSHA MAMBO YA UCHAGUZI 2015

“Mwaka 2015, ubunge haikuwa bahati yangu tu, alinipita Mbatia wa NCCR-Mageuzi kwa kura chache sana, kilichomukoa ni kupita kwa mheshimiwa Rais Magufuli (enzi hizo mgombea urais CCM) kwenye kampeni huko Vunjo.

“Alipofika pale mheshimiwa aliwaomba wananchi wa Vunjo wamchague Agustino Mrema wa TLP na si mimi wa CCM, kimsingi ilikuwa ni propaganda za kisiasa ambazo mimi siwezi kulaumu kwa chochote kwa sababu mimi ni mwanasiasa mkomavu.

“Sasa wananchi walipoambiwa hivyo ndiyo kura zangu zikapungua kidogo nikashika nafasi ya pili nyuma ya Mbatia,” alisema Innocent huku akiwa na imani na rais kuwa atasaidia kulinda maisha yake kutoka kwa wanaotaka kumtoa roho yake.

HAJAKATA TAMAA KATIKA SIASA

Pamoja na misukukosuko anayopitia katika maisha  yake, Innocent alimwambia mwandishi wetu kuwa, hawezi kuzipa kisogo siasa kwani lengo lake katika siku zijazo ni kuwatumikia wananchi wa Vunjo kwa nafasi ubunge.

“Hii ni nchi yangu lakini naishi kama mkimbizi nashinda sehemu nyingine nalala sehemu nyingine kuhofia maisha yangu, lakini sikati tamaa nitaendeleza kukipigania chama changu cha CCM hadi mwisho. Naamini siku moja ndoto yangu ya kuwa mbunge itatimia licha ya vitisho na vikwazo hivi.”

POLISI WAMSUBIRI INNOCENT APONE

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi (ACP) Mussa Tahibu alipotafutwa ili kujua kinachoendelea katika sakata hilo, simu yake haikuwa hewani kila ilipopigwa.

Hata hivyo, afisa mmoja mwandamizi wa jeshi hilo Mkoa wa Kindondoni aliliambia Uwazi kuwa kama tukio hilo lipo basi wanamsubiri mlalamikaji aende kuwapa ushirikiano kwa ajili ya hatua zaidi kwani jeshi la polisi chini ya IGP Simon Sirro haliwezi kufumbia macho matukio kama hayo

Stori: RICHARD BUKOS NA NEEMA ADRIAN , UWAZI

Comments are closed.