The House of Favourite Newspapers

Mfanyabiashara Ateswa, Auawa!

MFANYABIASHARA mmoja aliyetambulika kwa jina la Godfley Charles ameteswa na kuuawa na watu wasiofahamika baada ya kukatwakatwa na mapanga wilayani Newala, Mkoa wa Mtwara kwa kile kinachodaiwa ni kutaka kumpora pesa zilizokuwa kwenye simu yake ya mkononi.

 

Akizungumza kwa masikitiko, mama mzazi wa marehemu, Merina Charles akiwa nyumbani kwake Ubungo jijini Dar, alisema kuwa amepokea kwa masikitiko kifo cha mwanaye huyo kwani alikuwa akimtegemea na mbaya zaidi hajui kinachoendelea juu ya upelelezi wa mauaji ya mwanaye huyo.

 

“Ilikuwa Machi 4, mwaka huu, nilipigiwa simu kati ya saa moja hadi saa mbili usiku kutoka kwa Felix ambaye ni msimamizi wa harusi ya Godfley akiniambia kuwa amepigiwa simu kutoka Sua (Morogoro) kwamba wamepigiwa simu na polisi kutoka Newala mwanangu amefariki dunia na wamekuta note book pamoja na kitambulisho kinachoonyesha kuwa ni mfanyakazi wa Sua kwenye mfuko wake wa suruali,” alisema Merina.

 

Aliongeza kusema kuwa ikabidi ampigie mke wa marehemu ambaye alimuambia kuwa marehemu alisafiri kuelekea Newala kibiashara lakini kila akimpigia simu, hapatikani, inasemekana kule alipokelewa na mwenyeji wake, baada ya hapo walikwenda baa yeye marehemu alikuwa akinywa soda na wenzake wawili mmoja akiwa amevaa koti jeusi walinunuliwa bia.

 

“Wakamwambia kuwa kuna sehemu kwa rafiki yao kuna sherehe waende, wakatoka hapo, baada ya muda mfupi wakarudi na marehemu alionekana akiwa anacheza ‘pull’ huku wenzake wakiendelea kunywa pombe.

 

“Walipomaliza wakatoka ndio wakaenda kumfanyia kitendo cha kinyama cha kumkatakata mapanga sehemu za kichwani, inadaiwa kuna watu walikuwa wakimsikia marehemu akiomba msaada na wale wauwaji walikuwa wakimuamuru kutaja namba ya siri ya kwenye simu yake ya mkononi,’’ alidai Merina. Aliendelea kueleza: “Baada ya hapo tukaanza kufanya mawasiliano na viongozi wake wa kule Sua ili tujue mwili utafikaje hapa Dar es Salaam.

 

“Hivyo basi ikabidi mwanangu mwingine anayeitwa Christopher Charles Kanyosa, wa pili kuzaliwa baada ya marehemu, pamoja na baadhi ya majirani, wakatoka hapa Dar na kwenda Newala kuuchuka mwili.” Mdogo wa marehemu, Christopher Charles amesema hajui afanye nini kuhusu ndugu yao mpendwa waliompoteza kwa sababu inasemekana kuwa mzigo wa dagaa uliingia sokoni na ulipokelewa baada ya ndugu yao kupoteza maisha.

 

“Ilibidi tumfuatilie yule rafiki yake ambaye walikuwa wanafanya naye biashara. Alitupigia simu kuwa anakuja kuhani msiba, mimi nikafanya taratibu na jeshi la polisi, yule mtu alikamatwa akawekwa Kituo cha Polisi Mbezi Dar baada ya hapo alisafirishwa hadi ambako tukio limetokea (Newala) ili taratibu za upepelezi katika Kituo cha Polisi Newala ziendelee. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, SACP Lucas Mkondya alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.“Ni kweli tukio lilitokea na upelelezi bado unaendelea,” alisema.

Stori: Neema Adrian, Dar

Comments are closed.