Mfu Aliyerudiwa na Uhai-2

 

ILIPOISHIA WIKIENDA

Wakati tunataka kuagana alitia mkono mfukoni akatoa bupa la noti, akahesabu shilingi elfu hamsini akanipa.

“Chukua hii itakusaidia kwa usafiri.”

“Asante,” nikamwambia na kuzitia kwenye pochi yangu ndogo niliyokuwa nimeishika mkononi.

SASA ENDELEA…

BAADA ya hapo tukaagana nikaendelea na safari yangu na yeye akaingia kwenye gari lake.

Wakati nikiwa katika nyendo zangu niligundua kuwa yule mzee alikuwa akinifuata na gari lake kimya kimya kunichunguza nilikuwa ninakwenda wapi. Bila shaka alifikiria kuwa nilikuwa ninakwenda kwa wanaume.

Nilipomuona nilizuga nikaingia katika duka fulani. Nikatazama tazama vitu na kuuliza bei kisha nikatoka. Nikaona alikuwa ameliegesha gari lake kwa mbali. Nikafahamu kwamba ataendelea kunifuata na mimi sikutaka afahamu nilikuwa nakwenda wapi, nikaahirisha safari yangu na kwenda kwenye kituo cha daladala. Nikapanda daladala na kurudi nyumbani.

Licha ya kile kitendo chake kutonifurahisha, nilifurahia pesa alizonipa ikiwemo ile ahadi yake ya kesho yake ya kwenda kunifanyia shopping.

Vile nilivyofahamu kuwa alikuwa na uwezo wa kipesa nilihisi kuwa angenifanyia shopping ya nguvu kwa vile nilivyomwambia kuwa nimeafikiana na dhamiri yake ya kutaka kunioa.

Nilimuona mzee tena mwenye watoto wa umri wangu. Na bado nilikuwa nafikiria mustakbali wake na wangu lakini kama wasemavyo wahenga; “Baniani mbaya, kiatu chake dawa.”

Kama kulikuwa na kitu chochote kilichokuwa kinanivutia kwake ni pesa zake tu alizokuwa akinipa mara kwa mara ambazo nilikuwa sizipati hata kwa mpenzi wangu niliyekuwa nampenda kwa dhati ya moyo wangu.

Niliwaza hata kama Alhakim atanioa bado nitaendeleza uhusiano wangu na mpenzi wangu. Sitakuwa tayari kumuacha labda kwa kifo kwa sababu nilikuwa nampenda wakati yule mzee sikumpenda.

Siku iliyofuata nilipotoka shule niliharakisha kurudi nyumbani. Nikaoga harakaharaka na kubadili nguo. Kwa kawaida ninapotoka nyumbani kwetu huwa sibanwibanwi sana bora tu niseme ninakwenda wapi ili watu wafahamu niko wapi.

Nikamwambia mama kuwa ninakwenda kwa rafiki yangu mtaa wa pili kusoma kwa sababu mtihani ulikuwa unakaribia.

Nilipotoka nyumbani nikaenda pale nilipoahidiana kukutana na Alhakim. Nilipofika nikakuta ameegesha gari lake pembeni mwa barabara akinisubiri. Nilikwenda kufungua mlango wa upande wa pili wa dereva nikaingia kwenye gari.

“Shikamoo,” nikamwamkia.

“Marahaba. Habari ya nyumbani?” akaniuliza huku akiliwasha gari.

“Nzuri.”

Alitia gia tukaondoka. Watu wa mtaa huo walikuwa wakitutazamatazama tangu ninaingia kwenye gari hilo hadi tunaondoka.

Si unafahamu tabia za binaadamu kutaka kudadisi kila kitu.

“Ulifika muda mrefu?” nikamuuliza Alhakim.

“Si muda mrefu sana.”

“Labda nimechelewa kidogo kwa sababu walichelewa kututoa shuleni,” nikamdanganya.

“Kulikuwa na nini?”

“Walimu walitupa kazi ya kusafisha mazingira kabla ya kuondoka.”

“Inabidi uvumilie, ndiyo maisha ya shule.”

“Ni kweli lakini wakati mwingine walimu wanatuchokesha.”

“Na ni kwa nini wanafanya hivyo?”

“Kiburi tu. Kwa vile ni walimu wetu basi wanataka kutuonesha kuwa wao ndio kila kitu. Mtu anafika shule na hasira zake anazimalizia kwa mwanafunzi.”

“Na nasikia kuna huu mtindo wa baadhi ya walimu kuwatongoza wanafunzi wao, ni kweli?”

“Ni kweli. Wapo walimu wenye tabia hiyo. Sasa pale ukimkataa ndio anakufanyia visa lakini chanzo ni hicho.”

“Kwa hiyo na nyinyi mliwakataa walimu wenu ndio wakaamua wawape kazi katika muda wenu wa kurudi nyumbani ili kuwakomoa?”

“Labda wenzangu lakini mimi sina muda na mwalimu. Pale tumefuata masomo si mapenzi.”

Pengine maneno yangu yalimkosha Alhakim, nikamuona ametoa meno akicheka.

Pakapita ukimya wa sekunde kadhaa kabla sauti ya Halhakim kusikika tena.

“Mmeshazungumza na wazazi wako kuhusu hili suala?”

“Nilizungumza na mama.”

“Baba hakukueleza chochote?”

“Mara nyingi mimi huzungumza na mama sio baba. Kama baba atanieleza itakuwa siku nyingine.”

“Mimi nikikuoa wewe utaweza kuwasaidia wazazi wako kipesa. Si unaona baba amepata tatizo la mguu na hataweza kufanya kazi tena. Atakuwa anawategemea nyinyi watoto wake.”

Alhakim aliponiambia hivyo sikusema kitu ingawa nilikuwa na mengi ya kumuuliza. Nilishindwa kumuuliza kwa sababu sikuwa nimemzoea ukizingatia pia alikuwa mtu mzima.

Ni sawa angenioa mimi na ningepata uwezo wa kipesa kuwasaidia wazazi wangu kutokana na yeye lakini watoto wake ameshawafahamisha kuwa anataka kuoa binti mdogo na kwamba watoto wake watakubali kuwa na mama ambaye wanamzidi kiumri?

Nikiwa mke wake, watoto wake wataniheshimu kama mama?

Ataweza kuwadhibiti watoto wake wasiingilie maisha yetu?

Isionekane nimekwenda kwake kutafuta pesa wakati yeye ndiye aliyenipenda mwenyewe.

Katika suala hilo la ndoa niliona kama ninakokotwa bila hiyari yangu kutokana na tamaa ya pesa.

“Umeshawahi kupanda ndege?” Alhakim akaniuliza ghafla na kuyakatiza mawazo yangu.

Nikatikisa kichwa.

“Sikuwahi kupanda ndege.”

“Safari nyingine tutakwenda kufanya shopping Zanzibar kwa ndege. Sifahamu kama baba yako atakubali uende na mimi Zanzibar.”

“Labda atakubali niende mwenyewe.”

“Atahisi nataka kwenda kinyume labda?”

“Mzazi yeyote ni lazima aoneshe kuwa anamdhibiti mwanawe hata kama kwenda mimi na wewe Zanzibar kusingekuwa na madhara. Hatuwezi kulaumu.”

Alhakim alitoa tena meno yake akacheka. Alikuwa mwepesi wa kucheka. Ingawa alitaka kunionesha uchangamfu na nimuone kuwa ni mtu mwema lakini licha ya utoto wangu nilifahamu kuwa watu wa aina yake ndio wanaokuwa madikteta ndani ya nyumba.

Anakuwa mwepesi wa kucheka kabla ya kukuoa lakini akishakuweka ndani anabadilika na kuwa nunda! Hakuna kucheka. Wakati wote anakuwa mkali na vile anavyofahamu kuwa kwetu ni masikini ndio hatanithamini kabisa.

Tukatokea katika maduka ya Kariakoo. Tuliingia katika maduka matatu tofauti. Aliniambia nichague vitu ninavyovitaka. Sikuona aibu. Nilimkomoa.

Nilichagua nguo na vitu vingine vyenye thamani ya karibu shilingi laki nne. Mzee alilipa.

Akanirudisha karibu na kwetu kisha akaniacha.

Nilipofika nyumbani sikumficha mama. Nilimwambia kwamba Alhakim ameninunulia nguo na vitu vingine vyenye thamani ya shilingi laki nne.

“Si unaona mwenyewe. Ndoa bado lakini anakugharamikia!” Mama akaniambia na kuongeza.

“Mimi nakushauri mwanangu kubali akuoe.”

Sikusema kitu. Nikapanga nguo zangu ndani ya kabati.

Siku za mwishoni mwa wiki ndizo siku ambazo hukutana na mpenzi wangu. Alikuwa anaitwa Macheo, mfanyakazi wa shirika la bandari.

Macheo alikuwa mzaliwa wa Tanga. Aliwahi kuniambia alizaliwa Mwarongo eneo lililopo katika barabara ya Pangani kilometa kadhaa kutoka Tanga.

Elimu ya msingi alisoma Tanga lakini elimu ya sekondari na chuo alisoma Dar na akapata kazi hapo hapo Dar.

Wakati tunakutana na kuanza uhusiano alikuwa na miezi kadhaa tangu ameanza kazi yake.

Kwa vile alikuwa ndio anayaanza maisha na mimi bado ninasoma, tuliweka mikakati ya kuoana siku za mbele baada ya mimi kumaliza masomo.

Lakini uhusiano wetu ulikuwa siri yetu mimi na yeye. Nyumbani kwetu walikuwa hawafahamu kitu.

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu.


Loading...

Toa comment