Mfu Aliyerudiwa na Uhai-3

 

ILIPOISHIA IJUMAA…

Elimu ya msingi alisoma Tanga, lakini elimu ya sekondari na chuo alisoma Dar na akapata kazi hapohapo Dar.

Wakati tunakutana na kuanza uhusiano, alikuwa na miezi kadhaa tangu ameanza kazi yake.

Kwa vile alikuwa ndiyo anayaanza maisha na mimi bado ninasoma, tuliweka mikakati ya kuoana siku za mbele baada ya mimi kumaliza masomo.

Lakini uhusiano wetu ulikuwa siri yetu mimi na yeye. Nyumbani kwetu walikuwa hawafahamu kitu.

SASA ENDELEA…

SIKU za mwishoni mwa wiki huondoka asubuhi na kwenda kushinda nyumbani kwake, Tabata.

Kulikuwa na siku wazazi wangu wote waliniweka kikao na kunieleza kwamba wameshachukua pesa za uchumba kutoka kwa Alhakim. Kwa hiyo baba alitaka nitambue kuwa nilikuwa mchumba wa mtu.

“Ukimaliza masomo tu mnaoana,” baba aliniambia.

Nilikuwa ninawaheshimu sana wazazi wangu kiasi kwamba nilishindwa kupingana nao kuhusu suala hilo. Kila nilichoambiwa nilikuwa ninaitikia tu.

Lakini sikuona sababu ya kuacha kwenda kwa Macheo kwa sababu nilikuwa ninampenda. Kama kutakuwa na kitu ambacho kitatia doa katika ndoa yangu na Alhakim ni uhusiano wangu na Macheo ambao niliamini hata nitakapoolewa, bado utaendelea kuwepo.

Wakati wote nilikuwa nikimficha Macheo kuhusu suala la uchumba wangu na Alhakim. Lakini baada ya kufikiri sana, nikaona nikampe ukweli. Nikafunga safari kwenda Tabata.

Kwanza nilipitia Kariakoo, nikanunua vitu nilivyokuwa ninavitaka. Lakini wakati ninazunguka kwenye maduka, nililiona gari ya Alhakim, lakini mwenyewe sikumuona.

Nikaondoka haraka kwenye eneo hilo. Nikiwa katika mtaa mwingine sasa nikielekea katika kituo cha daladala. Nikaliona tena gari la Alhakim nyuma yangu. Nikagundua kuwa Alhakim alikuwa akinichunguza.

Sasa nifanye nini?

Nikafanya kama sikuliona gari lake, nikatembea harakaharaka kuelekea katika kituo cha daladala. Kwa bahati nzuri nilipofika tu daladala likasimama. Nikaingia haraka na kukaa kwenye siti. Daladala likaondoka.

Wakati ninashushwa kwenye kituo cha Tabata, nikaona gari la Alhakim hatua chache nyuma ya daladala.

Nikasema: “Mama yangu wee!”

“Huyu mzee ameniamulia leo!” Nikasema kimoyomoyo nikiwa nimeduwaa kando ya barabara nikiigiza kama ninasubiri magari yapite ndiyo nivuke barabara.

Kwa pembeni mwa macho yangu nililiona gari la Alhakim bado limesimama nyuma ya daladala. Mahali liliposimama, Alhakim alikuwa akiniona vizuri.

Bila shaka alikuwa anasubiri kuona ninaelekea wapi aendelee kunifuata.

Sasa nilithibitisha waziwazi kuwa Alhakim alikuwa ananifuatilia. Iliwezekana alishagundua kuwa nina mtu wangu mitaa ya huku ndipo alipoamua kuiandama daladala niliyopanda aone mwisho wangu.

Pale nilikuwa sina mbinu tena.

“Sasa nifanye nini?” Nikaiuliza nafsi yangu iliyokuwa imegwaya.

Nikawaza kwamba kama nitaendelea na safari yangu, Alhakim ataendelea kunifuatilia na kugundua ninakwenda wapi.

Pia niliona kubadili mawazo na kurudi isingekuwa busara. Ingempa picha kuwa nimerudi baada ya kumuona yeye.

Bado angeweza kuniuliza nilikuwa ninakwenda wapi na kwa nini nimeamua kurudi. Nisingekuwa na la kumwambia.

Sikuwa nimepata ufumbuzi. Nikaliona daladala linaondoka baada ya kushusha watu na kupakia wengine.

Niliwaza kwamba kama nitabaki palepale huku daladala limeondoka, Alhakim angepata nafasi nzuri ya kunifuata na nisingeweza kumkimbia tena.

Nikaona niwahi kuvuka barabara kabla daladalaa hilo kunipita. Nikavuka barabara. Ingawa hakukuwa na gari lolote lililokuwa linapita, nilipiga mbio hadi ng’ambo ya pili.

Sikutaka hata kugeuka kutazama nyuma, nikaingia kwenye vichochoro. Nilifahamu kwamba asingeweza kunifuata kwa gari kwenye vichochoro labda kama angekuwa na pikipiki.

Baada ya kukatiza vichochoro viwili, vitatu, nilichanganyika na watu wengine waliokuwa wanapita. Kwa vile nilikuwa nimezibwa nikatazama nyuma.

Moyo wangu ulishtuka nilipomuona Alhakim akitembea kwa miguu kunifuata.

“Huyu mzee ana tatizo gani?” Niliwaza kwa hamaki.

Maisha yale ya kuchungwa nilikuwa siyataki.

Nikaurudisha mbele uso wangu haraka na kuongeza mwendo. Kama atagundua ninamkimbia yeye shauri yake. Nani alimwambia anifuatefuate, nilisema peke yangu nikiwa nimechukia.

Nilikatiza tena kwenye vichochoro vingine nikatokea katika mtaa aliokuwa anaishi Macheo, lakini sikwenda nyumbani kwake.

Niliwaza kwamba kama Alhakim yuko nyuma yangu ataona nikiingia.

Niliipita nyumba ya Macheo ili kumpoteza Alhakim. Nikatokea mtaa mwingine. Nikasimama kwenye kioski na kununua vocha. Hapo nilikuwa ninamtega Alhakim kuona kama atatokea.

Baada ya kununua vocha na nilipoona simuoni tena ndipo nikarudi tena kwenye mtaa wa akina Macheo.

Hata hivyo, bado nilikuwa ninatembea huku ninatazama nyuma. Mzee nilishamchenga. Sikumuona tena.

Nilipoifikia nyumba yake, nilisukuma mlango na kuingia ndani harakaharaka.

Macheo aliyekuwa ameketi sebuleni akitazama video za muziki alishtuka alipoona ninaingia bila hodi.

“Vipi?” Aliniuliza huku akinitazama usoni.

“Poa tu,” nikamwambia na kuketi kwenye sofa.

“Mbona unatweta?”

“Kulikuwa na mzee ninayemkimbia…”

“Unamkimbia? Ana nini? Kichaa?”

“Si kichaa, ni mzima na akili zake bali alikuwa ananifuatilia…”

“Anakufuatilia, anakufahamu?”

“Ndiyo nilikuwa nimefika kwako kukueleza kuhusu yeye, kumbe naye alikuwa ananifuatilia na gari. Nashuka tu kwenye daladala nikamuona. Nikamkwepa na kuingia kwenye vichochoro. Kumbe aliacha gari na kunifuata kwa miguu…”

“Sasa ana tatizo gani?”

“Baba yangu alikuwa anafanya kazi ya udereva kwake. Huyo mzee kila akifika nyumbani kumtazama baba baada ya kuumia mguu alikuwa ananiona. Akamwambia baba kuwa anataka kunioa. Baba akakubali, akamwambia ampe shilingi milioni mbili za uchumba. Mzee akazitoa…”

Nikamuona Macheo akigwaya.

“Kumbe mwenzangu umeshapata mchumba!”

“Nifanye nini wangu? Wazazi wangu wamemtaka!”

“Duh! Sasa mbona unaendelea kufika kwangu?”

“Hutaki nifike tena baada ya kukwambia hivyo?”

“Hapana. Nimepata uoga. Umekuwa mchumba wa mtu na mwenyewe anakufuatilia.”

“Huo uchumba wake hautaharibu uhusiano wetu…”

“Kweli?”

“Uhusiano wetu utaendelea tu. Kila mtu anataka mapenzi. Na mapenzi unayapata kwa yule umpendaye.”

“Kwa hiyo huyo mchumba hukumpenda?”

“Kwa kweli sikumpenda, kwanza ni mzee sana!”

“Lakini ana pesa?”

“Pesa anazo. Ameniambia ataninunulia gari na hivi karibuni tutakwenda kufanya shopping Zanzibar kwa ndege.”

“Walichokosea wazazi wako ni kwamba hawakutaka kufahamu mawazo yako. Kwa vile wao ni wazazi, wakaona watoe wao uamuzi.”

“Hilo ni kosa, lakini siwezi kuwalaumu kwa sababu hivi sasa baba yangu hafanyi kazi, lakini analipwa mshahara kila mwezi na Alhakim na ni kwa sababu yangu.”

“Sasa, hivi alivyokuona huku anahisi ni kwa nani wako?”

“Nadhani anashuku kuwa nina mtu wangu huku.”

“Akitugundua itakuwa vipi?”

“Sitaki agundue, ndiyo maana nimemkimbia na siku atakaponiuliza nitamwambia nilikuwa ninaenda kwa shangazi yangu.”

“Sasa utakuwa unafika huku kiwiziwizi?”

Je, nini kiliendelea? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.


Loading...

Toa comment