Mfu Aliyerudiwa na Uhai-7

ILIPOISHIA IJUMAA…

“Kwa vile mama yako ndiye amesema hivyo, nitafanya bidii nipate hizo pesa kabla ya wiki hii kumalizika.”

“Itakuwa vyema kama zitapatikana haraka.”

 

SASA ENDELEA…

INA maana kwamba Alhakim akirudishiwa hizo pesa na uchumba utakuwa umekwisha?”

“Sasa nani atamkubali mchumba aliyetiwa mimba na mtu mwingine?”

“Kwa hiyo mimi ndiye nitakuwa mchumba wako?”

“Si unafahamu mila zetu, wewe ndiye umeniharibu na ndiye utakayenioa.”

“Baba anafahamu hivyo?”

“Baba hafahamu chochote. Mama ndiye niliyezungumza naye. Sasa labda yeye atamwambia.”

“Kwa hayo mawazo kwamba nirudishe hizo pesa za Alhakim yametoka kwa mama?”

“Yametoka kwa mama. Ameona mambo yameshaharibika sasa anataka kuyaweka sawa. Alihisi tatizo kubwa ni pesa za watu.”

 

“Ni lazima tufahamu na mawazo ya baba, ni kama hayo ya mama au atakuwa na mawazo mengine.”

“Mshauri wa baba ni mama. Kama mama amesema hivyo, baba hatakuwa na kipingamizi. Watazungumza wenyewe.”

“Sasa mimi nitahangaikia hizo pesa. Kwa upande wangu pia sipendi yatokee matatizo kwa Alhakim.”

“Nitakwenda kumueleza mama ulivyoniambia.”

Kidogo nilimuona Macheo akiwa amepata ahueni. Na kutokana na maelezo ya Macheo, mimi pia nilipata ahueni.

 

Sote wawili tukahisi furaha ndani ya mioyo yetu. Tulikuwa kama tumeutua mzigo mzito uliokuwa unatuelemea.

Niliporudi nyumbani nikamueleza mama tulivyozungumza na Macheo.

“Sasa hizo pesa atazileta lini?” Mama akaniuliza.

“Ameniambia wiki hii.”

“Itabidi azilete yeye mwenyewe ili tuweze kumtambua.”

“Nitamwambia azilete mwenyewe. Kwani umeshamwambia baba?”

 

“Nilikuwa ninasubiri maelezo kutoka kwa huyo mwanaume. Sasa kama amesema atatoa hizo pesa, nitakuwa nimeshapata maelezo ya kumwambia baba yako ingawa ninafahamu kwamba atakasirika sana kwa sababu umeharibu heshima yake kwa Alhakim.” Hapo sikusema kitu. Nilinyamaza kimya.“Sasa utamueleza lini baba?”“Nitamueleza leo.”“Sasa akiniita nitamwabia nini?”“Swali hilo unamuuliza nani? Kwani mimi umenieleza nini?”“Wewe ni mama, yule ni baba. Si umesema ukimwambia atakasirika!” “Kama atakasirika utafanya nini na kosa limeshatokea?” “Basi akiniita na wewe uwe hapohapo.”

Mama hakukubali wala kukataa, nilipomwambia hivyo aliinuka na kwenda uani kuendelea na shughuli zake. Nikabaki peke yangu nikiwaza.

 

Nilikuwa ninamuonea haya sana baba kuliko mama. Akiambiwa ile habari na akifahamu nina mimba, kwa kweli nitamkwepa. Sitaweza kuusogeza uso wangu mbele yake.

Mzee yule mawazo yake yote yalikuwa kwa Alhakim. Kitendo cha Alhakim, mtu mwenye pesa zake, kunitaka mimi si tu kilimpa matumaini ya maisha baba yangu, bali kilimtia fahari kuona kwamba mwanawe ataolewa na mtu mwenye pesa.

Nilikuwa ninafahamu kwamba siku zote baba yangu alikuwa akiombea nimalize masomo ili niolewe na Alhakim. Sasa akisikia nimepata mimba, sikuweza kuelewa atafedheheka kiasi gani.

Lakini tatizo ndiyo limeshatokea. Tangu hapo Alhakim sikumpenda licha ya kuwa na pesa. Niliyekuwa nikimpenda ni Macheo ambaye nilianzana naye tangu nikiwa kidato cha tatu.

 

Lakini nguvu ya wazazi wangu ndiyo iliyonifanya nimkubali Alhakim licha ya kuwa mtu mzima kama baba yangu. Sikupanga nifanye ufisadi wowote wala Macheo hakupanga hivyo. Kilichotokea kilikuwa ni bahati mbaya. Sikupenda kitokee.

Siku ile ambayo mama aliniambia atazungumza na baba, asubuhi yake baada ya kunywa chai, baba akaniita sebuleni. Moyo wangu ulishtuka sana. Nilishafahamu nilichokuwa ninaitiwa. Nikaenda sebuleni kumsikiliza.

“Kaa hapo,” akaniambia.

 

Uso wake na sauti yake viliniashiria kuwa alikuwa amechukizwa.

Baada ya kukaa, akaniambia.

“Mwanangu kwa nini unanifanya hivi?”

Ili kukwepa macho yake makali yaliyokuwa yakinitazama, niligeuza uso wangu upande mwingine.

“Kama ulikuwa humtaki huyu mchumba ungesema kuliko kunifedhehesha kiasi hiki!” Baba aliendelea kuunguruma. Mama hakuwepo. Moyoni mwangu nilikuwa ninamuita mama awepo pale ili amtulize baba.

 

“Mama uko wapi?” Nilikuwa nikisema peke yangu.

“Sasa mimi nitamwambia nini Saidi Omar (Alhakim) wakati ameshatoa pesa zake kwa sababu yako?”

“Pesa zitatolewa.” Nilikuwa nikimwambia baba kimoyomoyo, lakini sikuthubutu kupandisha sauti.

“Saidi Omar ataona sisi si watu wastaarabu kabisa. Mimi sina hata uso wa kumtazama..!”

Sikumlaumu baba ingawa kweli nilikuwa nimemfedhehesha, lakini nilifahamu alikuwa akitetea maslahi yake kwa Alhakim. Alikuwa akipewa pesa burebure kwa sababu yangu. Alhakim akifahamu nimetiwa mimba hatampa tena pesa baba.

 

Baba aligeuza uso wake pembeni, akalitazama kwa ghadhabu kabati alilokuwa amelielekea kama vile ndilo lililomkosea.Pale ndiyo niliona kama baba alikuwa ameghadhibika.

“Wanaume walikuwa wanakusaidia nini. Kama ni pesa Saidi Omar alikuwa anakupa. Mama yako alikuwa ananiambia…” Baba alisema kama aliyekuwa akisema peke yake kwani uso wake ulikuwa umeelekea kwenye kabati.

Baada ya kimya cha sekunde chache, baba aliyarudisha macho yake kwangu.

 

“Sasa hebu niambie ni mwanaume gani uliyenaye,” akaniuliza. Alikwepa kuniambia ni mwanaume gani aliyekutia mimba.

“Anaitwa Macheo,” nikamwambia. Sauti yangu ilitokea kwa mbali kama niliyekuwa ndani ya shimo.

“Anaishi wapi?”

“Tabata.”

“Anafanya kazi gani?”

 

“Anafanya kazi bandarini.”

“Anafanya kazi gani, kazi ya ukuli au..?”

“Ni afisa…”

“Afisa gani anayeharibu mabinti wa watu?”

Aliponiuliza hivyo, macho yake yaliwaka kwa hasira. Alionekana alikuwa na mengi ya kunisema, lakini alishindwa kunimalizia maneno kwa sababu nilikuwa mwanaye, tena wa kike. Maadili yalikuwa yanamzuia. Vinginevyo angenichamba vya kutosha.

Baada ya kunitazama kwa sekunde kadhaa, akaendelea kuniambia.

“Huyo Macheo anaweza kurudisha pesa za watu?”

 

“Anaweza.”

“Ataleta hapa shilingi milioni mbili?”

“Ndiyo, ataleta.”

“Mama yako yuko wapi?”

“Yuko uani, ana kazi.”

“Hebu muite.”

 

Nikainuka kwenda uani. Mwili wote ulikuwa umetota kwa hofu.

“Mama unaitwa na baba,” nikamwambia mama.

Tulifuatana hadi sebuleni. Nikakaa mahali nilipokuwa nimekaa kwanza na mama akakaa kando yangu.

“Msikilize mwanao anavyosema. Ameniambia kwamba huyo mwanaume wake atatoa hizo pesa shilingi milioni mbili ili kutengua uchumba wa Saidi omar…” Baba alimwambia mama kisha akanitazama mimi.

“Si ndiyo ulivyosema hivyo?” Akaniuliza kwa mkazo.

“Ndiyo nimesema kwamba atatoa pesa hizo,” nikasema.

“Sasa atazileta lini?”

“Mpaka aambiwe!”

 

“Aambiwe na nani?”

“Yeye ndiye atakayemwambia,” mama akaingilia kati.

“Sasa mimi ninawapa wiki mbili. Huyo mtu afike hapa akiwa na hizo pesa.” Baba akasema.

“Sawa…”

Je, nini kiliendelea? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.


Loading...

Toa comment