Mfuasi wa Trump Ahukumiwa miaka 4 na nusu Gerezani kwa Kuvamia Bunge
Mtu mmoja kutoka jimbo la Arkansas hapa Marekani aliyepigwa picha akiwa ameweka miguu yake juu ya dawati, katika afisi ya Spika wa wakati huo, wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi, Jumatano alihukumiwa kifungo cha miaka minne na nusu gerezani.
Richard Barnett, mwenye umri wa miaka 63, alidaiwa kujiunga na kundi la watu waliovamia majengo ya bunge la Marekani mwaka 2021.
Barnett alipigwa picha na mpiga picha wa shirika la habari la AFP, akiwa amekalia kiti kwenye afisi ya pelosi, na picha hiyo ikawa mojawapo ya vielelezo vya uasi wa Januari 6, 2021.
Barnett alikuwa ameungana na wafuasi wa Rais wa wakati huo Donald Trump, ambao walivamia Bunge lilipokuwa likikutana kumuidhinisha Mdemokrat Joe Biden, kama rais ajaye wa Marekani.
Mahakama hiyo ya hapa mjini Washington, ilimtia hatiani Barnett mwezi Januari kwa makosa manane, ikiwa ni pamoja na kuzuia bunge kuidhinisha uchaguzi, kuingia kinyume cha sheria katika majengo ya bunge na kusabaisha fujo na kutumia silaha hatari.
Waendesha mashtaka walikuwa wamemtaka Jaji Christopher Cooper kumhukumu kifungo cha miaka saba gerezani.