The House of Favourite Newspapers

MFUNGO WAMBADILI SANCHI!

Jane Rimoy ‘Sanch’

MFUNGO wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani umeonekana kumbadili mwanamitindo Jane Rimoy ‘Sanch’ kutoka kwenye kuvaa mavazi ya kihasarahasara ambayo amekuwa akiyavaa na sasa kutinga mavazi ya heshima kwa kuvaa mabaibui kuendana na wanaofunga.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Sanch amekuwa akitupia picha mbalimbali zinazomuonesha akiwa kwenye mavazi ya baibui na kuandika kuwa anapata baraka nyingi.

Hata hivyo, wapo waliodai kuwa mrembo huyo amebadilika kwa sasa lakini wapo wanaodai kuwa anavaa hivyo kwa sababu ya kutangaza maduka ya mabaibui ingawa yeye amekuwa akitaja nguo yake amenunua wapi lakini wakati mwingine anaishia tu kuandika kuwa ni baraka za Mwenyezi Mungu.

Baadhi ya mashabiki wamekuwa wakimpongeza na wengine kumshawishi kuendelea kuvaa mavazi hayo hata baada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwani anapendeza na kujistiri pia.

“Nakushauri uvae mavazi haya yanakupendezesha sana na mbali na kuonekana umependeza lakini pia yanaustiri mwili wako,” aliandika shabiki mmoja anayeitwa Ali.

Mbali na shabiki huyo wengine walimwambia kuwa ana sura nzuri akijistiri anapendeza zaidi kwani mwili wake una mvuto wa kipekee akiwa katika mavazi ya kujistiri.

Alipotafutwa na Risasi Mchanganyiko ili kuzungumzia maoni hayo ya mashabiki wake, Sanch hakuweza kupatikana mara moja lakini mara kadhaa amekuwa akisema anapendelea kuvaa vile anavyojisikia na hakuna wa kumpangia maisha yake.

Ukiingia kwenye ukurasa wake wa Instagram, Sanch ambaye ana umbo lenye mvuto wa kipekee, amekuwa kinara wa kutupia picha za nusu utupu akiwa katika nchi tofautitofauti na kusindikiza na jumbe mbalimbali.

STORI: Mwandishi Wetu, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.