Mganga Mkuu wa Manispaa ya Temeke Alivyozindua Dispensari ya Kisasa

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam, Dk. Jonas Lulandala amezindua dispensari ya kisasa iitwayo HNS iliyopo Mtaa wa Mwembe Bamia, Kata ya Chamazi jijini Dar na kutoa huduma za vipimo na matibabu bure kwa watu zaidi ya 100 waliofika kwenye hafla ya uzinduzi huo.
Akizungumza baada ya kuikagua na kuizindua dispensari hiyo, Dk. Lulandala ameupongeza uongozi wa wa dispensari hiyo kwa kuamua kuisaidia serikali katika kutoa huduma za afya kwa na kufanya uwekezaji huo eneo hilo ikiwa na vifaa vya kisasa kabisa na watoa huduma wenye vigezo vinavyostahili.

“Baada ya kufika hapa nilikagua maeneo mbalimbali ikiwemo maabara, vyumba vya kujifungulia wajawazito, vyumba vya kulaza wagonjwa, sehemu ya mapokezi na kujionea jinsi sehemu zote zilivyokidhi ubora.

“Na nimejionea jinsi hata mifumo yake kuanzia mgonjwa anapofika mapokezi na kila idara anayoingia taarifa zake zote zinasomana kwenye mfumo mmoja.
Hivyo ndivyo dunia ya kisasa inavyohitaji, niupongeze sana uwekezaji huu wa kisasa”. Alisema Dk. Lulandala.

Naye Mganga Mkuu wa Dispensari hiyo, Dk. Sharif Mollel alianza na kuupongeza utawala wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira bora kwa wawekezaji hali iliyowapa nguvu hata wao kuweza kuwekeza dispensari hiyo ya kisasa ambayo itakuwa mkombozi kwa wakazi wa eneo hilo na wengineo kwa ujumla.

“Napenda kuwakaribisha wakazi wote wa eneo hili la Chamazi Mwembe Bamia na wengineo kuja kujipatia huduma bora za afya kwenye dispensari yetu hii.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwembe Bamia, Abeid Kindamba kwa upande wake yeye aliushukuru uongozi wa dispensari ya Hns kwa kuamua kwenda kuwekeza kwenye eneo lake hivyo kuwapunguzia wananchi wake adha ya kwenda mbali kutafuta huduma bora za afya. HABARI/PICHA NA RICHARD BUKOS /GPL