The House of Favourite Newspapers

Mgombea Aangua Kilio Kwenye Mkutano wa Kampeni

0

MGOMBEA udiwani wa Kata ya Mumbaka, Masasi mkoani Mtwara, Salum Mwinyikheri, ameangua kilio mbele ya wananchi wakati akiomba kura.

 

Akihutubia wananchi wake kwenye mkutano aliouandaa, Mwinyikheri alianza kumwaga machozi na kufuatiwa na kilio cha kwikwi akieleza kuumizwa na changamoto zilizopo kwenye kata hiyo, hasa mgogoro wa ardhi na umilikiswaji ardhi.

 

Kabla ya kuanza kububujikwa machozi, Mwinyikheri alisema kata hiyo ina matatizo mengi na kama angepata ridhaa ya wananchi, angetumia uwezo wake wote kumaliza changamoto hizo na kufanya kata hiyo iwe mahali salama pa kuishi.

 

Wakati akizungumza maneno hayo, ghafla mgombea huyo alianza kufuta machozi huku yakiongezeka kutiririka. Baadaye baadhi ya viongozi wenzake walimfuata na kumbembeleza huku akitoa kwikwi za kilio.

 

“Kinachonitoa machozi hapa ni kuwa, natamani sana kuwa diwani wa hapa ili niwasaidie wananchi wa kata hii maana wana changamoto nyingi ikiwemo maji, barabara, afya kwa kinamama wajawazito na migogoro ya ardhi,” amesema.


Alisema, wananchi wa kata hiyo hawapaswi kufanya makosa kwa kuwachagua wagombea kutoka nje ya CUF, na kwamba wagombea wa chama chake watakapochaguliwa, wataona mabadiliko kwa muda mfupi.

 

“Ili tupate maendeleo ya haraka, wananchi wanapaswa kuchagua wagombea wa CUF kuanzia udiwani, ubunge na urais,” alisema Mwinyikheri.

 

Mgombea huo hakuweza kumaliza hotuba yake baada ya kuangua kilio, viongozi na baadhi ya wanachama walimfuata na kuanza kumbembeleza na kisha kumtoa uwanjani na kumpeleka kuketi kwenye kiti.

Leave A Reply