The House of Favourite Newspapers

Mgomo wa Wafanyakazi Uwanja wa Ndege Waleta Mzozo

 

USAFIRI wa ndege umetatizika na abiria wamekwama katika uwanja mkuu wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi, Kenya.

 

Wafanyakazi wa usafiri wa ndege wameanza mgomo kupinga mpango wa kuunganishwa shughuli za usimamizi wa uwanja huo wa ndege kati ya shirika kuu la ndege nchini Kenya Airways na mamlaka ya usimamizi wa viwanja wa ndege, KAA.

 

Kadhalika wafanyakazi wanatuhumu na kupinga makosa yanayofanyika katika uajiri wa wafanyakazi.

 

Muungano wa wafanyakazi hao (KAWU) unataka kujua sababu halisi za mipango hiyo ya kuunganisha shughuli kati ya pande hizo mbili na umeitisha mageuzi katika usimamizi wa shirika la ndege nchini humo,  Kenya Airways na shirika la usimamizi wa viwanja vya ndege KAA.

 

Hata hivyo, mamlaka hiyo ya KAA imetoa taarifa hapo jana ikieleza kuwa ilani ya mgomo iliyowasilishwa na muungano huo wa wafanyakazi wa usafiri wa ndege umesitishwa kufuatia agizo la kuzuia mgomo kutoka mahakama ya uajiri na kazi lililotolewa  jana, Jumanne.

 

Katika ujumbe wake, mamlaka hiyo imetoa hakikisho la shughuli kuendelea kama kawaida.

 

 

Ujumbe huo ulijibiwa na wananchi waliolezea kutatizika kwao kutokana na hali iliyoshuhudiwa hivi asubuhi.

 

 

Vyombo vya habari nchini vinaeleza kwamba licha ya mamlaka hiyo ya viwanja vya ndege kutangaza kwamba mgomo umesitishwa, ndege zote hazikusafiri kutoka uwanja huo wa JKIA.

 

 

Taarifa zinaeleza kwamba hakuna ndege iliyoondoka tangu saa tisa alfajiri Jumatano huku mamia ya wasafiri wakiwa wamekwama.

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.