The House of Favourite Newspapers

Mhe.Magufuli, kuna hili jipu kubwa, nalo litumbue!

0

raisiiRais John Pombe Magufuli.

LEO ni siku ya kwanza ya mwaka huu 2016, ikiwa ni zaidi ya takriban miezi miwili tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu ulioiweka madarakani serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli.

Wananchi wa kada zote, wameweka imani yao kwa serikali mpya, wakiamini itaweza kutatua kero nyingi zilizokuwa zikiwakabili katika nyanja mbalimbali za maisha yao ya kila siku.

Hakika, karibu katika kila sekta, kulikuwa na vitu ambavyo vilikuwa vinakera, vinaudhi na hata wakati mwingine kuchukiza.

Dalili zimekuwa nzuri angalau siku hizi za mwanzo, kwani viongozi wote, kuanzia rais, waziri mkuu, mawaziri, manaibu wao na hata wasimamizi wa ngazi nyingine, wanaonesha kupania kutekeleza kwa vitendo ahadi zote zilizotolewa na Rais Magufuli wakati wa kampeni.

Hata hivyo, kuna jambo moja la msingi ambalo ni lazima wahusika walifanyie kazi, kwa sababu kwa miaka mingi tulitengeneza serikali iliyofanya kazi kwa mitandao iliyotengenezwa na watumishi wa umma kwa masilahi yao.

Mitandao hii, ukiachana na ule wa wanasiasa, ipo katika sekta ya ardhi, madini, utalii, mazingira, afya na maeneo mengine ambayo siku zote wanufaika ni walewale na waathirika ni walewale.

Katika ardhi kwa mfano, wapo watu ambao walikuwa madalali wa watumishi wizarani na katika halmashauri kwa wahitaji wengine. Hawa ndiyo walioweka ugumu wa kupata hati za kumiliki ardhi, waliotengeneza migogoro na ndiyo viungo wakubwa wa matapeli wanaowadhulumu walalahoi viwanja vyao.

Wanajuana, wana watu wao wanaosaidia utapeli katika mabaraza ya ardhi ya vijiji, kata, wilaya hadi mkoa. Waziri anatakiwa kuuvunja mtandao huu ili haki ianze kuonekana kutendeka. Kila siku wenye viwanja vya kuuza ni walewale!

Hali kama hii ipo katika sekta ya maliasili na utalii hasa katika uuzwaji wa vitalu vya uvunaji mazao ya miti, magogo na bidhaa nyingine. Kila mara wanaofanikiwa kupata vibali vya kuvuna ni walewale ili hali kila mwananchi ana haki ya kupata kibali. Katika nchi inayothamini wananchi wote, angalau suala hilo lingefanywa kwa mzunguko na kwa kiasi kidogokidogo.

Hata huko kwenye madini nako kuko vilevile, wanaopata vibali na vitalu ni walewale, hata kama hawalipi kodi ipasavyo, au wanakosa vigezo vya kushindana na waombaji wapya. Hii ni kwa sababu ya mtandao mpana waliojijengea, wenye sura ya rushwa.

Hali kama hiyo utaikuta pia katika sekta nyingine kama afya, elimu na kadhalika. Huduma za serikali zinatolewa kuwapendelea watu f’lani, huku kada nyingine zikiwa zinaonewa, kukamuliwa na kudhulumiwa.

Serikali inapotaka kuondoa kero za wananchi wa kawaida ni lazima kwanza kuivunja mitandao hii kutoka kwa watumishi wa ndani. Utashangaa kuna mtu siyo mtumishi wa umma, lakini yeye ndiye mwenye kuwezesha fomu f’lani kujazwa, hati f’lani kusainiwa na hata nyaraka f’lani kupatikana.

Watu wa aina hii ndiyo wanaotumiwa kama makuwadi na wakubwa wa idara, wakisambaza rushwa kwa maofisa na hivyo kuwanyima haki mamilioni ya wananchi.

Mawakala hawa na watu wanaofanya nao kazi wanajulikana, kwa sababu wanaonekana nje ya ofisi za umma kuanzia asubuhi hadi jioni kila siku. Pale Kisutu Mahakamani wapo, Wizara ya Ardhi wapo, Maliasili na Utalii wapo, Kilimo na uvuvi wapo na hata pale Bohari Kuu wanapatikana.

Hawa ni jipu kubwa kuliko majipu mengine, maana yanawaumiza wananchi wa hali ya chini moja kwa moja.

Leave A Reply