The House of Favourite Newspapers

‘MHENGA’ ANASWA JUU YA UNGO MUBASHARA (PICHAZ + VIDEO)

0
‘Mhenga’ akiwa juu ya ungo baada ya kukutwa na wananchi siku ya Jumanne iliyopita asubuhi nyumbani kwa mkazi mmoja eneola Tuangoma, Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

MWANAUME mmoja aliyedaiwa kujihusisha na vitendo vya kilozi ‘Mhenga’ anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 33-35, ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, asubuhi ya Jumanne iliyopita alinaswa akiwa juu ya ungo, nyumbani kwa mkazi mmoja eneo la Toangoma, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

HUU HAPA MWANZO WA MCHEZO

Chanzo cha uhakika kiliwasiliana na Uwazi kutoka eneo la tukio na kueleza kuwa asubuhi na mapema, watu waliokuwa wakielekea kwenye shughuli zao za kijamii, walishangaa kumkuta mwanaume huyo aliyejifunga nguo nyekundu begani, mshipi kichwani na nguo nyeusi (kaniki) kiunoni, akiwa amejiinamia, huku mwili wake uliokuwa na majivu ukiwa ndani ya ungo!

…Baada ya kuzinduka. Kulia ni ungo aliokuwa ameukalia ukiwa na kioo.

 MSIKIE SHUHUDA ENEO LA TUKIO

“Watu wameamka asubuhi wanawahi kwenye mishemishe zao, ghafla kufika hapa wanamuona huyu jamaa amekaa hapa pembeni ya hii nyumba, jinsi alivyoalivyo, inaonekana wazi kuwa ni kama mhenga wa mambo ya kishirikina, watu wakaanza kujaa.

“Wanamsemesha hasemi chochote, kuangalia ndani ya ungo aliokaa, tukaona kuna vitu vya ajabuajabu kama bangiri, tunguri, hirizi na kioo, watu wakaanza kusema eti ile ni saitimira akiwa angani,” alisema shuhuda mmoja.

Polisi na wananchi wakiwa eneo la tukio.

WANANCHI WAJA JUU

Shuhuda huyo aliliambia Uwazi kuwa baada ya wananchi kukusanyika kwa wingi na kujiridhisha kuwa jamaa huyo ni mtaalam wa mambo yale, wakaja juu na kutaka kumtia kiberiti.

“Ilikuwa mshikemshike kwelikweli, watu wakataka wamchome moto wakidai kuwa hawa watu ndiyo wanaleta matatizo uswahilini, lakini hata hivyo, kuna wengine wakasema wasifanye hivyo, wamfikishe kwenye vyombo vya dola,” alisema shuhuda huyo.

Wale waliotaka asipigwe wakazidiwa nguvu, lakini bahati nzuri, wakapiga simu polisi na bahati ilikuwa upande wa njemba huyo, baada ya askari waliokuwa na bunduki kuwahi eneo la tukio mapema tofauti na ilivyozoeleka.

Umati uliofurika kushuhudia tukio hilo.

RISASI ZARINDIMA

Mara baada ya ‘Noah’ ya polisi kuwasili eneo la tukio na kutaka kumchukua mtu huyo, upinzani mkali ulitokea, wananchi hao wakitaka waachwe wafanye mambo yao, lakini ili kutuliza hali, iliwalazimu askari kupiga risasi kadhaa hewani, ambazo zilifanikisha kuwarudisha nyuma raia hao na hivyo kuwapa fursa ya kumchukua kijana huyo na kuondoka naye.

 

WAJUZI WAFAFANUA KILICHOTOKEA

Kwa mujibu wa shuhuda wetu, watu waliokuwepo eneo la tukio, walisikika wakisema kuwa kijana huyo alikuwa katika ‘safari’ zake za kikazi usiku, lakini alipofika eneo hilo, ‘alijikanyaga’ na hivyo kulazimika kutua bila kupenda.

“Wajuzi wa hizo kazi walisema jamaa ama alikusudia kufanya mambo yake kwenye nyumba hiyo, au alikatiza tu katika anga hiyo bahati mbaya, akakuta huyo mwenye nyumba yuko vizuri, kwa hiyo akakwama.

Akichukuliwa na polisi.

“Pale alipoangukia, wanasema asingeweza kuondoka bila kuonwa na watu. Baada ya polisi kumchukua, hakuna aliyefuatilia kilichoendelea,” alisema shuhuda huyo.

POLISI WATHIBITISHA

Uwazi lilifanya juhudi za kufika katika Kituo Cha Polisi Maturubai kilichopo Kizuiani, Mbagala ambako askari waliokutwa hapo, kwa sharti la kutotajwa majina kwa vile hawakuwa wasemaji walikiri kutokea kwa tukio hilo.

“Ni kweli, jamaa tulimkamata kule Toangoma na tukamleta hapa, lakini tusingeweza kumfikisha mahakamani kwa vile hatuna kosa la kumshtaki nalo, maana kama mnavyojua, serikali haiamini mambo ya kishirikina.

“Tulichofanya tulimshikilia hapa kwa muda kwa ajili ya kulinda usalama wake, tulipoona hali imetulia, tukamwachia aende zake,” alisema mmoja wa askari mwenye cheo kituoni hapo.

Hata hivyo, Uwazi liliwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke (SACP) Gilles Muroto kupata taarifa rasmi, lakini katika ujumbe mfupi aliotuma baada ya kupokea simu yetu, alisema alikuwa katika msafara wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyekuwa katika ziara ya kikazi mkoani Dar es Salaam bila kutoa ufafanuzi zaidi.

Uwazi lilifika Toangoma, sehemu aliyokutwa mtu huyo na kuambiwa na wenyeji kwamba nyumba aliyokutwa ni mpya na tajiri haishi hapo kwani bado hajahamia.

STORI: RICHARD BUKOS NA ISSA MNALLY | UWAZI | GLOBAL PUBLISHERS

Leave A Reply