The House of Favourite Newspapers

MIAKA 56 YA UHURU NA MAFANIKIO YA JPM

LEO ni siku ya kipekee kwa Watanzania wote kwani Taifa letu linaadhimisha miaka 56 ya uhuru tukiwa na amani na utulivu.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Uhuru Wetu ni Tunu, Tuudumishe, Tulinde Rasilimali Zetu, Tuwe Wazalendo, Tukemee Rushwa na Uzembe”.

Tunaadhimisha miaka hiyo chini ya uongozi imara wa Rais Dk John Magufuli. Miaka 56 ni mingi, lakini pia yenye changamoto nyingi.

Katika uchambuzi wa siku hii kwa kifupi tutaangalia mchango ama mafanikio ya Serikali ya Rais Magufuli ambaye anasisitiza umuhimu wa kufanya kazi.

Itakumbukwa kuwa, tangu aingie madarakani ameleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji ndani ya serikali, ikiwa ni pamoja na kusisitiza uwajibikaji kwa watendaji.

Kama alivyokuwa Rais wa Awamu ya Kwanza na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rais Magufuli ameonesha ni mzalendo mkubwa kwa nchi.

KUFANYA KAZI

Hii ni kutokana na ukweli kuwa ametumia kipindi kifupi cha uongozi wake kuamsha ari ya watu kufanya kazi kwani hakuna cha bure.

Katika hili ameweka bayana kuwa, chini ya serikali yake asiyefanya kazi atakufa njaa. Hakupenda kuremba maneno na badala yake anasema ukweli.

Hii imesaidia vijana kujituma badala ya kutumia muda wao kukaa vijiweni wakipiga soga au stori ambazo hazina tija kwao, familia na hata taifa.

Kwa hiyo, kila kijana mwenye nguvu/Mtanzania mwingine yeyote anatambua kuwa ili tonge liende mdomoni ni lazima afanye kazi.

Wengi wameanza kubadilika. Kila mmoja kwa nafasi yake anafanya kazi. Hii ni hatua nzuri. Ndivyo China ilivyofanya na leo hii ipo mbali kimaendeleo.

UTOZAJI KODI

Hakuna nchi inayoweza kupiga hatua ya kujivunia kimaendeleo bila kutoza kodi. Kwenye hili Rais Magufuli hana mchezo na mtu.

Watanzania wameanza kuhamasika kulipa kodi na matokeo yake ni kwamba kile kinachopatikana kinasaidia kukuza maendeleo yetu wenyewe.

Unapotoza kodi unasaidia pia kulinda bidhaa za ndani kwa sababu kila bidhaa inayoingia kutoka nje sharti ilipe kodi, asiyetaka anabaki hukohuko nje.

RUSHWA

Hii ni vita ngumu, lakini itoshe kusema hapa, kwamba Rais Magufuli ametafuna mfupa uliowashinda viongozi wengi waliopita. Kwenye tatizo hili tulifikia pabaya.

Wakati mmoja, Mwalimu Nyerere alisikika akisema; “Taifa linanuka rushwa” hivyo Magufuli analiponya taifa na ugonjwa huo hatari.

Penye rushwa, wanyonge wanaumia na matajiri wanarukaruka kwa furaha. Penye rushwa kitu kinachoitwa haki hakuna.

SERIKALINI

Rais Magufuli ameleta nidhamu ya kiutendaji serikalini. Kipindi cha nyuma hali ilikuwa si nzuri. Sehemu za ofisi zilionekana kama maeneo ya kutalii.

Ilikuwa ni kawaida ukifika ofisi hii au ile unahitaji huduma unaambiwa; ‘huyu katoka njoo baadaye’. Tabia hii imeanza kupotea. Watumishi wapo ofisini.

Kama ni huduma unahitaji unashughulikiwa haraka unaendelea na kazi zako. Hivi ndivyo inavyotakiwa na Rais ameyeyusha barafu iliyokuwa imeganda.

USAFI

Usafi ni tabia ya mtu, lakini Watanzania wengi tulijisahau mno eneo hili. Ukiondoa usafi wa mwili, usafi wa mazingira tulijisahau vya kutosha.

Rais huyu alipoingia madarakani alianza kampeni ya kufanya usafi na kuanzia hapo watu wamejiwekea utaratibu wa usafi katika maeneo yao.

Jiji kama la Dar es Salaam hali ilikuwa mbaya. Kila unakopita iwe ni Posta Mpya palikuwa hapafai. Ukiangalia pembeni kokwa la nazi au ganda la ndizi.

Pamoja na jitihada hizo bado suala la usafi linahitaji zaidi maeneo mengi ya nchi yetu. Miji yetu mingi ipo nyuma kwenye usafi wa mazingira.

Viongozi ni lazima wasimamie hili vizuri hasa kuanzia ngazi ya mitaa hadi taifa, vinginevyo jitihada za Rais Magufuli zitaishia ukingoni mara atakapoondoka.

ELIMU

Rais Magufuli amefanikiwa kutoa elimu bure kwa watoto wa Kitanzania na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu hasa wale wenye sifa zinazotakiwa.

Kwenye hili, kinachotakiwa ni walimu kufundisha vizuri na kusimamia mahudhurio ya wanafunzi ili elimu bure ilete mabadiliko nchini.

Endapo viongozi wa ngazi za chini hawatatimiza wajibu wao kusimamia vizuri elimu bure ni vigumu kupata matokeo chanya.

Kwa msingi huo, kila mdau wa elimu wakiwemo wazazi, ni lazima kila mmoja atimize lengo lake ili wanafunzi wanufaike vema na elimu hiyo.

Yapo mambo mengi yanayofanywa na serikali, ikiwemo kuboresha sekta ya afya, maji, umeme, barabara, viwanja vya ndege na matokeo yake yanaonekana waziwazi.

Kwa hiyo tunapoadhimisha miaka 56 ya Uhuru tuendelee kumuunga mkono Rais Magufuli chini ya kauli mbiu yake ya Hapa Kazi Tu.

Ili kupata undani wa miaka hii zaidi kuhusu mafanikio na changamoto, soma Gazeti la Uwazi siku ya Jumanne.

 Makala: Julian Msacky.

LIVE: Makeke ya JWTZ Maadhimisho ya Miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania

Comments are closed.