Miaka Minne Ndani ya Mapango ya Amboni – 31

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

“Nisamehe..nisamehe   sitarudi tena humu.”

 Mimi niliyekuwa nikitazama tukio hilo, nguvu zilikuwa zimeniishia na nilikuwa natetemeka.

 “Nikusamehe kwa kosa gani?” Kaikush akamuuliza yule mtu kwa jeuri.

 “Nisamehe…nisamehe …bwana mkubwa…” 

“Kwani wewe huna damu au huna ubongo?”

 “Jamani nakufaa…”

SASA ENDELEA…

Kaikush akanyoosha kidole chake cha shahada kilichokuwa na kucha ndefu na ngumu na kukikita kwenye utosi wa yule mtu. Kidole hicho kikazama chote!

Kufumba na kufumbua niliona damu ikiruka juu kutoka kwenye utosi wa mtu huyo kama maji yanavyoruka kutoka katika bomba lililotobolewa.

Kaikush akauweka mdomo wake kwenye ile tundu na kuanza kuifyonza ile damu huku akiwa amemshikilia yule mtu.

Hapo hapo nikageuka nyuma na kutimua mbio. Wakati wote miguu ilikuwa inaniuma lakini sikujua maumivu yale yalipotelea wapi kwani niliweza kukimbia kama vile miguu yangu ilikuwa mizima na sikuweza kuhisi maumivu yoyote.

Wakati nawafikia wenzangu, walipoona ninakuja mbio na wao wakakimbia. Nikawa nawafukuza. Kadiri nilivyozidi kuwafukuza na wao walizidi kunikimbia.

Sikuweza kujua walikuwa wakinikimbia mimi au walikuwa wakikimbia kitu gani. Nikawa nawapigia kelele kuwaambia wanisubiri.

“Nisubirini jamani, msinikimbie.”

Nilipowaambia hivyo mara mbili ndipo walisimama na kuningoja.

“Sasa mbona mnanikimbia?” nikawauliza nilipowafikia. Nilikuwa nikihema kama niliyekimbia kilometa kadhaa.

“Tulijua Kaikush alikuwa nyuma yako,” mmoja akanijibu huku naye akihema.

“Hapana, ni mimi tu,” niliwaambia huku nikishindana na pumzi zangu.

“Sasa mbona unakimbia na uko peke yako wakati mliondoka wawili?”

“Mwenzangu ameuawa?”

“Mlikutana na huyo jini?”

“Yeye ndiye aliyekutana naye. Nilimwambia aingie kufanya uchunguzi ili tujue kama Kaikush yupo au la, lakini nilikuwa namchungulia…”

Nilisita nikahema kidogo kabla ya kuendelea.

“Nikamuona anabisha kwenye ile sehemu ya Faiza, Faiza akatoka haraka na kumwambia aondoke kwani Kaikush anakuja. Kabla ya mwenzangu kugeuka Kaikush akatokea palepale akamshika…”

Nilinyamaza tena, sasa si kwa sababu ya kuvuta pumzi pekee bali maelezo yaliyofuata baada ya hapo yalinifanya nisite kwani yalikuwa yanasisimua.

“Alivyomshika alimfanya nini?” mtu mmoja akaniuliza.

“Alimtoboa utosi akawa anamfyonza damu…”

Wenzangu wote walitikisa vichwa kusikitika.

“Ikabidi mimi nikimbie…,” nikawaambia.

“Asije akaja na huku?” Mwenzetu mmoja akasema.

“Kama akija huku atatumaliza sote,” nikawaambia.

Bila kuambizana chochote tukajikuta tunasonga mbele kuondoka mahali pale kumkimbia Kaikush.

Sasa nikaanza kuisikia miguu ikiniuma. Yale maumivu ya zile mbio nilianza kuyasikia sasa.

Nilijitahidi kuendelea kutembea hivyo hivyo kusalimisha roho zetu. Tukafika mahali nikawa siwezi tena kutembea.

“Jamani siwezi tena kuendelea kutembea, miguu inaniuma vibaya sana. Safari yangu itaishia hapa,” nikawaambia wenzangu.

Sote tukasimama. Mimi nilikaa chini. Sikuweza kuendelea kusimama.

Wenzangu nao wakakaa.

“Sasa tutafanyaje?” mtu mmoja akauliza.

“Tupumzikeni kidogo,” nikawaambia.

Hakuna aliyenijibu chochote. Tukabaki kimya. Ule mwenge niliuacha kulekule. Pale tulipokuwa tumekaa hapakuwa na mwanga. Lakini kwa vile macho yetu yalishazoea kiza tulikuwa tunaonana.

Wakati tumekaa nilikuwa nikiichuachua miguu yangu. Wenzangu wengine walikuwa na afadhali. Sikuwasikia wakilalamika. Lakini huenda ni kwa sababu tulitoka katika mazingira tofauti.

Kwa upande wangu sikuwa mtu wa kupendelea kufanya mazoezi mara kwa mara. Hata kutembea kwangu kwa miguu kulikuwa ni kwa nadra sana.

Sasa kwa vile katika kipindi kile tulikuwa tunapoteza masaa mengi kutembea kwa miguu kutafuta njia itakayotutoa ndani ya pango lile, miguu yangu ilihisi kupata dhoruba ambayo haikuzoea.

Wakati ule tumekaa pale, tulianza kuulizana tunakotokea.

Mimi ndiye nilikuwa wa kwanza kujieleza. Niliwaambia wenzangu kuwa nilikuwa Mzanzibari niliyekuwa nikiishi Uingereza.

“Nilikuwa nimekwenda nyumbani Zanzibar kusalimia ndipo nikaja hapa Tanga kuzuru mapango ya Amboni.

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye gazeti hilihili Jumanne ijayo.


Loading...

Toa comment