The House of Favourite Newspapers

Miaka minne ndani ya mapango ya amboni – 33

0

ILIPOISHIA
“Loh! Poleni sana jamani kwa mateso mnayoyapata. Nilishawaambia tangu mapema kwamba hali ya hapa si nzuri. Sasa nitawasaidiaje kuwapa chakula na maji mliyokuwa mnahitaji?”
“Tafadhali kama hatutakusumbua tunakuomba utuletee wewe,” nikamwambia Faiza.SASA ENDELEA…

“Si kitu nitawaletea kwa vile nia yangu ni kuwasaidia.”
Kabla ya Faiza kuondoka nilimuuliza.
“Lakini unatuhakikishia kuwa hapa tulipo tuko salama?”
“Ninaamini mtakuwa salama. Kaikush hayupo.”
“Sawa.”

Faiza akaondoka. Kwa vile aliondoka na ule mwenge tuliendelea kumtazama hadi njia ilipopinda.
Ilichukua muda mrefu hadi Faiza aliporudi tena akiwa na chakula pamoja na maji.

Mimi sikuweza kula sana ila nilikunywa maji mengi kwa sababu ya kiu. Nilihisi afya yangu ilikuwa imeshaathirika. Tumbo langu halikuwa sawa na pia sikuwa nikijisikia vyema. Nilihisi kama vile ningepata homa.

Mmoja wa wale wenzangu naye alikuwa kama mimi. Lakini yeye alikuwa taabani zaidi. Alikunywa maji tu, hakutaka kula chakula.
Tulimbembeleza sana ale chakula japokuwa kidogo. Akasema hajisikii kula chakula.

“Kumbuka kwamba bado tuna safari ndefu ya kutafuta mlango wa kutokea, ni lazima uwe na kitu tumboni,” nikamkumbusha.
“Haya maji niliyokunywa yanatosha.”

Niligundua yule mtu alikuwa anakabiliwa na matatizo mengi. Mbali ya uchovu na kukata tamaa pia moyo wake ulikuwa umefadhaika kutokana na hofu ya kufa.

Lakini nilihisi kilichomuumiza zaidi na kumfanya ashindwe kula chakula ni mawazo ya kufa na kumuacha mchumba wake. Mwenyewe alituambia alikuwa amebakisha wiki mbili tu afunge naye ndoa.

Kwa vile alikuwa amekataa kula tuliona tumuache na tuendelee na safari yetu.Faiza akazidi kutupa moyo alipotuambia kuwa tutafika mahali tulipoingilia, akimaanisha kule kwenye mlango wa pango.

“Msinisahau jamani. Mkifanikiwa kutoka mtoe taarifa kuwa kuna kiumbe anateseka humu ndani,” Faiza akatukumbusha.

“Usijali, hilo ni muhimu. Kama tutafanikiwa kutoka ujue na wewe umeshakombolewa,” nikamwambia Faiza kabla ya kuagana naye.
Kwa vile na yeye alikuwa na kipande cha mwendo kurudi alikotoka, tulimuachia ule mwenge. Akaenda zake na sisi tukaanza tena safari ya kutafuta mlango wa kutokea katika pango hilo.

Safari hii mwendo wetu ulikuwa wa taratibu sana kwa sababu ya mwenzetu aliyeonekana kukosa nguvu kabisa.
Hata hivyo, mwendo huo wa taratibu uliendelea kupungua kadiri tulivyoendelea kwenda. Ghafla tulimuona mwenzetu huyo anaanguka chini.

Tulijaribu kumuinua lakini alikuwa hoi na alikuwa amepoteza fahamu.
Tukamlaza palepale chini.

“Mwenzetu ameshapotewa na fahamu, tutafanyaje?” nikamuuliza mwenzangu.
“Tumsubiri labda anaweza kuzinduka,” mwenzangu niliyebaki naye akaniambia.

“Hata akizinduka huyu hataweza tena kutembea.”
“Kwa hiyo ulitaka tumuache?”
“Tunajadiliana. Tutakachokubaliana ndicho tutakachokifanya.”
“Kwa vile umesema hata akizinduka hataweza kutembea, mimi naona tumuache.”

“Mimi pia naona hivyo. Kama tutafanikiwa kutoka tutatoa taarifa zake. Wanaohusika watamfuatilia yeye na yule msichana.”

Tulipokubaliana kuwa tumuache, tulimuacha tukaendelea na safari.
“Yule ana mahaba ya mchumba wake,” nikamwambia mwenzangu na kuongeza.

“Unajua mahaba yanaua.”
“Pamoja na hayo pia alikataa kula chakula. Mwili wake umekosa nguvu kabisa.”

“Mimi pia miguu inaniwaka moto lakini ninajikaza tu.”
“Wewe miguu, mimi kiuno. Kinauma kweli kweli.”
“Tujikaze. Pengine tumebakisha safari fupi, hatuwezi kujua.”
Tulitembea mwendo mrefu tukiwa bado tumo humohumo ndani ya pango. Ile sehemu iliyokuwa na njia mbili hatukuiona tena.

Ghafla tukajikuta tumetokea kwa yule mwenzetu aliyekuwa amezirai. Tulipomuacha alikuwa amelala kichalichali katikati ya njia. Lakini wakati ule tulipotokea tena mahali hapo tulimkuta amelala kifudifudi pembeni mwa njia.

“Tumetokea tena pale mahali?” nikamuuliza mwenzangu kwa mshangao.
“Naona tumetokea tena.”
“Humu ndani tunazungukaje!”
Mwenzangu alikuwa akimgeuza yule mwenzetu aliyekuwa amelala chini. Nikasikia akitoa sauti.
Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye gazeti hilihili Jumanne ijayo.

Leave A Reply