The House of Favourite Newspapers

Miaka Minne Ndani ya Mapango ya Amboni – 33

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Tukasimama.

 “Tusiendelee kwenda, tutakosa hewa kabisa,” nikawaambia wenzangu.

 “Mimi pia naona hivyo, tunaweza kufa.” Yule aliyekuwa akimkumbuka mchumba wake akasema.

 “Basi turudini nyuma,” nikawaambia.

SASA ENDELEA…

Tukageuka na kurudi nyuma.

“Huku tulikokuja hatukuwahi kufika,” nikasema.

“Hii ni njia nyingine, sio ile tuliyopita jana,” mwenzangu akabainisha.

“Ni kwamba tumepotea.”

“Ndiyo sababu haya mapango yamewekwa watu maalum wanaoyaelewa ili kuwaongoza watu.”

Tukaanza tena kutembea kurudi tulikotoka. Kule tulikoelekea kwanza kulikuwa kunatisha.

Nikakumbuka simulizi nilizowahi kuzisikia kuhusu mapango hayo kwamba yanasafiri hadi mbali sana.

Niliwahi kusikia kwamba kulikuwa na mbwa aliyeingia katika mapango hayo akatokea mjini Arusha baada ya kutembea mwendo wa siku kadhaa.

Nikajiambia huenda kule tulikokuwa tunaelekea ndiko alikopitia mbwa huyo.

Nilitaka kuwaeleza wenzangu kisa hicho lakini niliona hali tuliyokuwa nayo haikuwa ya kusimuliana hekaya, ilikuwa hali ya hatari kwani uhai wetu ulikwa ukiyeyuka kwa kasi kama barafu iliyowekwa juani.

Eneo lote lilikuwa kimya. Sauti zilizokuwa zikisikika zilikuwa za pumzi zetu tu.

Baada ya kutembea kwa mwendo mrefu tulichoka. Tulichoka sana hasa vile ambavyo tulikuwa tumekata tamaa ya kupona.

Tukaamua kukaa chini kupumzika.

“Jamani tuweke zile kumbukumbu za maelezo tuliyopeana,” nikawaambia wenzangu wakati tumeketi.

“Mimi nayakumbuka vizuri, sijui mwenzangu.” Mmoja wa wale wenzangu akasema huku akimtazama mwenzake.

“Mimi pia nayakumbuka,” jamaa huyo naye akasema.

“Sawa. Sasa tupumzikeni. Tukipata nguvu tutaendelea na safari,” nikawambia wenzangu.

Baada ya hapo hatukuzungumza tena, tukawa kimya. Kwa sababu ya uchovu niliokuwa nao nilipitiwa na usingizi nikalala fofofo.

Bila shaka wenzangu nao walilala kwani uchovu sikuwa nao peke yangu, sote tulikuwa tumechoka.

Baada ya saa kadhaa nilihisi kama vile macho yangu yalikuwa yamemulikwa na mwanga fulani wenye joto kali. Nikashituka na kufumbua macho.

Kweli macho yangu yakakutana na mwanga wa kimanjano ambao haukuwepo. Nikageuza macho yangu huku na huku. Nikaona mwenge ukiwa karibu yangu kabisa.

Huo mwenge ulinishitua zaidi nikainuka na kuketi ili niweze kuona vizuri. Nikamuona Faiza amesimama karibu yangu akiwa na mwenge huo.

“Faiza!” nikamuita.

“Ni mimi,” akaniambia na kuniuliza.

“Mmekuja kulala hapa?”

Wenzangu ambao pia walikuwa wamelala waliposikia sauti zetu waliamka, wakawa wanatusikiliza wakati naongea na Faiza.

“Faiza umetokea wapi?” Nikamuuliza Faiza.

“Nilikuwa napita pita huku na huko kuangalia kama bado mpo.” Faiza akanijibu.

“Umekuja mpaka huku?”

“Si mbali sana na pale nilipo mimi. Ni kama hatua hamsini tu.”

“Unasema kweli, mbona sisi tumetembea sana?”

“Huenda mlikuwa mnarudi tena bila kujua.”

Nikatazamana na wenzangu kwa mshangao.

“Inakuwaje kila mara tunajikuta tunarudi huku huku bila sisi wenyewe kujua?” Nikajiuliza kwa sauti ya kusikika kama vile nilikuwa nawauliza wale wenzangu.

“Humu ndani kuna njia zinazotatiza sana. Unaweza kudhani unakwenda kumbe unarudi,” Faiza akatuambia.

“Mh! Basi tutakufa sote humu humu. Tulikuja kwako mapema nikamshuhudia mwenzangu niliyefuatana  naye akiuawa na Kaikush.”

“Kumbe mlikuwa nyote. Mimi niliona mtu akiniita lakini wakati ule Kaikush alikuwa anakuja. Nikawahi kutoka na kumwambia aondoke haraka lakini hakuwahi hata kupiga hatua Kaikush akatokea.”

“Mimi niliona kila kitu. Nilimwambia yeye atangulie ili achunguze kama Kaikush yupo au hayupo. Nilipoona ameshikwa nikakimbia.

“Sasa mlifuata nini wakati niliwaacha sehemu nyingine ya mbali?”

“Tulifuata chakula na maji ya kunywa.”

“Kwa hiyo ulipokimbia ulikwenda wapi?”

Nilirudi kwa wenzangu nikawambia tuondoke, tukaondoka. Tulikwenda tukafika mahali hakuna hewa kabisa, tukageuka na kurudi. Ndiyo tukafika hapa.”

“Loh! Poleni sana jamani kwa mateso mnayoyapata. Nilishawaambia tangu mapema kwamba hali ya hapa si nzuri. Sasa nitawasaidiaje kuwapa chakula na maji mliyokuwa mnahitaji?”

“Tafadhali kama hatutakusumbua tunakuomba

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye gazeti hilihili Jumanne ijayo.

Leave A Reply