Miaka Minne Ndani ya Mapango ya Amboni-48

ILIPOISHIA

Baada ya kuwaelezea ndugu zangu masaibu yaliyonikuta huko Tanga, Faiza alionekana kioja kikubwa hasa kwa vile ambavyo nilimkuta katika lile pango akiwa amekaa kwa miaka minne.

Watu walitupa pole na kututakia maisha mema. Faiza ndiyo walimpongeza sana. Baada ya mazungumzo marefu na ndugu zangu, kaka yangu akaniambia alikuwa akiwasiliana na mke wangu karibu siku zote tangu nilipokuwa sijulikani niko wapi.

 Nikaomba simu kwa kaka nikaingia chumbani na kumpigia mke wangu. Nilizungumza na mke wangu kwa karibu robo saa. Nikamfahamisha kuwa nilikuwa niko katika maandalizi ya kurudi Uingereza.

Kama nilivyokuwa nimepanga, nilikaa Pemba kwa siku mbili. Siku ya tatu nikaondoka na wenzangu. Nilikuwa nimenunua simu mpya ambayo niliirudishia laini yenye namba yangu za zamani. Lakini wakati tumo kwenye boti tukirudi Dar nilimuona Faiza alikuwa amechukia.

SASA ENDELEA…

Nilijaribu kumuuliza Faiza alikuwa na tatizo gani lakini alitikisa kichwa na kuniambia hakuwa na tatizo.

Licha ya kuniambia hivyo niliendelea kuhisi kuwa alikuwa na tatizo ambalo hakutaka kulizungumza.

Tulipofika Dar, tulipanda basi kuelekea Bagamoyo. Mimi na Faiza tulikaa katika siti moja ya watu wawili. Dada yake alikaa katika siti nyingine.

Mara tu safari ilipoanza Faiza aliniuliza.

“Kumbe una mke?”

“Ninaye mke kwani sijawahi kukwambia?”

Faiza akabetua mabega yake.

“Hujaniambia kitu kama hicho.”

“Ninaye mke yuko Uingereza.”

“Ni Mzungu.”

“Ni Mpemba mwenzangu lakini anafanya kazi Uingereza.”

Baada ya hapo Faiza akanyamaza kimya.

Sasa niliweza kukisia kilichokuwa kimemfanya Faiza achukie tangu tulipoanza safari yetu kule Pemba.

Faiza alichukia baada ya kugundua kuwa nilikuwa na mke. Bila shaka alianza kuchukia pale nilipoomba simu kutoka kwa kaka yangu na kuzungumza na mke wangu kwa karibu robo saa. Sikuweza kujua kiini cha kuchukia kwake kilikuwa kitu gani.

“Unadhani nikiwa na mke itaathiri uhusiano wetu?” nikamuuliza baada ya kimya kifupi.

Faiza hakunijibu na uso wake ulizidi kuchukia.

“Kusema kweli nimegundua kuwa Faiza umepoteza furaha,” nikamwambia.

“Mbona niko kawaida,” akanijibu kwa kujikaza bila kunitazama.

“Hapana, Faiza niweke wazi tafadhali.”

Faiza akaamua kunyamaza.

Nikajaribu kumchokoa.

“Basi nikuchukue Uingereza uende ukaishi huko?”

“Utanichukuaje wakati una mke wako?”

“Kwani utajali kuwa nina mke wangu?”

“Nitajali sana.”

Hapo kila kitu nilikiona kwa uwazi. Faiza alitarajia kuwa niwe mume wake baada ya kunusurika naye kutoka mapangoni lakini aliona suala la mke wangu lilikuwa kikwazo na ndiyo sababu alichukia.

Faiza alipoona tupo kimya aliniambia.

“Inaelekea hukunipenda!”

Kauli yake ile ilinitia majonzi hasa nilipokumbuka tulivyokuwa mapangoni.

“Ngoja nikwambie ukweli, nimekupenda sana.”

“Lakini ndiyo hivyo tayari una mke wako.”

“Mke wangu si tatizo. Tunaweza kukubaliana kitu.”

Faiza akanitazama usoni kwangu haraka kama vile alitarajia ningemueleza jambo ambalo lilikuwa muhimu kwake.

“Kitu gani?” akaniuliza.

“Kule Uingereza nina mke na wewe utakuwa mke wangu wa huku kwetu.”

Nilipomwambia hivyo alionekana kufikiri.

“Kumbuka sisi ni Waislamu, kuna Suna ya Bwana Mtume,” nikamwambia.

“Suna ipi?” Faiza akaniuliza.

“Ya kuoa hadi wake wanne. Si unajua jiko moja haliinjiki chungu?”

Maneno yangu yalimfurahisha Faiza nikaona uso wake ukitabasamu.

“Mimi nilidhani nigekuwa peke yangu,” akaniambia.

“Sasa kuna mwenzako aliyewahi. Si unajua kila kitu kinakwenda kwa riziki?’

“Ni sawa,” Faiza akakubali kwa unyonge.

Baada ya kimya kifupi akaniuliza.

“Sasa huyo mke wako atakuruhusu?”

Nilielewa maana ya swali la Faiza. Alikusudia kuniuliza mke wangu ataniruhusu nioe mke mwingine.

“Sheria hainilazimishi nipate ruhusa yake. Tunaweza kuoana tu. Yeye atajua baadaye. Fikiria mimi nafanya jambo la suna. Suna na ruhusa ya mke kipi muhimu?”

“Suna ya Bwana Mtume ndiyo muhimu,” Faiza akanijibu kwa sauti  laini.

Jibu lake lilinifanya nitabasamu na yeye akatabasamu.

“Faiza ulisoma madrasa?”

“Nilisoma sana.”

“Sawa. Mimi nafikiri kinachohitajika hapa ni utayari wa mimi na wewe. Mimi niko tayari, nataka kukusikia wewe mwenzangu unasemaje?”

“Mimi pia niko tayari.”

“Naomba ulifikishe hilo kwa wazazi, tusikie na wao wana mawazo gani?”

Tulipofika Bagamoyo niligundua kuwa azma yangu ya kurudi Uingereza haraka inaweza kuzuiwa na makubaliano yangu na Faiza. Nilijua kuwa ingenigharimu lakini sikujali sana kwa sababu ya historia iliyotukutanisha mimi na Faiza ambayo tunzo yake adhimu.

Je, wazazi watakubali na mke wa kwanza atakubaliana na wazo hilo? Nini kitatokea? Ni maswali ambayo utapata majibu wiki ijayo, ngoja usome Jumanne ijayo.

Loading...

Toa comment