The House of Favourite Newspapers

Michael Fagan: Njemba aliyepenya kwa siri hadi chumbani kwa Malkia Elizabeth

0

Michael-FaganMichael Fagan

Hebu vuta picha, jamaa anaruka ukuta wa Ikulu, anaingia ndani na kupenya mpaka chumbani anakolala mheshimiwa rais, bila kushtukiwa na mtu yeyote wala kamera. Ghafla, mheshimiwa anashtuka usingizini na kukuta kuna mtu amekaa pembeni ya kitanda chake! Unaona kama haiwezekani si ndiyo? Basi tukio kama hilo limewahi kutokea nchini Uingereza.

queenMalkia Elizabeth II

Unajua ilikuwaje? Jamaa aitwaye Michael Fagan (68), aliruka ukuta mrefu wa Ikulu ya Buckingham, yalipo makazi ya Malkia Elizabeth II na kuingia mpaka chumbani kwa malkia. Ishu ilianza majira ya saa moja asubuhi, Julai 9, 1982 ambapo kwa ustadi mkubwa jamaa huyo alikwea kwenye fensi ndefu yenye urefu wa mita 4.3, na kupita kwenye seng’enge zilizokuwa juu kabisa ya uzio, akarukia upande wa ndani wa Ikulu.

Walinzi wakiwa hawana hili wala lile, jamaa alijipenyeza mpaka kwenye paa la jengo hilo upande wa nyuma, akapanda na kufanikiwa kuingia ndani kwa kupitia dirishani. Wakati hayo yakiendelea, walinzi walikuwa wakirandaranda nje ya Ikulu, wengine wakiwa na silaha nzito.

Baada ya kufanikiwa kuingia ndani, Michael alianza kurandaranda huku na kule, akishangaa mandhari nzuri ya jengo hilo, akaingia mpaka kwenye ofisi ya malkia na kukalia kwenye kiti cha enzi akipumzika. Akawa anaendelea kushangaa kila alichokiona. Mara akaona chupa ya mvinyo mweupe ambao hunywewa na malkia, akachukua glasi na kujimiminia, akawa anaendelea kuburudika.

Katika kupitapita, mara akatokezea chumbani kwa malkia, akanyata na kuingia, akawa anamtazama Malkia Elizabeth ambaye alikuwa amelala fofofo, akiwa hana hili wala lile. Jamaa akanogewa kumuangalia malkia akiwa amelala, na yeye akakaa pembeni ya kitanda na kutulia kimya.

Ghafla malkia akazinduka usingizini na kukuta kuna ‘namba ngeni’ chumbani kwake, akakurupuka na kutoka mbio kuwafuata walinzi ambao hawakuwa na taarifa kwamba kuna njemba iliingia hadi chumbani kwa malkia.

Muda mfupi baadaye, askari wengi na walinzi wa Ikulu, walimuweka jamaa huyo chini ya ulinzi na kumtoa nje msobemsobe huku kila mtu akishangaa jamaa aliwezaje kupenya mpaka ndani. Kwa bahati nzuri, sheria za kipindi hicho, hazikuwa zimeainisha kwamba kuingia Ikulu bila ruhusa ni kosa kisheria.

Jamaa akashtakiwa kwa kosa moja tu la kuiba mvinyo mweupe wa malkia na kunywa, shtaka ambalo baadaye lilitupiliwa mbali. Mahakama ikaamuru jamaa akachunguzwe akili zake kama alikuwa timamu, akapelekwa hospitali lakini baadaye aliachiwa huru.

Huku nyuma, msala ulibakia kwa walinzi wa Ikulu, maafisa kadhaa wakafukuzwa kazi kwa uzembe kwani kama Fagan angetaka kumdhuru malkia ni dhahiri hakukuwa na kipingamizi.

Leave A Reply