The House of Favourite Newspapers

Michelle Obama Aalivyokataa Kushindwa Mpaka Mafanikio

Michelle Obama,

BAADA ya kuwatazama wanawake wa chuma na kina dada wa chuma wa hapa nyumbani katika matoleo kadhaa, leo turuke hadi ng’ambo mpaka nchini Marekani kwa mwanamke wa chuma, Michelle Obama, ambaye bila shaka anafahamika kwa wengi kutokana na kuwa mke wa rais wa kwanza mweusi Marekani, Barack Obama.

Michelle, jina lake halisi la kuzaliwa ni Michelle LaVaughn Robinson. Amekulia kwenye familia ya maisha ya kati huko kusini mwa Chicago, kwani baba yake Fraser Robinson III, alikuwa ni mfanyakazi wa kumwagilia miti maji aliyeajiriwa na serikali ya jiji hilo.

Mama yake, Marian Shields Robinson, alikuwa ni sekretari katika kampuni iitwayo Spiegel’s Catalog, lakini baadaye mama huyo alikuwa mama wa nyumbani.

 

MICHELLE AMEPITIA MAISHA MAGUMU!

Wengi wanaweza kumtazama mwanamke huyu wa chuma tofauti. Kwamba, kwa kuandika historia ya kuwa mwanamke mweusi wa kwanza kukaa kwenye ‘White House’ ya Marekani na kuwabadilisha wanawake wengi duniani kutokana na ‘speech’ zake, pengine hajaonja joto la jiwe la msoto kwenye maisha.

Hakika haipo hivyo. Kama wengi waliyofanikiwa kupitia kwenye msoto, Michelle pia amepita maisha magumu. Wakati anakua nyumbani kwao walikuwa wakitumia chumba kimoja pamoja na choo kimoja na wazazi wake pamoja na kaka zake.

 

Aliwahi kueleza kwenye mahojiano na chombo kimoja cha habari, Marekani akizungumzia maisha yake ya nyuma kwamba, hakukulia kwenye familia ya kwenda wikiendi kwenye majumba ya sinema wala kununua ‘ice-cream’. Lakini maisha yalibadilika zaidi kwenye familia yake na kuwa magumu mwaka 1991, baada ya baba yake kufariki dunia. Wakati huo yeye alikuwa na miaka 27.

Lakini Michelle, alieleza kwamba aliamini ana jukumu la kuitoa familia yake kwenye dimbwi hilo la umasikini na kufikia maisha mazuri na yenye furaha ikiwezekana hata kuandika historia. Akazidi kukomaa na masomo yake ya sheria.

ALIPIGANIA  NDOTO ZAKE

Katika maisha yake Michelle, ameweka wazi mara kwa mara kwamba alikataa kushindwa na alikuwa ni mtu wa kupigania ndoto zake. Ndoto zake kubwa kwenye maisha zilikuwa ni kuwa mwanasheria maarufu na mwenye msaada kwa watu pamoja na kuwa mwandishi wa vitabu.

Ndoto zote aliweza kuzikamilisha kwa kufanikiwa kuwa mwanasheria baada ya kuhitimu digrii ya sheria katika Chuo cha Harvard, Law School. Baada ya hapo akaanza kutetea haki za wanawake, usawa, pamoja na matumizi mazuri ya silaha. Mbali na kuwa mwanasheria, Michelle aliweza kufanikiwa pia kwenye ndoto yake ya kuandika vitabu kwa kuandika vitabu viwili ambavyo ni American Grown pamoja na Becoming.

ANASEMAJE KUHUSU MAFANIKIO?

Michelle, kuhusu mafanikio mara kwa mara amekuwa akisisitiza watu kuzidi kupambana katika ndoto zao na kutokata tamaa. Katika mazungumzo yake mengi na wanafunzi katika vyuo mbalimbali kwamba mtu yeyote anayetaka kufanikiwa kwenye maisha hatakiwi kuogopa kufeli.

Hatakiwi kurudi nyuma lakini zaidi afanye kazi kwa bidii. Huyo ndiye mwanamke wetu wa chuma wiki hii, Michelle Obama, ambaye pia ni mama wa watoto wawili, Sasha na Maria.

Makala: Boniphace Ngumije na mtandao

Comments are closed.