The House of Favourite Newspapers

Michirizi Ya Damu – 13

0

Walichanganyikiwa, hawakuamini kile walichokuwa wamekikuta. Wakaanza kumtafuta kila kona ndani ya hospitali hiyo lakini mtu huyo hakuonekana. Hawakujua ni kitu gani walitakiwa kufanya, hawakujua mahali alipokuwa ameelekea, hawakujua ni jinsi gani wangemwambia bosi wao, Belleck ambaye alikuwa akisubiri taarifa ya kifo cha Fareed kwa hamu kubwa.

“Yupo wapi?” aliuliza Dk. Watson.

“Hatujui! Ila tulimuacha humu ndani!”

“Sasa yupo wapi?”
“Hatujui!”

Walimfikiria Belleck, alikuwa mwanaume makini aliyetaka kuona kila kitu alichoagiza kikifanyika kwa haraka sana. Alitaka mtu huyo afe lakini la zaidi aliyataka madawa yake ya kulevya ambayo yalikuwa na thamani kubwa mno.

Hawakujua angefanya nini kama wangempa taarifa kuwa mwanaume huyo alimimbia, aliwatoroka wakati nesi alipopiga kelele kwa kuhisi kwamba walikuwa watu wabaya.

Hawakutaka kuona wakishindwa, waliamini kwamba kama wangemtafuta mtu huyo angepatikana hivyo kuingia mitaani na kuanza kumtafuta. Walitumia saa nne lakini hawakufanikiwa kumpata na muda wote huo Belleck alikuwa akiwasumbua kwenye simu kwa kutaka kujua kile kilichokuwa kikiendelea.

Walianza kwa kumficha lakini mwisho wa siku walipoona muda umekwenda sana na hawakumpata, wakaamua kumwambia ukweli kwamba Fareed aliwatoroka hospitali.

“Alitoroka?”
“Ndiyo!”
“Aliwatorokaje?”

Wakaanza kumwambia namna mtu huyo alivyowatoroka, alitaka kuwalaumu lakini baada ya kuambiwa mazingira yote jinsi alivyotoroka, akaridhika na kuona kwamba hata kama angekuwa yeye ilikuwa ni lazima kutorokwa kama ilivyokuwa kwa wenzake.

“Ila hakikisheni mnamtafuta hapo. Najua atakuwa hapohapo Marseille,” alisema Belleck huku akiwa na uhakika kwamba mtu huyo hakuwa ametoka hapo Marseille.

“Haina shida mkuu!”

****

Fareed alikuwa ndani ya chumba cha hoteli, moyo wake ulikuwa kwenye majonzi tele, siku hiyo hakujisikia vizuri kabisa. Aliyakumbuka maisha yake aliyokuwa amepitia, jinsi alivyokumbwa na pepo la ngono ambalo lilimfanya kushiriki mapenzi ya jinsi moja.

Moyo wake ulimuuma mno, ulichoma kiasi kwamba hadi machozi ya uchungu yakaanza kutiririka mashavuni mwake. Alijijua kwamba yeye alikuwa mkosaji, alijua kwamba Mungu alimuumba mwanaume kwa kuwa alikuwa na makusudi naye, hapo akagundua kwamba Mungu hakufanya makosa kumuumba mwanaume bali alikuwa na makusudi mengi.

Alijuta, siku hiyo alijikuta akianza kuyafikiria maisha yake, njia zake mbaya alizopitia, alilia kama mtoto chumbani mule. Nafsi yake ilimuhukumu, ilimwambia kwamba alichokuwa amekifanya kwa miaka yote halikuwa kusudio la Mungu bali la shetani ambaye aliamua kumtumikisha kupitia mwili wake.

Alitaka kubadilika, hakutaka kuendelea kumtumikia shetani, alitaka kubadilika na kuwa mtu mwingine kabisa. Tangu azaliwe, hakuwahi kwenda msikitini wala kanisani, hakujua yeye alikuwa dini gani, alijichagulia maisha yake kuishi hivyo hata alipotaka kuyabadilisha maisha yake.

Kwa kuogopa maneno mengi ya watu akaamua kuchagua kwenda kanisani, lakini isiwe nchini Tanzania, aliijua mitandao ya kijamii, magazeti ya kidaku ambayo kwa namna moja au nyingine yangemwandika, hivyo kama aliamua kwenda kanisani, basi iwe nchi za hukohuko.

Akalifikiria kanisa kubwa la St. Peter lililokuwa jijini New York nchini Marekani. Lilikuwa miongoni mwa makanisa makubwa ambalo liliwahi kutembelewa na Papa José Kentenich miaka ya 1880.

Padri aliyekuwa akilichunga kanisa hilo aliitwa Mathew Luke. Alikuwa miongoni mwa mapadri waliojulikana nchini Marekani ambapo watu wengi na kumuheshimu huku wengine wakiombea padri huyo achukue nafasi ya upapa siku moja.

Alikuwa mwanaume mpole, aliongea taratibu huku akipenda sana kuonyesha tabasamu pana usoni mwake. Watu wengi walimpenda, uzuri wake wa sura ukawafanya watu wengi kwenda kuabudu katika kanisa hilo.

Mbali na uzuri wa sura aliyokuwa nayo, kitendo cha Papa José Kentenich miaka ya 1880 kuwahi kutembelea huko kikalifanya kanisa hilo kuwa maarufu na wengi kwenda huko kuabudu.

Fareed hakutaka kusikia jambo lolote lile, hakutaka kuzuiwa na mtu yeyote kuelekea huko, alidhamiria kwa moyo wake kwamba ilikuwa ni lazima aende akaungame dhambi zake, Mungu amsamehe kwa yote aliyoyatenda katika maisha yake.

Alipoamaliza kuyafikiria sana maisha yake akaondoka na kwenda chooni, huko, akajisaidia kete za madawa ya kulevya aliyokuwa amewekewa tumboni na kukiflashi choo kwa maana kwamba hakutaka kuyachukua kwa kuwa alitaka maisha yake yawe upya tena, yawe safi na amuabudu Mungu kwa hali na mali.

Siku iliyofuata akaanza safari ya kuelekea nchini Marekani. Hakutaka kuondoka kwa ndege jijini Marseille, alichokifanya ni kupanda basi ambalo lilimpeleka mpaka Monaco ambapo huko ndipo alipopanda ndege na kuelekea huko.

Ndani ya ndege, mawazo yake yalikuwa katika maisha yake tu, bado aliendelea kuumia kupita kawaida, hakuacha kulia, moyo wake uliendelea kuwa kwenye majuto kiasi kwamba kuna wakati alijiona kuwa na dhambi nyingi kuliko hata shetani mpaka kuhisi kwamba hata kama angefanya kitu gani Mungu asingeweza kumsamehe.

“Mungu naomba unisamehe!” alisema Fareed wakati ndege ikikata mawingu kuelekea Uingereza kabla ya kuunganisha na kuelekea nchini Marekani.

****

Fareed alifika nchini Marekani majira ya saa 10:30 jioni. Hali yake hewa ilikuwa ni baridi kali, katika sehemu kubwa ya Jiji la New York kulikuwa na theluji kitu kilichomfanya kuwa kwenye wakati mbaya mno.

Akaondoka uwanjani hapo kwa kuchukua teksi ambayo ilimpeleka mpaka katika Hoteli ya Queen Cleopatra ambayo haikuwa mbali sana kutoka katika uwanja huo. Alipofika, akakifuata kitanda na kutulia.

Bado kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, akili yake ilichanganyikiwa kupita kawaida. Maisha aliyokuwa amepitia yalikuwa machafu yaliyomfanya kulia sana.

Hakutaka kumwambia mtu yeyote kwamba aliamua kuyabadilisha maisha yake, hata Asteria alipokuwa akimtumia meseji kwa njia ya WhatsApp au hata kumpigia hukohuko hakuwa akipokea simu kwani alihitaji muda wa kuwa peke yake, Mungu ayasafishe maisha yake na kuishi maisha matakatifu.

“Nilisikia kwamba Yesu alikufa kwa ajili yetu wanadamu! Alisulubiwa ili tupate ukombozi, kwa kupigwa kwake, sisi tumepona. Mungu naomba unisaidie, uusafishe moyo wangu kwa damu ya Yesu,” alisema Fareed huku akiwa kitandani, hakuishia hapo, akatoka kitandani hapo, akapiga magoti na kuanza kusali kwa maneno aliyoyafahamu yeye kwani hakuwahi kuingia kanisani hata mara moja.

Sala yake ilichukua dakika tano, alikuwa akilia kwa uchungu mkubwa, aliuona upendo wa Mungu mpaka kumtoa mwanaye wa pekee kuja duniani kwa ajili ya maisha ya wanadamu lakini mwisho wa siku wanadamu hawakutaka kuyabadilisha maisha yao akiwemo yeye.

Alisikia hukumu kubwa moyoni mwake, alikuwa akilia na wakati mwingine alikipiga kifua chake kwa maumivu makali mno kwani hakuamini kama alikuwa amefanya uovu mkubwa kiasi hicho.

“Mungu! Naomba unisamehe! Mungu, mimi ni mwanadamu, nimekutenda dhambi, moyo wangu unalia, unahuzunika na kuumia, sikustahili kukutendea hay. Mungu! Nisamehe, usafishe moyo wangu,” alisema Fareed huku akiendelea kulia kama kawaida.

Siku hiyo ilikuwa ni siku ya kutubu dhambi zake, ulipofika usiku akalala huku akisubiri asubuhi ya kesho aende katika Kanisa la St. Peter ili kuungama dhambi zake kwa padri aweze kusamehewa.

Akalala, alipoamka hakutaka kuendelea kubaki hotelini, akachukua mkoba wake na kuelekea katika kanisa hilo ambalo nalo wala halikuwa mbali kutoka mahali pale alipokuwa.

Alipofika, hakukuwa na watu wengi kanisani, kulikuwa na watu watatu tu ambao walikaa kitofautitofauti wakisali na kusoma Biblia. Akaa kwenye kiti na kisha kupiga ishara ya msalaba na kupiga magoti.

Hapo kanisani, akaanza kulia tena, bado moyo wake ulichoma mno, maovu mengi aliyokuwa ameyafanya kipindi cha nyuma yalikuwa yakijirudia kichwani mwake kama mkanda wa video kitu kilichomuumiza kupita kawaida.

Alipomaliza, akatoka na kwenda kule kulipokuwa na chumba cha kuungamia dhambi zake ambapo akakuta kiti kikiwa karibu na kidirisha kidogo kilichokuwa na wavu ambapo ndani ya chumba kile kulikuwa na padri aliyekuwa na kazi ya kusikiliza dhambi za watu waliokuja kuungama.

Fareed akakaa kwenye kiti kile huku akilia. Akaanza kumsubiri padri Luke ambaye akafika mahali hapo baada ya dakika mbili kupita.

“Karibu sana mtoto wa Mungu!” alisema padri Luke.

“Nashukuru padri!”

“Niambie, unataka kumwambia nini BWANA?”

“Nimefanya dhambi nyingi. Nimekuja kuungama,” alisema Fareed huku akiendelea kulia.

“Zipi hizo?”

Hapo ndipo alipoanza kumuhadithia Padri Luke dhambi zake alizokuwa amezifanya. Alikuwa akilia kwa uchungu. Hakutakiw akuficha kitu chochote kile, alimwambia kila kitu kilichotokea katika maisha yake, jinsi alivyoanza kufanya mchezo wake wa ushoga mpaka pale alipofikia, alimwambia jinsi alivyolala na wanaume na kuwachezea alivyotaka.

Padri Luke alikuwa kimya akimsikiliza, Fareed aliungama dhambi zake na mwisho wa siku padri kumwambia kwamba Mungu alimsamehe dhambi zake zote na siku inayofuata alitakiwa kurudi kanisani hapo kwa ajili ya kupakwa mafuta ya baraka kwani alikuwa akiingia katika maisha mapya ya kumuabudu Mungu.

Fareed akaondoka mahali hapo huku moyoni mwake akiwa na amani kubwa. Majuto yote yakatoka moyoni mwake, alijiona kuwa mtu mpya, tamaa za kuwataka wanaume zilipotea ghafla kiasi kwamba yeye mwenyewe alishangaa. Alilala hotelini huku akisubiri siku ya kesho ambayo ilikuwa ni lazima aelekee huko kwa ajili ya kupakwa mafuta ya baraka kama alivyoambiwa.

Kesho yake ilipofika, akaondoka hotelini na kwenda kanisani humo. Padri akamwambia amfuate katika chumba kile cha kuungamia dhambi alipokuwa akikaa ambapo ndipo kulipokuwa na mafuta hayo.

Fareed hakutaka kujali, akatoka katika kiti kile alichokalia jana na kwenda katika chumba kile. Hakikuwa na mwanga mkali, kulikuwa na mwanga hafifu, mbele yake alimuona padri akiwa amesimama huku akimsubiri, alipomkaribia akaambiwa apige magoti na kufumba macho.

Alipofanya hivyo, padri akamsogelea na kuanza kumshika shingoni. Ushikaji wake haukuwa wa kawaida hata kidogo, ulikuwa ni ushikaji wa kimahaba ambayo uliyawehua pepo la ngono alilokuwa nalo Fareed, hapohapo akaanza kusisimka.

Padri hakuacha, aliendelea kumshika shingoni tena kwa ustadi mkubwa. Fareed aliendelea kusisimka, hisia alizokuwa akizisikia zilikuwa ni za ajabu sana, mwili ukaanza kumlegea, padri hakuacha, ndiyo kwanza akaendelea kushuka chini na kuanza kumvua mkanda wa suruali.

“Padriiiiiiiiiiii…” aliita Fareed huku akiwa hoi.

“Bebi! Unanukia vizuriiiii…” alisema padri huku akionekana kuchanganyikiwa kwani hata pumzi zake hazikuwa za kawaida.

Ndani ya dakika kadhaa tu, Fareed akajishtukia akiwa mtupu, alitaharuki, akaanza kumtoa padri lakini hakutoka kabisa, alipotaka kupiga kelele, alizibwa mdomo kwa kiganja cha padri huyo.

Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kubakwa, moyo ulimuuma sana, hakutegemewa kubakwa na padri huyo ambaye kwake alionekana kuwa mtumishi wa Mungu mpaka kufika kwake na kuanza kuungama.

Padri Luke alichukua dakika ishirini kumbaka na alipomaliza, akamchukua na kumpitisha mlango wa nyuma huku Fareed akiwa hoi, hata kusogeza viungo vyake alishindwa.

Kupitia mlango wa nyuma, kulikuwa na gari lake, akampakiza na kuondoka naye. Safari ilikuwa ndefu na walipofika sehemu iliyoonekana kuwa na takataka nyingi, akasimamisha gari lake na kumwangalia Fareed aliyekuwa hoi japokuwa nguvu zilianza kumjia.

“Nisamehe tu! Shetani aliniingia. Amekuwa akinitesa sana katika mchezo huu, uliponiambia shida yako, nilizidiwa kabisa, naomba unisamehe,” alisema Padri Luke huku akimwangalia Fareed aliyekuwa akilia tu.

“Nitakuua! Nitakuua padri!” alisema Fareed, akaufungua mlango na kuteremka, hakupiga hatua nyingi, akadondoka na kupoteza fahamu. Padri Luke akaliwasha gari lake na kuondoka mahali hapo huku akimwacha Fareed akiwa hoi.

***

Bado bilionea Keith alikuwa kwenye penzi la dhati na msichana Maria, moyo wake ulichanganyikiwa, ulikufa na kuoza, hakutaka kusikia kitu chochote, kwake, msichana huyo alikuwa kila kitu.

Alitumia kiasi kikubwa cha pesa kwa msichana huyo, hakutaka kabisa kumuona akipata tabu ya aina yoyote ile. Alimpenda, alimpeleka nchini Ufaransa, Italia, Dubai na sehemu nyingine nyingi kwa ajili ya kula naye maisha.

Msichana huyo hakutaka kuleta uvivu kitandani, alifanya kila linalowezekana kumchanganya mzee huyo, alijua kucheza na kiuno chake, alijua kucheza na mdomo wake uliomchanganya mzee huyo na kuona dunia yote ilikuwa yake.

Maria hakurudi nchini Nigeria, aliendelea kubaki nchini MArekani huku akiendelea kutanua na mwanaume huyo. Penzi likamchanganya mno Keith, wakati mwingine hakuwa akifanya kazi zake, alitamani sana kuendelea kuwa na mwanamke huyo kwani kila alipomuacha hata kwa saa tano, alihisi kulikuwa na mwanaume aliyekuwa akiliiba penzi lake.

“Have you ever seen collossium?” (Umewahi kuliona Collessium?) aliuliza Keith.

“I’ve just seen it but I’ve not touched it!” (nimewahi kuliona lakini sijawahi kuligusa) alijibu msichana huyo.

“Are you serious baby?” (kweli bebi?)

“Yeah!” (ndiyo)

“I want to take you there!” (nataka nikupeleke huko)

“I real want to touch it,” (natamani sana niliguse) alisema msichana huyo.

Collossium lilikuwa jengo kubwa la kizamani lililokuwa Roma nchini Italia. Jengo hilo ni miongoni mwa majengo makubwa ya zamani ambayo Waroma walikuwa wakiyatumia kwa ajili ya michezo na kuwaua mateka wao kwa kuwataka kupambana na simba.

Lilikuwa jengo la kutisha, lililomwaga damu za watu wengi miaka ya nyuma kipindi cha mtawala Julius Caesar. Kila mtuu katika kipindi hicho alitamani kuliona jengo hilo lililokuwa na historia kubwa na ya kutisha.

Kwa mtu kama Keith, kwa kuwa alimpenda sana Maria akaona kwamba kumpeleka katika jengo hilo na kuliona jinsi lilivyokuwa ingemfanya msichana huyo kufurahia. Hakutaka waendelee kukaa nchini Marekani, siku mbili mbele wakapanda ndege na kuelekea nchini Italia.

Walichukua saa kumi na tano kufika huko ambapo wakachukua chumba katika Hoteli ya Pretorita. Usiku ulikuwa ni wa mahaba tele, walishikana hapa na pale, walifanya michezo yote ambayo wapenzi walitakiwa kufanya wawapo faragha.

Kwa Maria, alifanya kama siku nyingine, alimuongezea mautundu kwa ajili ya kumpagawisha mzee huyo aliyekuwa tayari kufanya kitu chochote lakini si kumuacha msichana huyo mrembo. Alimchanganya mno kitandani, moyo wa Keith ukazidi kumpenda Maria kiasi kwamba akawa hajiwezi kwa msichana huyo.

Siku iliyofuata wakaelekea katika jengo hilo. Maria hakuamini, alizoea kusoma historia ya jengo hilo kubwa lakini siku hiyo alikuwa akiliona kwa macho yake na kuligusa. Walikaa huko kwa dakika arobaini na tano ndipo wakaondoka kurudi hotelini ambapo kama kawaida mchezo wao ukaanza upya.

Walichoka, walipomaliza, wakaondoka na kwenda chini kabisa kulipokuwa na mgahawa, wakaagiza chakula na kuanza kula. Wakiwa huko, macho ya Keith yakatua kwa mtu ambaye alimfahamu kabisa, alikuwa bilionea mwenzake kutoka nchini Hispania, Jose Mendoza.

Wakasalimiana, kama alivyokuwa yeye, hata huyo Mendoza naye alikuwa hivyohivyo, mtu wa wanawake wadogo ambapo alitumia kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya kuuridhisha moyo wake.

“Nakuona umekaa na mtoto mkali,” alisema Mendoza huku akimwangalia Keith.

“Mimi ni kama wewe. Leo umechukua mtoto wa Kifaransa?” aliuliza Keith.

“Hapana! Ni Venezuela!”
“Aisee ni mzuri sana.”

Walikuwa wamseogea pembeni wakizungumza tu, waliwaacha wasichana wao katika meza nyingine kabisa. Maria alibaki akiangalia na demu wa Mendoza, hakumfahamu lakini kwa kuwa bwana wake alikuwa rafiki wa Keith, wakaanza kuzungumza kwa lengo la kuzoeana.

Wakati wakiwa hapo, ghafla akatokea mwanaume mmoja, aliyevalia suti, nywele alizipaka dawa, alionekana kuwa mwanaume mkakamavu, akawasogelewa wasichana wale na kisha kuwasalimia.

“Mna kampani?” aliuliza mwanaume huyo.

“Ndiyo! Tukusaidie nini?”
“Naomba unitafute,” alisema mwanaume huyo huku akimpa Maria kikaratasi kilichokuwa na namba yake ya simu.

“Mmh!”
“Usiogope! Mimi si muuaji! Naomba unitafute! Usihisi kwamba nakutaka, hapana, ila ninataka kuzungumza nawe mambo fulani kwa faida yako,” alisema mwanaume huyo.

“Mambo gani?”
“Ndiyo maana nimekupa namba yangu unitafute!” alisema mwanaume huyo, alikuwa akizungumza harakaharaka ili asionekane na wanaume wale wakajua kwamba alikuwa akiwamendea mademuu zao.

“Sawa.”

Hakuendelea kubaki mahali hapo, alichokifanya mwanaume huyo akaondoka zake mahali hapo. Wasichana hao walibaki wakimwangalia, alikuwa mzuri wa sura, alivalia suti iliyomkaa sana mwilini, mwili wake ulionekana kujazia, hakuwa na kitambi kama walivyokuwa mabwana zao.

Wote walimwangalia alivyokuwa akiondoka, alitembea kijeshi, akatoka ndani ya mgahawa huo na kutokomea zake. Japokuwa kikaratasi kile alipewa Maria lakini hata demu wa Mendoza naye alitamani kuwa na namba za mwanaume huyo.

Alikuwa na sura nzuri, alimpenda, hakutaka kuona akiacha mwanaume huyo aondoke zake kwani kwa jinsi alivyokuwa akivutia, hata moyo wake ulimchanganya.

“Ni mzuri!” alisema demu wake Mendoza.

“Sisi wengine tumezaliwa na bahati tu,” alisema Maria na kisha kukiweka kikaratasi kile mkobani.

Kichwa cha Maria kikachanganyikiwa, uzuri aliokuwa nao mwanaume yule ukampagawisha, moyoo wake ukahisi akianza kuanguka katika penzi la mwanaume yule, hata alipoondoka bado aliendelea kuhisi kitu cha tofauti moyoni mwake.

Akili yake ikahama, akaacha kumtafakari Keith, akaanza kuweka hisia zake kwa mwanaume ambaye hakuwa akimfahamu, hakujua alitokea wapi lakini kwa jinsi alivyoonekana, aligundua kwamba alikuwa mwanaume aliyekuwa na uwezo mkubwa kitandani.

Alikuwa akitafuta nafasi ya kuwasiliana na mwanaume huyo, alitaka kutumia hata usiku mmoja kulala naye kitandani na kufanya naye mapenzi, ilikuwa ni mara ya kwanza kumuona lakini hakutaka kuona akimkosa, alikuwa tayari kufanya kitu chochote kile lakini mwisho wa siku kuwa naye.

“Usiku huuhuu lazima niongee naye,” alijisemea.

Huo ndiyo ulikuwa uamuzi wake, hakutaka siku hiyo ipite pasipo kuwasiliana naye, alichokifanya usiku huo ni kuamka usiku wa manane, akatoka kitandani huku akinyata na kuelekea chooni kwa lengo la kuzungumza na mwanaume huyo kwani pasipo kufanya hivyo asingefanikiwa kutokana na Kaith kumng’ang’ania kama ruba.

“Naomba upokee simu,” alisema wakati simu ikianza kuita, baada ya sekundee kadhaa tu, simu ikapokelewa.

“Bila shaka ni mrembo wa mgahawani,” alisema mwanaume huyo baada ya kupokea simu, alionekana kabisa kuwa macho japokuwa usiku ulikuwa umekwenda sana.

“Ndiyo! U mzima bebi,” alisema Maria, hakutaka kujivunga, alikuwa tayari mwanaume huyo ajue kwamba alikuwa akimpenda.

“Nipo poa.”
“Upo wapi nije tuzungumze kama ulivyotaka?” aliuliza Maria.

“Nipo hotelini! Ila nipo na mke wangu!”

“Jamani! Kumbe umeoa?”
“Yeah! Lakini nahisi hili haliwezi kuninyima kuwa na wewe,” alisema mwanaume huyo.

“Kweli kabisa. Umetokea kunichanganya sana mpenzi. Naomba nionane na wewe hata kesho!” alisema Maria.

“Haina shida. Wewe tu! Bye!”

“Bye! Nakupenda.”
“Nakupenda pia!”

****

Fareed aliumia moyoni mwake, hakujua sababu iliyomfanya Mungu kumpitisha katika maisha aliyokuwa akipitia kipindi hicho. Alidhamiria kubadilisha maisha yake, alidhamiria kumuabudu Mungu katika roho na kweli lakini pale alipokubaliana na moyo wake kwamba alitakiwa kubadilika, tayari tatizo likawa limetokea.

Alilia, alihuzunika, moyo wake ulichoma mno. Alimwamini Padri Luke kwa kuona kwamba angemuombea msamaha kwa Mungu ili maisha yake mapya yaanze rasmi lakini kitu cha ajabu kabisa, mwanaume huyo akaamua kumbaka.

Hakutaka kuendelea kubaki pale alipotupwa, akaondoka na kurudi hotelini, huko akakaa na kulia sana, akahuzunika mno na mwisho wa siku kupanga kurudi nchini Tanzania, alitaka kuanza upya kabisa, kama mtu aliyezaliwa kwa mara ya pili.

Alirudi nchini kimya kimya, hakutaka kumtaarifu Asteria kama alikuwa amerudi, alifanya hivyo kwa sababu alitaka kuyabadilisha maisha yake, aiondoe tamaa iliyokuwa mwilini mwake, asimtamani tena mwanaume ashinde vishawishi vyote na kuwa mtu mpya.

Akamtafuta daktari aliyekuwa akiwahudumia sana wanaume tata, huyo aliitwa Emmanuel Kihampa, daktari maarufu aliyekuwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Alipofika huko, akamfuata katika ofisi yake na kuanza kuzungumza naye.

Hakutakiwa kumficha kitu chochote kile, alitakiwa kumwambia kila kitu kilichokuwa kikiendelea mwilini mwake, alimwambia tabia yake hiyo ambayo ilianza tangu utotoni, alimwambia juu ya tamaa kali aliyokuwa nayo.

Daktari huyo akampa vidonge vya kumeza lakini pia alitakiwa kuchomwa sindano nyumba kwa ajili ya kuua vijidudu ambavyo vilikuwa vikimuingiza katika matamanio makubwa. Hilo halikuwa tatizo, alidhamiria kubadilika, alidhamiria kuyabadilisha maisha yake, hivyo akachomwa sindano hiyo.

Haikutosha, akaambiwa kwamba ilikuwa ni lazima auweke mwili wake kimazoezi, alitakiwa kufanya mazoezi ya kila aina kuhakikisha anakuwa sawa. Akaanza kukimbia mitaani, akawa anajiunga na vijana wengine kufanya mazoezi huku ikifika usiku, alitumia muda wake mwingi kusoma vitabu, yote hiyo ilikuwa ni harakati za kuachana na tabia chafu alizokuwa nazo kwamba asingeweza kufikiria ngono kama kipindi cha nyuma.

Ilikuwa kazi kubwa, alipambana nayo, ilimtesa, ilimnyima raha kwani wakati mwingine alikuwa akishtuka kutoka usingizini, mwili ulikuwa ukimsumbua na kutandani, alikuwa na matamanio makubwa ya kuwa na mwanaume kipindi hicho, alivyokuwa akiiona hali hiyo, haraka sana alichukua mazoezi humohumo, kuruka kamba na kupiga pushapu kisa kulala.

Hayo yalikuwa ni maisha yake, hakuacha kwenda hospitalini, kila alipokwenda, alichomwa sindano nyumba kwa ajili ya kuua vijidudu vilivyokuwa vikimpa hamu ya kufanya mapenzi na mwanaume, ilimsaidia japokuwa ilionekana kuwa vigumu kumalizana na matatizo aliyokuwa nayo.

Kila siku alikuwa akienda katika sehemu ya mazoezi, gym kwa ajili ya kuchukua mazoezi mbalimbali hata kunyanyua vyuma. Alikuwa na muonekano wa kike, alikuwa na sauti iliyofanana na mwanamke lakini baada ya kuanza kufanya mazoezi, kunyanyua sana vyuma hatimaye mwili wake ukaanza kubadilika.

Akaanza kujazia, kifua chake kikaanza kuwa kipana, muonekano wa kike ukapotea, akaanza kuwa na six packs tumboni, mabadiliko hayo yote yalitokea ndani ya miezi sita, akaonekana kuwa mwanaume kamili, aliyeendelea kupata tiba kila siku na kufanya mazoezi ya nguvu.

Hakuwasahau watu waliomtenda, aliwachukia mno na hakutaka kabisa kuona watu hao wakiendelea kuishi. Alimkumbuka Keith, mwanaume mwenye roho mbaya ambaye alidhamiria kumuua baharini lakini kwa bahati nzuri sana akanusurika baada ya kuokolewa na mvuvi mmoja.

Hakuishia hapo, alimkumbuka bilionea Belleck ambaye alijifanya kumpenda, alimtumia alivyotaka na mwisho wa siku kutaka kumuua kwa kumtoa madawa ya kulevya yaliyokuwa tumboni, tena pasipo kujali kama alimsaidia kusafirisha madawa hayo au la.

Na mtu wa mwisho kabisa aliyemkumbuka alikuwa Padri Luke Mathew ambaye alimfuata kwa ajili ya kutubu dhambi zake lakini mwisho wa siku mwanaume huyo akambaka. Alikumbuka kila kitu, hakutaka kuona watu hao wakiendelea kuishi kwa raha na wakati walishirikiana kumuumiza moyoni mwake, walishirikiana hata kuuumiza moyo wake.

Mtu wa kwanza kabisa aliyetaka kumuua alikuwa Bilionea Keith. Hakutaka kumuona mwanaume huyo akiendelea kuvuta pumzi ya dunia hii na wakati alimtenda vibaya. Mara ya mwisho kumsikia mwanaume huyo ni kwamba alikuwa na msichana mrembo mwenye asili ya Kinaigeria aliyeitwa Maria.

Alitaka kujua mahali alipokuwa, hakuendelea kuishi nchini Tanzania, akasafiri mpaka nchini Marekani, kwa kuwa bilionea huyo alikuwa akifahamika sana, hakupata kazi kuzipata data zake tena kutoka kwa watu walioonekana kuwa wa karibu sana.

Akaambiwa kwamba mwanaume huyo alikuwa akijiandaa na safari ya kuelekea nchini Italia kwa ajili ya kula bata na mpenzi wake na kuliona jengo kubwa la Collosseum. HAkutaka kubaki nchini Marekani, ilikuwa ni lazima kwenda huko.

Alijiamini kwamba alikuwa na sura nzuri, mwili uliojengeka, alijua fika kwamba mara baada ya Maria kumuona ilikuwa ni lazima kumtamani na kutaka kulala naye. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa, alivyoonana na msichana huyo hotelini, akampenda na kuchukua namba yake ya simu.

Wakaanza kuwasiliana, alimdanganya kwamba alikuwa na mkewe hotelini, hakutaka kuona msichana huyo akipata muda wa kuwa naye kwa kujiachia, alitaka kumuingizia hofu ajue kwamba kweli mwanaume huyo alikuwa na mkewe hapo hotelini.

Mazungumzo yao yalikuwa ya kwenye simu, walitumiana meseji za mapenzi, kwa kipindi kifupi tu tayari Maria alionekana kufa na kuoza, hakutaka kuona mwanaume Fareed akiendelea kuwa na mkewe, alijipanga na alijipiza kwamba ni lazima alale naye kwa gharama yoyote ile.

“Siwezi kumuacha mwanaume mwenye mwili mzuri kama yule, nitamuachaje mwanaume mwenye sura nzuri kama yule?” alijiuliza.

Hakutaka kuona hilo likitokea, alijipiza kwamba ni lazima amfuate kitandani, alale naye na kufanya naye mapenzi. Ni kama Keith alijua, ukaribu kwa Maria ukaongezeka zaidi au kwa Kiswahili chepesi cha mtaani ni kwamba alikuwa akikaba mpaka penalti.

“Bebi naomba nionane na wewe,” aliandika ujumbe mfupi.

“Leo!”

“Ndiyo! Kesho tunaondoka!”
“Kwenda wapi?”
“Misri!”

“Kuna nini?”
Tunakwenda kuangalia mapiramidi ya Giza!”

“Ooh! Nitakuweepo huko, nitakuja peke yangu kuonana nawe,” aliandika Fareed.

“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Niahidi kama tutakuwa wote!”
“Nakuahidi!”

Moyo wa Maria ukaridhika, hakuamini kama hatimaye mwanaume huyo alikubaliana naye kwamba wangeonana na kufanya mambo yao. Moyo wake ukawa na furaha tele, akajitupa kitandani huku akiiona dunia yote kuwa yake kwani kile alichotaka kukisikia ndicho alichoambiwa na mwanaume huyo.

“Nitalala naye na kumuonyeshea kwa nini yule babu amepagawa kwa penzi langu,” alisema Maria na kujilaza kitandani huku akiisubiri kesho ifike, waondoke kuelekea Misri ambapo huko angeonana na mwanaume huyo.

****

Keith hakutaka kukaa sana na mpenzi wake nchini Italia, alichokifanya ni kuondoka na kuelekea katika Mji wa Giza, nchini Misri kwa ajili ya kuyatazama mapiramidi yaliyokuwa nchini humo.

Njiani, bado walionyesheana mapenzi ya dhati, walikuwa wakibusiana sana lakini mawazo ya Maria hayakuwa hapo, alimfanyia mwanaume huyo kila kitu lakini moyo wake, kichwa chake, vyote vilikuwa vikimfikiria Fareed, mwanaume ambaye hakujua kama alikuwa akitoka kimapenzi na mpenzi wake.

Ndege haikuchukua muda mrefu ikafika nchini Misri ndani ya Jiji la Cairo ambapo hapo wakachukua basi lililowapeleka mpaka katika Mji wa El Giza. Macho ya Maria yalishangaa, hakuamini kile alichokuwa kikiona, aliyaona mapiramidi makubwa ambayo alikuwa akiyasoma kwenye vitabu na wakati mwingine kuyaangalia kwenye televisheni.

Alishangaa mno, wakati mwingine alitamani kulia kwani furaha aliyokuwa nayo kipindi hicho ilikuwa kubwa sana. Akamkumbatia mpenzi wake, Keith na kumshukuru sana kwa kumsafisha macho kwa kumpeleka nchini Misri.

“Tutakwenda kule kesho, leo tulale hotelini,” alisema Keith, wakati huo waliyaona mapiramidi yale yakiwa mbali kabisa.

Walipoingia hotelini, kama kawaida wakaanza kucheza michezo ya kimahaba kitandani, kila mmoja alimtamani mwenzake, kila mmoja alihitaji sana kuwa na mwenzake wakati huo.

Japokuwa Maria alijitoa sana kama ilivyo kawaida yake lakini kichwa chake hakikuacha kumfikiria Fareed, kwake, mwanaume huyo alikuwa kila kitu, alikichanganya kichwa chake, muda mwingi alikuwa na mawazo tele juu yake.

Walipomaliza kucheza, wakatoka kitandani na kuelekea bafuni kuoga na walipomaliza, wakaenda kula chakula. Muda mwingi Maria alikuwa akiangalia huku na kule, macho yake hayakutulia, alikuwa akimtafuta mwanaume wake, alitaka kujua kama alifika mahali hapo au la.

Hakuacha kuangalia na simu yake pia, aliingia WhatsApp kwa kuhisi labda mwanaume huyo angekuwa amemtumia ujumbe mfupi lakini napo hakuona kitu jambo lililomshangaza mno.

“Amekuja kweli au alinidanganya kuniridhisha?” alijiuliza huku akionekana kushtuka. Wakati akiwa bize na simu yake huku akijiuliza maswali mengi, Keith akagundua kwamba mpenzi wake huyo hakuwa sawa.

“Kuna nini?” aliuliza Keith swali lililomfanya Maria kushtuka.

“Eeh!”
“Kuna nini?”
“Nina mawazo sana, nimekuwa nikiwafikiria sana wazazi wangu!” alijibu Maria, alikuwa akimdanganya.

“Pole sana! Ila tutakwenda. Nakuahidi kwamba tukitoka hapa, tunaelekea Nigeria,” alisema Keith.

“Kweli?”
“Ndiyo!”

Kidogo Maria akajifanya kuwa na furaha lakini ukweli ni kwamba bado moyo wake ulikuwa na mawazo tele kwani mwanaume aliyekuwa akimpenda kwa penzi la dhati kutoka moyoni mwake hakuwa amewasiliana naye kwenye simu japokuwa alimuahidi kufanya hivyo.
Akainuka na kurudi chumbani. Huko, hakutulia, alijilaza kitandani lakini kichwa chake kilikuwa mbali kabisa. Keith alipoingia na kumuona msichana huyo kajilaza, akajua kwamba alikuwa na uchovu wa safari hivyo kumuacha na kuondoka kwenda baa kunywa pombe.

Kule ndani, Maria akachukua simu yake na kuanza kumtafuta mwanaume huyo kwa kumtumia meseji mbalimbali kwenye Mtandao wa WhatsApp, japokuwa hakuwa hewani lakini aliamini kwamba mara atakapofungua akaunti yake basi angekutana na ujumbe aliokuwa amemtumia.

Wala hazikupita hata dakika thelathini, akapokea ujumbe kutoka kwa Fareed ambaye alimwambia kwamba na yeye mwenyewe alifika na kuchukua chumba ndani ya hoteli hiyo.

“Unasemaje?”
“Nipo chumba namba ishirini!”
“NAkuja!”
“Eeh! Nipo na mke wangu mpenzi! Subiri, leo usiku nitakushtua. Mnakwenda muda gani kwenye piramidi?” aliuliza Fareed.

“Kesho asubuhi!”
“Basi na mimi nitakuwepo huko mpenzi!” alisema Fareed.

Moyo wa Maria ukafarijika, akajisikia furaha moyoni mwake, hakuamini kama mwisho wa siku mwanaume huyo angemtumia ujumbe na kumwambia kwamba tayari alifika nchini Misri. Akasimama na kuanza kuzungukazunguka ndani ya chumba kile, kwa jinsi alivyojisikia moyoni mwake, alikuwa radhi kufanya jambo lolote lile mahali hapo.

Siku hiyo alilala kwa amani kabisa tena akiwa amekumbatiana na mpenzi wake, Keith. Ilipofika asubuhi, wakaamka na kuelekea bafuni ambapo baada ya kumaliza, wakaondoka na kuchukua gari ndogo na kwenda kulipokuwa na mapiramidi yake.

“Huku utafurahia kwa roho yako! Ni pazuri na kunasisimua sana,” alisema Keith.

“Leo nitajione mwenyewe mpenzi!” alisema Maria.

Wakati wao wakielekea huko, huku nyuma Fareed alikuwa akitoka chumbani kwake. Siku hiyo alidhamiria kufanya mauaji, alikumbuka vema Keith alichokuwa amemfanyia, moyo wake ulikuwa na hasira naye na hakutaka kumwacha hata kidogo.

Alikuwa radhi kumuua kwa sababu tu aliyaumiza maisha yake, alikuwa tayari kumuua kwani hapo kabla mwanaume huyo alitaka kumuua, pasipo kuokolewa na mvuvi, angekuwa tayari marehemu.

Akaingia ndani ya gari na kuanza kwenda kwenye mapiramidi yale. Hawakuchukua muda mrefu wakafika ambapo akateremka na kuanza kuelekea kule kulipokuwa na piramidi kubwa.

Kulikuwa na idadi kubwa ya watu waliokuwa wamefika mahali hapo. Wengi walisafiri kutoka nchini mwao na kufika Misri kwa ajili ya kuangalia jinsi mapiramidi hayo makubwa yalivyokuwa yametengenezwa.

Fareed alisimama mbali kabisa, aliwaona wakiwa wamesimama karibu na geti huku wakisubiri kufunguliwa kwa geti na kuingia ndani. Ilipofika saa mbili kamili, muda wa kufungua mageti, likafunguliwa na watu kujiandikisha na kuanza kuingia ambapo kwa hatua za haraka sana, naye Fareed akaanza kwenda kule, alipofika, akalipia na yeye kuingia.

“Huu ndiyo mwisho wake,” alijisemea.

Alivalia kofia kubwa, ilikuwa vigumu sana kumgundua, ndani ya piramidi lile, walikuwa wakitembea huku na kule, hakukuwa na mtu aliyekuwa akimfuatilia mwenzake, kila mmoja alionekana kuwa bize na mambo yake.

“Today is the day!” (leo ndiyo siku yenyewe) alisema Fareed huku akigusa kisu chake kuona kama kilikuwepo kiunoni.

****

Ndani ya piramidi kulikuwa na mwanga hafifu, watu waliokuwa ndani ya piramidi hilo walikuwa wakiongozwa na watu maalum waliokuwa na kazi ya kuwatembeza watu huku na kule.

Macho ya Maria hayakutulia, muda wote alikuwa akiangalia huku na kule, alitaka kumuona mwanaume aliyeuteka moyo wake, alimwambia kwamba angekuwa mahali hapo pamoja naye lakini mpaka muda huo hakumuona na hakugundua kwamba alikuwa katika kundi la watu waliokuwa wameingia na kundi hilo.

Fareed hakutaka kuonekana, macho yake yalikuwa chini, hakutaka kukutanisha macho yake na msichana Maria. Waliendelea kusonga mbele, hakuwa akimsikiliza muongozaji aliyekuwa akiwaambia kuhusu kila kitu kilichokuwa mule ndani.

Alichokifanya Fareed ni kuchukua simu yake na kumtumia ujumbe mfupi Maria kwamba watakapofika sehemu kubwa, basi aachane na Keith na kumfuata yeye.

“Sawa. Utaniambia utakapokuwa,” alisema Maria, kidogo moyo wake ukapoa, alikuwa na hofu kubwa na alipowaangalia vizri watu wale waliokuwa katika kundi lile, akamuona mwanaume huyo japokuwa kulikuwa na mwanga hafifu.

Walikwenda mpaka walipofika sehemu kubwa, ilionekana kuwa kama uwanja fulani, sehemu ambayo Wamisri kwa zamani walitumia kama sehemu za wafalme kufanya vikao na viongozi wengine, kwa pembeni, kulikuwa na vyumba vingi ambavyo vingine vilitumika kama vyumba vya kulalia lakini vingine vilitumika kama makaburi.

“You can go to other rooms to have a look,” (mnaweza kwenda kwenye vyumba vingine kuangalia) alisema msimamizi.

Keith hakutaka kumuachia Maria, alimshikilia msichana huyo na kuanza kwenda kwenye chumba kimoja. Kwenye chumba walichokuwa wakienda, walikuwa wawili tu.

“Baby! Just wait,” (mpenzi! Subiri kwanza!) alisema Maria.

“What’s wrong?” (kuna tatizo gani?)

“I have seen my aunt?” (nimemuona shangazi yangu)

“Where is she?” (yupo wapi?)

“In that room,” (ndani ya chumba kile) alisema Maria huku akijifanya kuwa na hofu.

Alimdanganya mwanaume huyo, aliyemuona hakuwa shangazi yake bali mwanaume ambaye alitamani sana kulala naye. Akataka kuondoka hapo kumfuata Fareed, Keith alipong’ang’ania akamwambia kwamba huo si muda mzuri wa kumuona shangazi yake kwani hakuwa akijulikana nyumbani na haikuwa mila za kiafrika.

Keith hakuwa na jinsi, kwa kuwa alimpenda sana msichana huyo, akamuacha aendele kwa huyo shangazi yake na yeye angemsubiri ndani ya chumba hicho.
Wakati hayo yote yakiendelea, Fareed alikuwa akiangalia kupitia mlangoni huku akiwa ametokeza jicho tu. Alipomuona Maria akianza kuja kule alipokuwa, kwa haraka sana akapitia mlango mwingine, wakati msichana yule akiingia ndani ya chumba kile, na yeye alikuwa akitoka kutoka katika mlango mwingine.

Alitakiwa kuwa na haraka sana, hakutakiwa kupoteza muda hata mara moja. Akatembea kwa mwendo wa haraka mpaka katika chumba alichokuwemo Keith, akaingia ndani.

“Who are you?” (wewe nani?) aliuliza Keith kwani kwa jinsi Fareed alivyoingia ndani ya chumba kile, alionekana kama mtu mwenye haraka nyingi.

“Nobody!” (si mtu yeyote) alijibu Fareed,

ITAENDELEA KESHO.

FULL Hadithi ipo hapa

Android ===>Google Play

iOS ===>Apple Store

Leave A Reply