The House of Favourite Newspapers

Michirizi Ya Damu – 15

“Nigeria!”
“Ooh! Sawa. Kwenda Ulaya si tatizo. Ila una pesa?” aliuliza kijana mmoja.

“Kiasi gani?”
“Kukufanyia mpango ni paundi mia tano. Ukiingia ndani ya meli, mwenyewe utatakiwa kumlipa,” alisema kijana mmoja.

“Kiasi gani?”
“Huwa anahitaji paundi elfu moja!”
“Hilo si tatizo!”
“Una passipoti?”
“Ndiyo!”
“Umegongewa viza?”
“Yeah! Ya hapa ila nilikuwa mpitaji tu!”

“Sawa.”

Hiyo ndiyo ilikuwa kazi yao kubwa, walikuwa wakiwasafirisha watu wengi katika Mfereji wa Suezi kuelekea nchini Uturuki, Hispania au Ugiriki. Walikuwa wakilipwa kiasi kikubwa cha fedha ambacho waligawana na watu wa ulinzi na kuwaruhusu watu hao kupita bila tatizo lolote lile.

Fareed alipowapa kiasi hicho, wakachukua mtumbwi mmoja na kuanza safari ya kufuata meli moja kubwa ya mizigo. Kabla ya kuifikia, wakawasiliana na nahodha aliyekuwa akihusika katika meli hiyo, walimwambia kwamba walikuwa na mtu aliyetaka kuingia nchini Uturuki.

Hilo halikuwa tatizo, walipofika katika meli hiyo, wakakaribishwa kinyemela, nahodha, Mzee Ahmed akakabidhiwa kiasi chake cha dola elfu moja na kumpeleka Fareed ndani ya chumba kimoja cha siri kilichokuwa na mizigo mingi na kumwambia akae huko.

Moyo wa Fareed ukaridhika, akahisi kwamba hiyo ndiyo njia salama ya kuepuka mkono wa sheria nchini Misri. Alijifungia ndani ya chumba hicho, baada ya saa kadhaa, meli ikatoa nanga mahali hapo na kuanza safari ya kuelekea Cyprus kabla ya kuingia nchini Uturuki.

Mfereji Wa Suez ulikuwa ni miongoni mikubwa duniani, ukiachana na mfereji wa Panama, huu ndiyo uliokuwa ukishika nafasi ya kwanza kabisa kwa urefu ambao ulikuwa na urefu wa kilometa 102 huku ukiwa na madaraja mawili makubwa ambayo yalikuwa yakitoka Cairo ambapo ni Magharibi mwa Misri kwenda Sinai ambapo ni Mashariki mwa Misri.

Safari ilikuwa ikiendelea, njiani, kulikuwa na vizuizi vingi walitakiwa kuvipitia na kote huko meli ya Mzee Ahmed ilikuwa ikiachiwa, haikuwa ikikaguliwa kwani kazi yake kubwa ya kuwavusha watu ilijulikana na alikuwa akiwapoza kiasi fulani cha pesa.

Kwake, safari haikuwa ngumu, alipita Ismailia, meli iliendelea mbele mpaka Al Firdan, kote huko alipokuwa akipita, hakuwa na hofu yoyote ila kitu kilichomfanya kuona ugumu wa kumvusha Fareed ni kwenye bandari ya Said ambayo ndiyo ilikuwa ya mwisho kuelekea nchini Cyprus.

Alimuomba Mungu kwani watu wa hapo hawakuwa wakikubali kuiona meli yoyote ikivuka na watu ambao walikuwa wakizamia Ulaya. Kila meli ilipekuliwa vilivyo na kitu ambacho kilikuwa kikimsaidia Mzee Ahmed kutokugundulika kama alikuwa akiwavusha watu ni kwamba alikuwa akiwaweka katika chumba ambacho kilikuwa karibu na injini.

Ili kumuweka mtu humo kulitakiwa kuwa na maandalizi makubwa, ilitakiwa chumba kiandaliwe wiki moja kabla. Kwa Fareed ilikuwa vigumu kumuweka humo kwa kuwa alikuwa mteja wa ghafla ambapo hawakuwa wameandaa chumba kama kinavyotakiwa na hivyo kuepelekwa katika chumba kingine.

Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika bandari hiyo, walipofika katika bandari hiyo, meli hiyo ikawekwa katika foleni na meli nyingine, walitakiwa kubaki mahali hapo mpaka meli walizozikuta zikaguliwe na ndipo waendelee na safari.

Wakati huo, picha za Fareed zilikuwa zimesambaa kila kona, zilibandikwa na kila mtu alitaka kumkamata mtu huyo. Mbali na kuwatafuta watu waliokuwa wakivuka kuelekea barani Ulaya lakini pia walikuwa wakimtafuta Fareed ambaye mpaka katika kipindi hicho hawakujua mahali alipokuwa.

Meli ikakaa siku ya kwanza, Mzee Ahmed alikuwa na kazi ya kumpelekea chakula, ikakaa siku ya pili na siku ya tatu ilipoingia ndipo zamu yao ilipofika. Mzee huyo hakuwa na hofu, hakudhani kama polisi wangeweza kuingia mpaka katika chumba kile kwani haikuwa kawaida yao.

Siku hiyo, mbali na kuwatafuta watu waliokuwa wakizamia, ilikuwa ni lazima wamtafute na Fareed. Walihisi kwamba mtu huyo angeweza kutumia nafasi hiyo kutorokea nchini Cyprus ambapo hakukuwa mbali kutoka katika bandari hiyo.

“Leo ni tofauti na siku nyingine,” alisema mwanajeshi mmoja.

“Kivipi?”

“Tutapekua kila kitu katika meli yako. Mbali na watu wanaozamia, pia kuna mtu tunamtafuta. Ni mtu hatari sana,” alisema mwanajeshi huyo.

“Ni nani? Kafanya nini?”
“Amefanya mauaji ya bilionea!”
“Mauaji ya bilionea? Eeh! Ndiyo kwanza nasikia leo,” alisema Mzee Ahmed.

Moyo wake ulikuwa na hofu, hakujua kama mtu aliyempakiza kwa ajili ya kumvusha kwenda nchini Uturuki ndiye ambaye alikuwa akitafutwa. Wanajeshi wanne wakafika mahali hapo, huku wakiwa na bunduki zao, wakaingia ndani ya meli hiyo.

Siku hiyo hawakutakiwa kuangalia sana kuhusu wazamiaji, mtu waliyekuwa wakimtaka alikuwa Fareed tu. Wakaingia kwenye vyumba vyote vya juu, hawakukutana na mtu huyo kwani hata wafanyakazi wa kiume waliokuwa humo walivuliwa kila kitu na kuangalia ili kujua kama walikuwa yeye au la.

“Bado vyumba vya chini. Leo tutapekua meli nzima,” alisema mkuu wa kikosi kilichokuwa mahali hapo katika Bandari ya Said.

Wakaelekea chini, kule kulipokuwa na chumba alichokuwemo Fareed, wakaanza na vyumba vingine, wakaangalia katika vyumba vyote, vikabaki vyumba viwili, kile alichojificha Fareed na chumba kingine kilichokuwa karibu na chumba cha injini.

Wakajaribu kuufungua mlango wa chumba hicho, haukufunguka. Walijua kwamba ulifungwa kwa nje, na kama ulifungwa basi kuna uwezekanao humo kukawa na kitu. Walichokifanya ni kumuita mzee Ahmed na kumwambia afungue ndani ya chumba hicho, ilikuwa ni lazima wapekue.

“Eeeh!”

“Fungua chumba hiki,” alisema mkuu wa kikosi, Mzee Ahmed alibaki akitetemeka, hakuogopa kukamatwa kwa Fareed kama muuaji bali alichoogopa ni kukamatwa kwa Fareed kama mzamiaji. Siku hiyo kila mwanajeshi alibadilika kana kwamba hawakuwa wale watu aliokuwa akiwahonga kuwavusha watu wengine kwenda Ulaya.

“Fanya haraka tunataka kuwahi,” alisema mkuu yule.

“Sawa,” aliitikia mzee Ahmed na kuufungua mlango. Moyo wake ulikuwa na presha kubwa, akajua huo ndiyo mwisho wa Fareed kukamatwa ndani ya meli hiyo.

****

Fareed alikuwa ndani ya meli, moyo wake ulikuwa na shauku kubwa ya kufika nchini Uturuki. Alikuwa na hofu moyoni mwake, alihisi kwamba huo ingewezekana kuwa mwisho wa maisha yake kwani kila alipoangalia, hakuamini kama angefika salama nchini humo.
Alibaki ndani ya chumba hicho huku akiwa na hofu kubwa. Meli ilipofika katika Bandari ya Said, akashtuka kuona meli ikizimwa. Mara ya kwanza alihisi kwamba ilikuwa tayari imefika nchini Uturuki lakini alipoangalia muda waliotumia, akahisi kwamba kulikuwa na kitu, hasa msako wa kumtafuta yeye.

Hakutaka kukamatwa, hakutaka kuona kwamba huo ndiyo uwe mwisho wake, ilikuwa ni lazima ajifiche ili asiweze kuonekana na watu hao hivyo alichokifanya ni kuangalia ndani ya chumba hicho kuona kama angeweza kuona kitu chochote ambacho kingemfanya kujificha.

Humo ndani kulikuwa na maboksi mengi na kitu kilichomfurahisha zaidi ni kwamba kulikuwa na maboksi makubwa ambayo yengemfanya kuingia ndani na kujificha.

Hakutaka kuchelewa, hapohapo akalifuata boksi moja kubwa, akalisogeza pembeni kabisa kisha kulifungua, mule ndani hakukutana na vitu vingi vizito, aliona kukiwa na vitambaa vingi vya kushonea kanzu hivyo alichokifanya ni kuvitoa, akaingia, akavirudisha juu yake na kulifunga boksi hilo kwa ustadi mkubwa.

Akahisi kwamba hapo angefanikiwa kujificha na kutokugundulika. Baada ya dakika kadhaa, akasikia watu wakiongea nje ya chumba hicho na baada ya sekunde chache mlango kufunguliwa na kuingia ndani.

Wanajeshi wale walidhamiria kuyafungua maboksi yote, waliamini kwamba inawezekana humo ndani kulikuwa na mtu waliyekuwa wakimtafuta. Mkuu wa kikosi akawaagiza watu wake wayafungue maboksi yale na kuangalia ndani.

Mzee Ahmed alibaki akitetemeka, kitendo cha kumkosa Fareed ndani ya chumba kile ilionyesha kwamba mwanaume huyo alikuwa amejificha ndani ya boksi mojawapo hivyo kuona kwamba kama asingemtumia shetani mkubwa duniani, pesa basi mtu huyo angeonekana na kugundulika kwamba alikuwa akimsafirisha mzamiaji.

“Hivi kweli dola mia mbili haziwezi kuniruhusu kuondoka niwahi?” aliuliza Mzee Ahmed.

“Mia mbili?”
“Ndiyo!”

“Ongeza kidogo!”
“Basi mia tano! Ilimradi niwahi tu!”

Kiasi alichokitaja kilikuwa kikubwa, mkuu wa kikosi kile alijua kwamba walikuwa wakipoteza muda na mule ndani hakukuwa na mtu yeyote yule. Hakutaka kuona pesa hizo zikimpita, uchumi ulikuwa mbaya na hivyo kukubaliana na Mzee Ahmed kwamba ampe kiasi hicho na kumruhusu kuondoka.

Akawaambia vijana wake waachane na upekuzi na hivyo waondoke ndani ya meli hiyo. Vijana wale walitii na kuondoka pasipo kujua kwamba mkuu wao alikuwa amepewa mkwanja chinichini.

Hiyo ndiyo ikawa salama kwa Fareed, kule ndani ya boksi alipokuwa, baada ya kusikia watu wakiondoka akashusha pumzi nzito na kumshukuru Mungu. Baada ya muda, meli ikawashwa na kuanza kuondoka mahali hapo.

“Asante Mungu! Ndiyo maana niliamua kuyabadilisha maisha yangu kwa ajili yako ila yule mpumbavu aliamua kuyaharibu tena,” alisema Fareed huku akionekana kuwa na furaha tele.

Mzee Ahmed alifurahi, alipoianza tena safari hakuamini kama alikuwa amefanikiwa kuondoka bandarini hapo. Hakujua kama mtu aliyekuwa amembeba alikuwa akitafutwa kila kona hapo Misri tena huku mtu ambaye angefanikisha kukamatwa kwake angelipwa kiasi kikubwa cha pesa.

Safari ya siku nne ikaendelea majini, ilikuwa ni lazima wapite Cyprus hata kabla ya kuelekea Uturuki. Ilikuwa ni safari ndefu ya majini lakini walitakiwa kuvumilia. Fareed aliyekuwa ndani ya chumba kile, akapewa uhuru wa kuzungukazunguka ndani ya hiyo meli kwani kusingekuwa na mtu yeyote ambaye angewababaisha kwani tayari waliondoka barani Afrika.

Baada ya siku nne kukatika, wakafika Cyprus na meli kutia nanga katika bandari kubwa ya Limmasol ambapo wangekaa hapo kwa siku mbili na kuondoka kwenda kutia nanga katika Bandari ya Latchi kabla ya kuendelea na safari yao ya kuelekea nchini Uturuki.

“Utahitaji kutembeatembea katika Mji wa Limmasol?” aliuliza Ahmed.

“Hapana! Nitakaa humuhumu. Nitatoka nikifika nchini Uturuki!” alisema Fareed.

“Hakuna tatizo! Ngoja tukale bata kwanza na warembo wa Kicyprus,” alisema Mzee Ahmed huku akionekana kuwa na furaha mno.

Walitumia siku sita nchini Cyprus mpaka kuiacha nchi hiyo na kuelekea nchini Uturuki. Hakukuwa na umbali mkubwa, ni ndani ya siku saba tu meli ikaanza kuingia katika Bandari ya Akdeniz iliyokuwa katika Jiji la Antalya.

“Tumefika Uturuki! Utakwenda wapi sasa?” aliuliza Mzee Ahmed huku akimwangalia mwanaume huyo.

“Popote pale.”
“Kwa hiyo utaishi hapa?”
“Kwa muda!”
“Halafu?”
“Nataka kuondoka kuelekea Marekani!”
“Unataka kwenda Marekani?”

“Ndiyo!”

“Utafikaje?”
“Kivyovyote vile,” alisema Fareed.

“Hautakiwi kuhisi. Ngoja nitafute mtu wa kukusaidia,” alisema Mzee Ahmed na kuchukua simu yake na kuwasiliana na mtu mmoja upande wa pili.

Fareed akashukuru Mungu, hakuamini kama angepata urahisi wa kuingia nchini Marekani kama ule aliokuwa amepewa. Alimshukuru Mzee Ahmed kwani alionekana kuwa mwanaume mwema kabisa.

Mara baada ya mzee huyo kumaliza kuzungumza na mtu huyo, akamwambia Fareed asubiri ambapo baada ya saa moja, mwanaume mmoja akafika hapo bandarini ambapo kinyemela akamchukua Fareed na kuondoka naye.

Mzee huyo akajitambulisha kwa jina la Al Fakh. Alikuwa mzee mwenye ndevu nyingi mno, aliongea kitaratibu sana, hakuwa na mapepe, alikuwa mwanaume mstaarabu sana kiasi kwamba wakati mwingine Fareed alihisi kwamba mwanaume huyo alikuwa mtumishi wa Mungu hapo Uturuki.

Walizungumza mambo mengi mno, Fareed alimdanganya mzee huyo kwamba alitaka kwenda nchini Marekani kwa kuwa alikuwa mzamiaji, alitaka kwenda kutafuta maisha nchini humo. Mzee Al Fakh alifurahi sana, akamwambia kwamba angemsaidia kwa hali na mali pasipo gharama zozote zile.

“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Nashukuru sana!”

Wakachukua dakika chache wakafika nyumbani kwa mzee huyo. Ilikuwa nyumba kubwa, yenye walinzi wengi na kila kitu kwa ndani. Wakaingia ndani, akakutana na familia ya mzee huyo ambaye alimkaribishwa kwa furaha tele.

Akapelekwa katika chumba ambacho alitakiwa kukaa kwa siku zote ambazo angesubiri safari ya kwenda nchini Marekani. Moyo wa Fareed ulikuwa na furaha tele, hakuamini kama kweli alikutana na familia ya watu waliokuwa na upendo mkubwa kama watu hao.

“Jisikie huru!” alisema mzee huyo.

“Nashukuru sana!”

ITAENDELEA KESHO

Comments are closed.