The House of Favourite Newspapers

Michirizi Ya Damu – 17

Aliendelea kumwambia rubani yule ashushe ndege kwa kiasi fulani ili aweze kuruka. Baada ya kubembelezwa sana hatimaye rubani huyo akaishusha ndege hiyo kwa umbali wa mita hamsini kisha kumruhusu Fraeed kuruka.
“Una parachuti?” aliuliza rubani.
“Hapana!”
“Boya!”
“Hapana!”
“Hebu subiri!” alisema rubani huyo.
Akaangalia chini ya kiti chake, akaona boya la kuvaa na kumwambia Fareed alivae kwani hapo alipokuwa akirukia palionekana kuwa sehemu ya hatri sana. Hilo halikuwa tatizo, akalichukua boya hiyo, akalivaa, akaufungua mlango na kisha kuruka baharini.
Alikuwa kwenye hali mbaya, wakati mwingine alishindwa kuhema vizuri kutokana na upepo mkali uliokuwa ukiendelea kuvuma. Baada ya sekunde chache akatumbukia ndani ya maji.
Bahari ilichafuka, kulikuwa na mawimbi makubwa yaliyopiga huku na kule. Fareed alipelekwa huku na kule, hakutulia baharini pale, kitu kilichokuwa kikimsaidia kilikuwa ni lile boya tu alilokuwa amelivaa.
Ilikuwa ni mchana lakini kitu cha ajabu, kulionekana kama jioni, hakuweza kuona hata mita kumi na tano kutoka pale alipokuwa. Alikiona kifo, mawimbi makubwa yaliendelea kumpiga na kumpeleka huku na kule mpaka kuona kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake.
“Mungu nisaidie,” alisema Fareed huku mawimbi yakiendelea kumpeleka huku na kule.
****
Bilionea Belleck alikuwa kwenye kiti chake ofisini kwake, masikio yake yalikuwa kwenye simu yake iliyokuwa mezani. Alikuwa na presha kubwa, alitaka kuona simu kutoka kwa De Leux ikiingia na kumpa taarifa kwamba tayari walifanya mauaji ya Fareed ili moyo wake uridhike.
Muda ulizidi kusonga mbele, dakika ziliendelea kukatika lakini hakukuwa na taarifa yoyote ile. Moyoni mwake akawa na hofu, akahisi kabisa kwamba watu hao walishindwa kumuua au kulikuwa na tatizo jingine ambalo lilitokea.
Aliwaambia kwamba walitakiwa kufanya mauaji hayo haraka sana baada ya ndege kupaa lakini kitu cha ajabu kabisa hakukuwa na simu iliyoingia kumpa taarifa hiyo ambayo aliamini kwamba ingeufanya moyo wake kumtukuza Mungu kwa hicho kilichotokea.
Baada ya kupita saa mbili, akaamua kumpigia mwanaume huyo ili kujua ni kitu gani kiliendelea. Simu haikuwa ikipatikana, ilionekana kuzimwa kitu kilichomuudhi sana Belleck kwa kuona kwamba amedharauliwa.
Alichokifanya ni kumtumia ujumbe wa sauti (voice mail) ili atakapoiwasha simu yake aweze kuipata sauti hiyo na kumwambia kitu kilichokuwa kimeendelea.
“Kitu gani kinaendelea? Kwa nini umekuwa kimya sana? Mmekamisha au bado hamjakamilisha? Hebu ukifungua simu nitafute nijue manake nilishatuma pesa, kama amekufa niambie nizitoe pesa kabla hajathibitisha kuzipata,” alisema Belleck huku simu ikiwa sikioni mwake.
Moyo wake haukuwa na amani hata kidogo, bado aliendelea kuwa na hofu kwamba inawezekana kulikuwa na jambo lililokuwa limetokea huko. Hakutulia, moyo wake ulikuwa na shaka tele kwa kuona kwamba kama Fareed hakuuawa basi kile kiasi alichokuwa amemtumia, kingeweza kuondoka mikononi mwake jumla kama tu mwanaume huyo angethibitisha kukipokea ndani ya siku saba.
Alitaka afe haraka iwezekanavyo! Alifanya kazi aliyoitaka, mtu aliyetakiwa kuuawa aliuawa hivyo alichokuwa akikiangalia kwa sasa ni kupewa taarifa kwamba kazi ile ilifanyika.
Siku ya kwanza ikapita, ukimya ukatawala, siku ya pili nayo ikapita, ukimya ukatawala, siku ya tatu na nne nazo zikaingia lakini hakukuwa na taarifa yotoye ile kama Fareed aliuawa au la, mbaya zaidi hata alipokuwa akimpigia simu rubani, naye hakuwa akipatikana.
****
Fareed alikuwa akielea juu ya maji, alipelekwa kila kona na kitu kilichokuwa kikimsaidia asizame ni lile boya alilokuwa amelivaa. Aliendelea kuelea mpaka bahari ilipotulia, akaangalia huku na kule na kwa mbali sana akafanikiwa kukiona kisiwa kimoja, hakikuwa kikubwa sana, kilikuwa kidogo hivyo kuanza kupiga mbizi kuelekea kule.
Alichoka, maji yalimchosha, yalimpeleka huku na kule, mikono yote alihisi ikiuma kupita kawaida. Japokuwa kisiwa kile kilionekana kuwa kama umbali wa nusu kilometa lakini alitumia dakika arobaini na tano mpaka kukifikia.
Kilikuwa kisiwa kilichokuwa na miti mingi, hakujua kilikuwa nchi gani lakini kwa jinsi kilivyoonekana, hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akiishi humo. Akazunguka huku na kule, aliogopa, moyoni mwake alihisi kama angekutana na watu wabaya, au wala wala watu waliokuwa wakipatikana katika nchi nyingine lakini kwa bahati nzuri kwake hakuweza kukutana na mtu yeyote yule.
Alitafuta sehemu chini ya mti na kutulia, macho yake yalikuwa yakiangalia huku na kule kutafuta msaada, pale alipokuwa ilikuwa ni sawa na mtu aliyetengwa, kila kona alipoangalia, hakuona kitu au mtu yeyote yule zaidi ya kisiwa kile kuzungukwa na bahari kila upande.
Alihisi baridi, hicho kilikuwa kisiwa kilichokuwa katika Bahari ya Atlantiki, moja ya bahari zilizokuwa na baridi kali. Alibaki akitetemeka pale alipokuwa kiasi kwamba mpaka akahisi kuwa muda wowote ule angeweza kufa.
Alitulia kwa saa moja, hakuona msaada wowote ule zaidi ya maji yale yaliyokuwa yamezunguka kisiwa kile. Alikaa mpaka usiku, giza likaingia, hakuwa na sehemu salama ya kulala zaidi ya mtini, tena huku akiangalia huku na kule.
Usiku mzima alikesha macho, moyo wake ulimwambia kwamba kungekuwa na msaada kutoka mahali fulani lakini kitu cha kushangaza mpaka inafika asubuhi hakukuwa na msaada wowote ule alioweza kuupata kitu kilichomfanya kukosa tumaini la kuondoka kisiwani hapo.
“Inamaana ndiyo nitakufa hapa?” alijiuliza huku akiangalia huku na kule.
“Labda! Lakini haiwezekani hata kidogo! Siwezi kufa kirahisi namna hii,” alijisemea huku akiteremka kutoka mtini.
Siku hiyo alishinda katika kisiwa hicho, alipokuwa akisikia njaa, aliingia katika pori lililokuwa kisiwani hapo, akachuma makomamanga na kuanza kula. Hayo ndiyo yakawa maisha yake, alipata tabu mno kisiwani humo, alitamani kuondoka lakini ilishindikana kwa kuwa tu hakukuwa na msaada wowote uliotokea.
Alidhamiria kurudi nchini Marekani, ilikuwa ni lazima kwenda kukamilisha kazi aliyokuwa ameiacha. Aliwaua watu wawili ambao walidiriki kumuondoa duniani lakini kutokana na ujanja wake, akanusurika kufa.
Hakutaka kuwaacha watu hao, akawaua na hivyo kubaki mtu mmoja ambaye alikuwa Padri Luke. Naye ilikuwa ni lazima amuue kwa kile alichomfanyia. Moyo wake haukujisikia hukumu wala huzuni, alichokuwa akikihitaji ni kuhakikisha mwanaume huyo anakufa kama walivyokufa wenzake.
Muda ulizidi kwenda mbele, alishindia makomamanga, hakuweza kupata chakula kingine zaidi ya hicho. Aliendelea kuishi kwa mateso makubwa, kila siku akawa anapigwa na baridi kali, alihuzunika mno, aliumia moyoni mwake na wakati mwingine alihisi kwamba huko ndipo ambapo kungekuwa nyumbani kwake milele, hakuona kama angeweza kuondoka mahali hapo salama.
Kila wakati ilikuwa ni lazima kuangalia huku na kule, alitaka kuona kama angebahatika kuona meli yoyote ile ili aweze kuomba msaada lakini hilo halikuwezekana, kila kona alipoangalia aliona kuwa peupe.
“Mungu wangu! Ni nini hiki?” Fareed alishtuka, ghafla tu akaanza kusikia maumivu makali ya tumbo, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea tumboni mwake, akalishikilia tumbo lake vilivyo, alisikia maumivu mahali ambayo hakuwahi kuyasikia kabla.
Akaanza kusikia kichefuchefu na kuanza kukohoa, madonge ya damu yakaanza kumtoka mdomoni, alishindwa kuvumilia, akalala chini na kuanza kulia. Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea,
Hakupata msaada wowote ule ule. Baada ya dakika kadhaa, akaanza kutapika, madonge makubwa ya damu yakaanza kutoka. Akahisi kwamba yale matunda ndiyo yaliyokuwa yakimsababishia hali hiyo na kuanza kujitahidi kuyatema.
“Mungu nisaidie,” alisema Fareed huku akiwa kwenye hali mbaya, kwa jinsi tumbo lile lilivyoanza kuuma ghafla, akahisi kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake.
****
Mauaji ya Bwana Belleck yaliyokuwa yametokea nchini Ufaransa yalimshtua kila mtu, watu hawakuamini kile kilichokuwa kimetokea, ni ndani ya siku tatu mabilionea wawili walikuwa wameuawa na kwa jinsi alama za mauaji zilivyokuwa zikionyesha, kila mtu akagundua kwamba muuaji alikuwa mmoja.
Polisi walichanganyikiwa, wakawasiliana na polisi wa nchini Misri na kuwaomba kuwatumia picha ya mtuhumiwa, hilo halikuwa tatizo, picha ikatumwa na ilipowafikia, wao wenyewe walishangaa.
Alikuwa mtu yuleyule aliyekuwa akitafutwa sana na FBI kwa kosa la kulipua kituo cha treni cha Pennsylvania. Hawakujua sababu ya mwanaume huyo kufanya matukio yote hayo. Wengi walihisi kwamba alikuwa gaidi, lakini gaidi na mabilionea wale kulikuwa na kitu gani kilichokuwa kikiendelea?
Hakukuwa na aliyekuwa na majibu, kila mmoja alikuwa na hamu ya kumkamata Fareed na kuweka wazi kile kilichokuwa kikiendelea mpaka kufanya matukio yote hayo.
“Atafutwe kila kona, wekeni picha zake katika vituo vyote vya televisheni duniani, sambazeni kadiri mnavyoweza mpaka kuhakikisha huyu mtu anatiwa mikononi mwa poli,” aliagiza mkurugenzi wa FBI nchini Marekani, Bwana Sandal Peters.
Mawasiliano yakafanyika kwenda nchini Ufaransa, polisi wa huko hawakujua mahali alipokuwa mtu huyo hivyo kwenda hotelini kwa ajili ya kuangalia kamera za CCTV ambazo waliamini kwamba zilimnasa mwanaume huyo.
Hilo halikuwa tatizo, wakapata picha ya mwanaume huyo, wakafuatilia kumfahamu zaidi mtu huyo, picha zake zikasambazwa kwenda sehemu nyingine, walijua kwamba mwanaume huyo alivyokuwa ameingia nchini Ufaransa alipitia sehemu katika bandari au uwanja wa ndege hivyo kwenda huko.
Walitafuta kila kona, walichukua picha za wasafiri wote waliokuwa wameingia katika sehemu hizo lakini hawakufanikiwa kuipata picha yake. Walipohamia kwa watu walioingia humo kwa ndege binafsi wakafanikiwa kuipata picha ya mwanaume huyo, maelezo yalisema kwamba aliingia ndani ya nchi hiyo kwa kutumia ndege binafsi iliyokuwa ikimilikiwa na bilionea kutoka nchini Marekani, Peter Williams.
“Is this Williams’ jet?” (hii ni ndege ya Williams) aliuliza polisi mmoja.
“Yeah! Why did he do this?” (ndiyo hii! Kwa nini amefanya hiv?) aliuliza polisi mwingine.
“We don’t know! We have to arrest him,” (hatujui! Tumkamateni) alisema polisi huyo.
Kwa msaada wa interpool, Bwana Williams akakamatwa, akawa mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ya mauaji yaliyotokea nchini Ufaransa. Na kwa sababu alikuwa amemsafirisha mtu aliyehusika katika ugaidi, akapewa kesi hiyo nyingine kwa kuwadhamini magaidi kulipua kituo cha treni cha Pennslyvania.
“Simfahamu kijana huyo,” alisema Williams wakati akiwa katika chumba cha mahojiano.
“Na alifikaje ndani ya ndege yako? Nani alimtafutia vibali? Kwa nini aliingia nchini Ufaransa kwa ndege yako na kuondoka kwa ndege yako?” yalikuwa maswali kadhaa ambayo alishindwa kuyajibu. Kila mtu akajua kwamba alihusika katika mauaji ya Bilionea Belleck lakini pia alihusika katika tukio la kigaidi lililotokea hapo Pennslyvania.
****
Fareed alikuwa akilia, maumivu ya tumbo yaliongezeka, alijua kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wake. Siku hiyo hakula kitu, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea tumboni mwake. Mawazo yake yakamwambia kwamba yale matunda aliyokuwa akila ndiyo yaliyomsababishia hali ile.
Siku hiyo ilipita huku akiwa kwenye maumivu makali, aliumia kupita kawaida. Usiku hakulala, alikesha akilia kwa maumivu makali, aliendelea kukohoa na kutoa madonge ya damu.
Ilipofika majira ya saa tano asubuhi ndipo kwa mbali akaiona meli moja kubwa ikielekea kule alipokuwa. Hakuwa na nguvu za kutosha lakini akasimama na kuanza kupunga mikono yake juu huku akijitahidi kutoa sauti ili asaidiwe pale alipokuwa.
Hiyo ilionekana kuwa nafasi pekee ya yeye kuondoka kisiwani pale. Meli ile ikaendelea kusogea, kwa mbali akawaona watu kutoka kwenye meli ileile wakipunga mikono kuashiria kwamba walimuona.
Vijana wawili wakafungua mtumbwi uliokuwa katika meli yao na kisha kupanda, hapohapo wakaanza kuelekea kule alipokuwa Fareed kisiwani ambapo baada ya kumfikia, wakaanza kumuuliza maswali kadhaa kuhusu sababu iliyomfanya kuwa mahali pale.
“Tumbo linauma…” alilalamika Fareed huku akilishika tumbo lake, hata maswali aliyoulizwa akashindwa kuyajibu kabisa.
Wakamchukua na kumpakiza ndani ya mtumbwi na kuelekea naye kwenye meli ile. Alikuwa akiugulia kwa maumivu makali, wakati mwingine aliwaambia watu hao kwamba alikuwa akifa na kitu kilichomuuma zaidi ni kwamba alikuwa akifa hata kabla hajamuua padri Luke ambaye alimbaka badala ya kumuongoza sala ya toba alipokwenda kuungama kwenye kanisa lake.
Hiyo ilikuwa meli kubwa ya wavuvi waliokuwa wakivua samaki katika eneo la kimataifa, walitokea nchini Marekani na miaka mingi kazi yao ilikuwa hiyo, walishinda kwenye meli na ni mara chache sana walikuwa wakitoka na kwenda kuzurura sehemu mbalimbali.
Hawakujua kitu chochote kuhusu Fareed, wakati dunia ikimtafuta kwa mauaji aliyokuwa ameyafanya, wao hawakuwa na habari hata kidogo. Walimkaribisha katika meli yao, wakampa dawa ya tumbo na kuondoka naye.
Kidogo dawa hiyo ikampunguzia maumivu makali. Wakati meli ikiendelea kuvua kama kawaida, alichokuwa akikifikiria ni kutoroka mara baada ya meli kufika nchi kavu.
Fareed akapata nafuu, akawa muongeaji mkubwa, alitaka kuwazoea watu hao ili wasiwe na maswali mengi. Alipoulizwa kuhusu sababu iliyomfanya kuwa mahali pale, hakutaka kuwaambia ukweli, aliwadanganya kwa kuwaambia kwamba alikuwa akisafiri kwa meli na wezake, ghafla bahari ikachafuka, meli ikapasuka na maji kuingia, kilichoendelea ni meli hiyo kuzama.
Ilikuwa rahisi kumwamini kwa kila kitu alichokuwa akikiongea, alizungumza huku akionekana kumaanisha kile alichokuwa akikisema mbele yao. Sura yake ilivyokuwa, ilifanana na maneno aliyokuwa akizungumza hivyo kumwamini kwa asilimia mia moja.
Zoezi hilo la uvuaji liliendelea kwa siku kadhaa na ndipo wakarudi nchi kavu tayari kwa kuuza samaki wao waliokuwa wamewavua katika kipindi walichokuwemo huko.
Japokuwa walimzoea Fareed na waliahidi kumsaidia lakini baada ya meli kufika nchi kavu walishangaa kuona mtu huyo akiwa amewapotea katika mazingira ya kutatanisha. Hawakujua alikuwa wapi, walijaribu kumtafuta kila kona, mwanaume huyo hakuwepo kitu kilichowapa maswali mengi yasiyo na majibu.
Fareed alikuwa njiani akielekea kulipokuwa na mgahawa wa McDonald, alikuwa akitaka kula, kwa kiasi cha pesa alichokuwa nacho mfukoni mwake aliamini kingemsaidia.
Wakati akiwa kwenye mgahawa huo, akiwa ameagiza chakula ndipo macho yake yakatua katika televisheni ambapo kulikuwa na habari iliyokuwa ikizungumzia kuhusu kukamatwa kwa Bilionea Williams.
Alishangaa, alipoangalia sababu ya kukamatwa huko akaona ni kwamba alikuwa akihusika kushirikiana na magaidi katika kulipua kituo cha treni huko Pennsylvannia na pia alihusika kumtuma mtu kwenda kuwaua mabilionea wawili kwa kumtumia mtu aliyeonekana kwenye picha.
Fareed alipoangalia picha ile, alikuwa yeye, alionekana vilivyo alivyokuwa ameingia kwenye piramidi kwenda kumuua Bilionea Keith, alipoingia hotelini kumuua bilionea Bellck mpaka pale alipokuwa akikimbia katika kituo hicho cha treni.
Sura yake ikaanza kuwa maarufu, hapo mgahawani hakutaka kukaa sana, akasimama, akalipia na kisha kuondoka. Alijua fika kwamba ilikuwa ni lazima kukamatwa, hakutaka kuona akikamatwa pasipo kumuuua Padri Luke aliyekuwa amembaka, alitaka kumaliza kila kitu ili pale atakapokuja kukamatwa na kushtakiwa kifo basi afe akiwa na amani moyoni mwake.
“Ni lazima niende kanisani!” alisema Fareed.
Hakutaka kubaki mahali hapo, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kwenda katika kanisa hilo lililokuwa umbali wa kilometa mbili kutoka hapo alipokuwa. Akakodi teksi ambayo ikaanza kumpeleka huko.
Macho yake yalikuwa chini, aliogopa kuonekana na kugundulika, na hata alipokuwa ameongea na dereva wa teksi hiyo alikiinamisha kichwa chake chini.
Safari iliendelea mpaka alipofika kwenye kanisa hilo, akaingia. Kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma ndivyo ilivyokuwa kipindi hicho, kulikuwa na watu wachache sana kanisani humo, akaelekea mpaka katika sehemu ya kuungamia dhambi na kukaa tayari kwa kuzungumza na padri huyo ambaye ndani ya dakika chache, akaingia humo.
“Nimekuja kuungama dhambi zangu,” alisema Fareed huku akiangalia chini.
Padri Luke hakumgundua kwani alikuwa amebadilika, hakuwa kama vile alivyokuwa kipindi cha nyuma. Alizungumza naye kwa kirefu na kumwambia kwamba angerudi baadaye kwa ajili ya kuzungumza naye.

 ITAENDELEA KESHO

Comments are closed.