The House of Favourite Newspapers

Michirizi Ya Damu – 17

ILIPOISHIA:

“Sasa kazi itafanyika,” alimwambia Williams kwenye simu.

“Ukikamilisha

! Nakuahidi kukupa dola milioni kumi. Huyu mpumbavu ananinyima sana usingizi,” alisema William huku akiwa na uhakika kwamba ilikuwa ni lazima mwanaume huyo ammalize Bilionea Belleck. Ila la zaidi, alitaka kuona bilionea huyo akifa na yeye kumuua Fareed kwani kama angemuacha, siri ingeweza kuvuja. Ili siri itunzwe ilikuwa ni lazima hata naye Fareed afe.

Fareed hakujua mahali mwanaume huyo alipokuwa, ila aliambiwa kwamba angepewa maelezo yote kwani yale aliyopewa mara ya kwanza, yalibadilika kwani mtu huyo aliondoka Paris na hakukuwa na aliyejua kama alikwenda Monaco au Marseille.

Baada ya dakika hamsini akapigiwa simu na kuambiwa kwamba mwanaume huyo hakuwa hapo Paris bali alikuwa jijini Marseille katika Hoteli ya Melkizedeki ambapo alikuwa akilala huku kila siku akishiriki katika kikao cha matajiri.

Hilo halikuwa tatizo, haraka sana akaondoka hotelini alipokuwa, akachukua ndege na kuelekea Marseille ambapo ndipo aliambiwa mwanaume huyo alipokuwa. Njiani, alikuwa akimuomba Mungu afike salama kwani alikuwa na hasira kali, asingeweza kumuacha mwanaume huyo akaishi kwani alikuwa miongoni mwa watu waliotaka kumuua kwa nguvu zote.

Walichukua dakika arobaini na tano tu mpaka kufika jiji humo ambapo akateremka na kuchukuliwa kwa gari mpaka katika hoteli moja na kutulia huko. Ilipofika saa mbili usiku, wanaume wawili wakafika hotelini hapo na kuomba kuzungumza naye.

Hilo halikuwa tatizo, alipewa taarifa na Williams kwamba watu hao wangefika mahali hapo, na wao ndiyo ambao wangemwambia kuhusu Belleck ambaye hakujua alikuwa katika hoteli gani.

“Belleck yupo anakula raha, hivi tunavyoongea, keshokutwa anaondoka kurudi Marekani,” alisema mwanaume mmoja aliyejitambulisha kwa jina la De Leux.

“Sawa. Kingine?”

“Huwa anapenda sana kununua malaya mitaani! Tunajua sehemu ambayo hupenda kununua na pia tunajua hoteli anayokaa mpaka chumba alichokuwepo,” alisema De Leux.

“Haina shida! Ningependa nikutane naye na kufanya kazi yangu,” alisema Fareed.

Hakwenda huko kufanya jambo lolote zaidi ya kumuua bilionea huyo na kuondoka zake. Wanaume hao wawili ndiyo walikuwa wachora ramani wakubwa, walikuwa wakienda hotelini hapo, wanaonana na wahudumu wa hapo, wakatengeneza urafiki wa kizushi kwa ajili ya kuwasaidia hapo baadaye.

Hawakujua kama lengo la watu hao ni kumpata mwanaume aliyekuwa ndani ya hoteli hiyo. Wakati mwingine walikuwa wakikaa mapokezini, Belleck alipokuwa akiingia ndani ya hoteli ile na machangudoa walikuwa wakimuona hivyo kuwa kazi nyepesi kwao kufanya kile walichokuwa wakikitaka.

“Cha kwanza ni kupata kadi ya kufungua vyumba vyote,” alisema De Leux.

Hilo ndilo lililotakiwa, kwa kutumia uzoefu mkubwa wa kuzungumza waliokuwa nao, wakajenga ukaribu zaidi na mhudumu aliyeitwa kwa jina la Natalie ambaye bila tatizo lolote lile, naye akaukaribisha ukaribu huo na mwisho wa siku De Leux kumtongoza.

“Acha masihara wewe! Mzuri mimi?” aliuliza Natalie huku akitabasamu, japokuwa alipinga kwamba hakuwa mzuri lakini sifa zile zilimfurahisha.

“Wewe ni mzuri sana. Una tabasamu pana, msichana mrembo sana! Umeumbinka kama Mona Liza,” alisema De Leux huku akimwangalia Natalie kwa macho ya nipe nikupe.

Akamsifia usiku mzima, msichana huyo akachanganyikiwa, kila wakati akawa anapandisha juu mpaka katika chumba alichokuwa akilala De Leux na kuingia ndani. Hakutaka kufanya mapenzi na msichana huyo, kitu muhimu kilikuwa ni kuweka ukaribu na mwisho wa siku kuichukua kadi ambayo alikuwa akiitaka mno.

Wakati walipokwenda kuonana na Fareed, walimwambia kabisa kile kilichokuwa kimetokea kwamba kulikuwa na kadi moja muhimu ambayo ingewawezesha wao kuingia ndani ya chumba chochote kile.

Fareed akafurahi kwani urahisi huo ndiyo aliokuwa akiutaka kwa hali na mali. Siku hiyo wakaondoka na kwenda katika hoteli hiyo. Wakachukua chumba kwa ajili ya Fareed ambaye akaingia bila tatizo na uzembe mkubwa ambao waliufanya wahudumu wa hoteli hiyo ni kutokuishikilia passport yake.

Akaingia mpaka chumbani, akajipumzisha na kuambiwa kwamba mtu aliyetakiwa kumuua alikuwa njiani kufika mahali hapo hivyo alitakiwa kusubiri.

De Leux na mwenzake wakarudi mapokezi, wakatulia kochini. Ilipofika saa sita usiku, wakamuona Belleck akirudi hotelini hapo huku akiwa na mwanamke ambaye alivalia hijabu ila kwa nyuma alijazia hasa kiasi kwamba hata wao walipokuwa wakimwangalia walimtamani kupita kawaida.

“Huyo hapo! Subiri!” alisema De Leux.

Wakati mwanaume huyo akiingia ndani na mwanamke huyo, De Leux akamuita Natalie na kuanza kuongea naye. Alimwambia wazi kwamba siku hiyo alitaka kukaa naye na kuzungumza naye mambo mengi lakini iwe baada ya kufanya usafi katika vyumba mbalimbali.

“Haina shida mpenzi! Nitakuja,” alisema Natalie huku akionekana kuwa na furaha tele.

De Leux akaondoka na mwenzake mpaka chumbani kwake, wakakaa huko na kuyapanga kwamba siku hiyo ndiyo ilikuwa mwisho wa mtu huyo ambaye alikuwa adui wa bosi wao kwa kipindi kirefu.

Wakamfuata Fareed na kumwambia kilichokuwa kikiendelea kwamba ni yeye tu ndiye aliyekuwa akisubiriwa kufanya mauaji hayo.

“Haina tatizo!”

“Sawa. Ngoja nimuite huyu msichana alete kadi,” alisema De Leux na hapohapo kuchukua simu ya mezani na kupiga mapokezi ambapo alimtaka Natalie aende huko kuchukua shuka kwenda kulifua.

Msichana huyo hakuchelea, baada ya dakika kadhaa, akawa ndani ya chumba hicho. Alijua fika kwamba hakuitwa kwa ajili ya kubadilisha shuka bali aliitwa kwa sababu kulikuwa na kitu kingine.

Alivaa kimitego na hata alipoingia ndani ya chumba hicho, kitu cha kwanza kabisa ni kuipandisha sketi yake kwa juu, upaja wake ukaonekana, kidogo De Leux akatetemeka.

“Mmh! Leo hatoki!” alijisemea huku akimwangalia msichana huyo kwa matamanio makubwa. Ila akili yake haikuhama kutoka kwenye kadi ile. Ilikuwa ni lazima aipate na kumpelekea Fareed ambaye angefanya kazi hiyo aliyokuwa ameifuata nchini Ufaransa.

****

Huo ndiyo ulikuwa muda wa kukamilisha alichokuwa akikitaka. Alimwangalia Natalie kwa macho yaliyomaanisha kwamba alimtaka sana kitandani hapo. Msichana huyo pasipo kugundua kwamba kila kitu kilichofanyika kilikuwa ni maigizo, akaanza kumfuata mwanaume huyo.

Hatua zake zilikuwa za taratibu, za mahaba zilizoashiria kwamba alimuhitaji sana De Leux, mwanaume huyo akasimama na kumsogelea, alipomfikia, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuuwahi mdomo wake na kuanza kubadilishana mate.

Zoezi hilo liliambatanisha na kushikana hapa na pale. Wakati yote yakiendelea, akili ya De Leux ilikuwa kwenye kadi aliyokuwa nayo msichana huyo, hakutaka kupoteza lengo lake kwani aliamini kwamba kama asingefanikisha suala hilo muda huo basi kazi waliyokuwa wakiitaka isingeweza kufanyika.

Wakapelekana mpaka kitandani, wakavuana nguo na kuendelea na zoezi lao. Miguno ya kimahaba ilikuwa ikisikika kila kona na baada ya muda fulani, sauti zile ziliongezeka zaidi.

Kulikuwa na mwanga hafifu, Natalie alichanganyikiwa, muda wote wakati mwanaume huyo alipokuwa juu yake, aliyafumba macho yake, hisia za raha zilikwenda mpaka kwenye ubongo wake, zikamchanganya kiasi kwamba akaona hakukuwa na kitu kilichokuwa na raha duniani kama hicho kilichokuwa kikiendelea kitandani hapo.

De Leux akachukua nafasi hiyohiyo kupekua katika mifuko ya msichana huyo, alichokuwa akikitaka ni kadi iliyokuwa na uwezo wa kufungua milango yote, hilo wala halikuwa zoezi gumu kwani ndani ya sekunde chache, tayari alikuwa na kadi hiyo mkononi mwake.

Akaificha kwenye mfuko wa suruali yake, alipomaliza kufanya mapenzi na msichana huyo, wakabaki wamelala huku wakivuta raundi ya pili iendelee. Muda wote Natalie alikuwa akifikiria ngono, kilipita kipindi kirefu pasipo kufanya mchezo huo na ndiyo maana alipoambiwa aende chumbani kwa mwanaume huyo, hakutaka kujiuliza, haraka sana akaenda tena huku akiwa amejiandaa kikamilifu.

“Una pumzi sana,” alisema natalie huku akiupeleka mkono wake chini ya kiuno cha De Leux.

“Kweli?”
“Yeah! Sijawahi kukutana na mwanaume mwenye pumzi kama wewe. Halafu unajua, kuna wakati nilihisi kama unataka kunivunja kwa jinsi ulivyokuwa ukinikunja,” alisema msichana huyo huku mkono ule ukiwa kulekule.

“Pole sana jamani! Ila nataka tuendelee!”
“Wewe tu! Mimi nipo tayari!” alisema De Leux.

Hata kabla hawajaendelea, De Leux akasimama na kumwambia Natalie kwamba alitaka kwenda kumuona rafiki yake kwamba ikiwezekana asimpigie simu asubuhi sana kwani ilikuwa ni lazima alale na msichana huyo ambaye kwa siku inayofuatia ilikuwa ni ya mapumziko kwake.

Hilo halikuwa na tatizo, akaruhusiwa na kuondoka huku akiwa na kadi ile mkononi. Alipofika katika chumba cha rafiki yake, akagonga mlango, ulipofunguliwa, akampa kadi na kumwambia ampe Fareed ambaye alitakiwa kukamilisha kazi ya mauaji na kuondoka hotelini hapo.

Hilo halikuwa tatizo, kadi ikachukuliwa, De Leux akarudi chumbani kwake kuendelea kufanya mapenzi na msichana huyo. Huku nyuma, rafiki yake akampelekea kadi ile Fareed ambaye aliichukua na kuufuata mlango wa chumba kile.

Fareed hakuwa mikono mitupu, alikuwa na kisu pamoja na dawa kali ya usingizi ya Microphenon ambayo ilikuwa ikitumika sana katika vyumba vya upasuaji. Alipoulikia mlango ule, akaingiza kadi, mlango ukafunguka, akaingia ndani.

Belleck na mpenzi wake walikuwa wamelala, kabla ya kufanya chochote, akaanza kupulizia dawa ile ya usingizi ambapo baada ya kuwaingia wote wawili, wakapitiwa na usingizi mzito, tofauti na ule waliokuwa nao.

Kwa haraka sana Fareed akamfuata Belleck pale alipokuwa, akamshusha na kumuweka sakafuni, akanza kumchomachoma visu vya tumbo. Damu zilitoka lakini hakujali, alichoma mara kadhaa, akauacha mwili wa mwanaume huyo chini na kuuburuza kidogo hali iliyoifanya damu ile kutengeneza michizrizi sakafuni pale.

Hakutaka kuondoka hivihivi, akachukua kalamu na karatasi kisha kuandika maneno mafupi yaliyosomeka C’est fait yakiwa na maana ya kukamilika kwa jambo au ‘done’ kwa Lugha ya Kiingereza.

Fareed hakutaka kubaki ndani ya chumba hicho, kwa haraka sana akatoka na kuelekea chumbani kwa rafiki yake, De Leux ambapo akampa ile kadi na yeye kuichukua na kumpeleka mwanaume huyo ambaye bado alikuwa akiserebuka na msichana yule chumbani kwake.

Alipopiga hodi tu, De Leux akafungua mlango, akapewa kadi ile na kisha kurudi kitandani. Mpaka mambo hayo yote yanafanyika, Natalie hakujua kitu chochote kile, alichukulia kawaida, hakujua kama mwanaume huyo alichukua kadi na kwenda kufanya mauaji ndani ya chumba kimoja humo.

Williams akapewa taarifa kwamba kila kitu kilichotakiwa kufanyika, kilifanyika. Moyo wake ulikuwa na furaha kwani hakukuwa na mtu aliyekuwa akimchukia kipindi hicho kama alivyokuwa Belleck. Akampa pongezi zake, hakutaka kuchelewa, kwa kuwa alimuaidi kumpa kiasi cha dola milioni kumi, haraka sana akamuhamishia kiasi hicho mpaka kwenye akaunti yake kwa mategemeo kwamba kama atamuua basi kiasi kile kingeweza kuchukuliwa kirahisi ndani ya saa arobaini na nane.

Ilipofika asubuhi, hawakutaka kuendelea kukaa ndani ya hoteli hiyo, muda wao ulikuwa umefika na hivyo wote kuondoka hotelini humo. Safari yao ilikuwa ni uwanja wa ndege, tayari rubani alikuwa ameandaliwa na alikuwa na taarifa kwamba ilikuwa ni lazima warudi kuelekea nchini Marekani.

Walipofika uwanja wa ndege, wakapanda ndege na safari ya kurudi nchini Marekani ikianza. Huko, Williams akamtumia ujumbe mfupi De Leux kwamba Fareed hakutakiwa kufika nchini Marekani salama, ilikuwa ni lazima auawe njiani na kutupwa katika Bahari ya Atlantiki kitu ambacho kwa mwanaume huyo, jinsi alivyokuwa na ubavu, hilo halikuwa na tatizo lolote lile.

“No problem,” (hakuna tatizo) alijibu De Leux huku akiachia tabasamu. Wakati huo ndege ilikuwa njiani, ndiyo kwanza ilikuwa ikielekea katika anga ya bahari hiyo ambapo mauaji yalitakiwa kufanyika ndani ya ndege. Alichokifanya ni kuwaambia wenzake kwamba piga ua mwanaume huyo alitakiwa kuuawa ili kuficha siri.

****

Hali ya hewa ilibadilika ghafla, mawingu mazito yakaanza kujikusanya angani kumaanisha kwamba mvua kubwa ingenyesha muda mfupi ujao. Kila mtu alikuwa na hofu kwamba mvua ya siku hiyo ingekuwa kubwa kuliko zote ambazo ziliwahi kutokea nchini Ufaransa.

Watu wa idara ya hali ya hewa nchini Ufaransa walitoa angalizo kabla kwamba siku hiyo mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali ingeweza kunyesha hivyo watu wote walitakiwa kujiandaa.

Miungurumo ya radi ilikuwa ikisikika kila kona, watu wengi waliogopa na kujifungia ndani. Kabla ya mvua hiyo kuanza kunyesha, upepo mkali ukaanza kuvuma. Ulikuwa mkubwa uliosababisha maafa makubwa kiasi kwamba wengine wakasema kwamba upepo kama huo mara ya mwisho ulivuma mwaka 1956 ambapo uliacha madhara makubwa kwa watu kufa na mali nyingi kuharibiwa.

Watu wengi waliogopa, katika viwanja vya ndege, hazikuruhusiwa kupaa kwani hali ilitisha sana na hata kwa ndege ambazo ziliondoka, kila mmoja alikuwa na hofu kwamba zingeweza kuanguka na kulipuka.

Miongoni mwa ndege zilizoondoka ilikuwa ile ndogo binafsi aliyokuwa Fareed na wenzake. Walipanga kumuua ndani ya ndege lakini kabla ya kufanya kile walichoambiwa wakifanye, ndege ikaanza kuyumba huku na kule.

Upepo ulikuwa mkali mno, rubani aliyekuwa akiiendesha ndege ile alichanganyikiwa, alijitahidi sana kuiweka sawa lakini ilishindikana kabisa. Ilikuwa katika usawa wa bahari, upepo mkali uliendelea kuvuma huku mawingu yakiwa yametanda kila kona. Wote wakajua kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wao na hivyo ilikuwa ni lazima wajiokoe.

“Tunakufa…” alisema De Leux huku akionekana kuchanganyikiwa, hata wazo la kumuua Fareed likapotea.

Akaanza kuelekea mpaka kule alipokuwa rubani, akamuuliza juu ya hali iliyokuwa ikiendelea, akamwambia kwamba walikuwa usawa wa bahari, mita mia moja na ilikuwa ngumu kurudi kwani yeye mwenyewe alishindwa kabisa kuiweka sawa ndege hiyo.

“Kwa hiyo?”

“Hatujui tufanye nini! Tusalini sala zetu za mwisho!” alisema rubani, hakuona kama wangeweza kupona kutokana na hali iliyokuwa ikiendelea mahali hapo.

Hakukuwa na mtu aliyejiona kuwa salama, kila mmoja aliona kuwa huo ndiyo ungekuwa mwisho wake. Wakachukua maparachuti yaliyokuwa katika viti vyao kwa ajili ya kurukia baharini ambapo kulionekana kuwa salama kwa maisha yao.

Nje, hakukuwa na mwanga wa kutosha, mawingi mazito yalitanda na upepo mkali uliendelea kuvuma kama kawaida. Chini, hawakuona kitu kwani mawingu yale yalianza kushuka chini kutokana na upepo huo uliokuwa ukiendelea kuvuma kama kawaida.

“Let’s jump,” (turuke) alisema De Leux huku akimwangalia mwenzake, tayari maparachuti yalikuwa migongoni mwao.

“What about me?” (na mimi je?) aliuliza Fareed.

Hawakumjibu kitu chochote zaidi ya kumwangalia. Wakaufungua mlango wa ndege na kutokana na upepo mkali uliokuwa ukiendelea kuvuma, hali ikawa mbaya zaidi, ndege ikayumbishwa kupita kawaida, De Leux na mwenzake wakaruka na maparachuti yale kuelekea chini huku wakimwacha Fareed akiwa na rubani wa ndege ile.

Alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, alitamani kuruka lakini alishindwa kufanya hivyo. Haraka sana akamfuata rubani na kuanza kuzungumza naye, alimwambia kwamba lengo lake lilikuwa ni kuruka kwani vinginevyo ndege ile ingepata ajali na kufa humo.

Akamtaka kushusha ndege, kutoka kwenye umbali wa mita mia moja mpaka hamsini ili aweze kujirusha baharini. Kwanza rubani akaogopa, aliijua bahari hiyo, ilikuwa hatari kuliko bahari nyingine kwani baridi lililokuwa likipiga humo, lilikuwa kubwa na ndiyo bahari ileile iliyoua watu katika meli ya Titanic miaka hiyo ya nyuma.

“It’s impossible! You can’t jump,” (haiwezekani! Huwezi kuruka) alisema rubani yule huku akimwangalia Fareed.

Fareed hakutaka kuelewa, alichokitaka kilikuwa ni kuyaokoa maisha yake kutoka katika ndege ile. Alimwangalia rubani, aliangalia mbele ya ndege ile, ni kweli kulikuwa na upepo mkali na mawingu mazito yalitanda kiasi kwamba ilikuwa vigumu sana kuona mbele.

Aliendelea kumwambia rubani yule ashushe ndege kwa kiasi fulani ili aweze kuruka. Baada ya kubembelezwa sana hatimaye rubani huyo akaishusha ndege hiyo kwa umbali wa mita hamsini kisha kumruhusu Fraeed kuruka.

“Una parachuti?” aliuliza rubani.

“Hapana!”
“Boya!”
“Hapana!”
“Hebu subiri!” alisema rubani huyo. ITAENDELEA KESHO

Comments are closed.