The House of Favourite Newspapers

MIFUKO YA PLASTIKI YAANDIKA HISTORIA!

DAR ES SALAAM: Katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki nchini limeanza kutekelezwa Jumamosi iliyopita nchi nzima na tayari jijini Dar es Salaam mifuko hiyo haikuonekana popote, hali ambayo inaelezwa kuwa amri hiyo imeandika historia. 

 

Uchunguzi wa Gazeti la Uwazi ulibaini kwamba, sheria hiyo imeandika historia kwa sababu imepokelewa na wakazi wa jiji hilo kwa mikono miwili, huku wengi wakiungana na Serikali kuwa walinzi wa utekelezaji wa sheria hiyo. Mwongozo kwa wakaguzi na watekelezaji wa katazo la mifuko hiyo, unaelekeza kuwa ukaguzi utafanyika madukani, magengeni, sokoni, katika maduka makubwa, ghalani, viwandani na kwenye maeneo mengine zinakouzwa bidhaa.

“Wakati wowote wa ukaguzi, wakaguzi wajitambulishe na kuonesha vitambulisho vyao kwa wahusika kwenye maeneo wanayoyakagua, hairuhusiwi kumsimamisha mtu na kumpekua au kupekua mizigo yake ili kutafuta mifuko ya plastiki,” inaeleza sehemu ya mwongozo huo na uchunguzi umeonesha hakuna watu waliopekuliwa.

 

Pia hairuhusiwi kuingia kwenye makazi ya watu au kusimamisha magari au vyombo vingine vya usafiri ili kutafuta mifuko ya plastiki, iwapo vitasimamishwa kwa sababu nyinginezo na kukutwa na mifuko hiyo, adhabu stahiki itatolewa kwa wahusika na wataelekezwa mahali pa kupeleka shehena hiyo.

 

Atakayekutwa na kosa la kuendelea kuuza, kuhifadhi na kutumia mifuko hiyo ataelekezwa pa kuipeleka, atapigwa faini na atasainishwa fomu kukubali faini hiyo na atapewa muda wa kulipa. “Atakapokataa kusaini au kushindwa kulipa katika muda aliopewa ndipo atafunguliwa mashtaka. Watakaotozwa na kulipa faini watapewa risiti za Serikali kwa malipo yao,” unaeleza mwongozo huo.

Jijini Dar es Salaam, Uwazi lilitembelea katika masoko ya Afrika-Sana, Kariakoo, Mchikichini, Buguruni na Mbagala Rangi-Tatu ambalo ni maarufu kwa kuuza nguo, viatu vya mtumba na vyakula na kushuhudia wafanyabiashara na watu waliokwenda kutafuta bidhaa katika masoko hayo wakiwa na mifuko mbadala.

 

Wamachinga ambao mara nyingi walikuwa wakitembeza mifuko ya plastiki, juzi na jana walionekana wakiuza mifuko mbadala kila kona ya jiji. Mwenyekiti wa Soko la Afrika- Sana, Adam Lugano Kapola Mwasele alipohojiwa na Gazeti la Uwazi alisema; “Tunazingatia, na kutekeleza maelekezo yanayotolewa na Serikali na tayari tumeshatoa elimu kwa wafanyabiashara wa soko letu na zoezi linakwenda vizuri.”

Wafanyabiashara kadhaa waliozungumza na Uwazi walisema tatizo kubwa wanalokabiliana nalo ni kupanda kwa bei za bidhaa kwa kile walichodai kuwa mifuko mbadala imeongeza bei kwani inauzwa bei ghali. Uchunguzi wa Uwazi ulibaini mifuko mbadala inauzwa kati ya Sh 200 hadi 2,500 kutegemeana na ukubwa wa mfuko husika.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Januari Makamba juzi alitembelea sehemu mbalimbali za Jiji la Dar na akiwa Mbagala alisema ameridhishwa na utekelezaji wa sheria hiyo bila shuruti na hivyo katazo hilo limeandika historia.

Hata hivyo, Makamba alisema zuio hilo la matumizi ya mifuko ya plastiki halitahusisha mifuko ile inayotumika kukusanyia taka katika ndoo za takataka maarufu kwa Kingereza kama trash bags. Zaidi kuhusiana na sheria itakayokubana ukikamatwa na mfuko wa plastiki soma ukurasa wa pili.

 

WAZIRI MKUU Ashtukia Mchezo wa Maafisa Tarafa” Rudisheni Siku ya Usafi”

Comments are closed.