The House of Favourite Newspapers

Migogoro vyuo vikuu ishughulikiwe mapema isingoje vurugu

0

ndalichako

Nichukue nafasi hii kumshukuru Mungu kwa kutupa uhai leo na kutuwezesha kuwasiliana kupitia kona hii.

Nianze kwa kusema kwamba wiki iliyopita taifa lilishuhudia migomo miwili, mmoja ukihusisha walimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na ukasababisha kutimuliwa kwa wanachuo na mwingine ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo wanafunzi walikuwa wakidai fedha za kujikimu kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Upo umuhimu wa kuzuia mambo kama haya kwani imeelezwa kuwa hatua ya wanafunzi wa UDSM kugoma ilitokana na taarifa zisizoeleweka za HESLB juu ya lini fedha zao za mikopo zitatolewa ikielezwa kwamba kwa kawaida fedha za chakula huingizwa kila baada ya siku 60 na kwamba karibu wiki mbili zilikuwa zimeshapita pasipo fedha hizo kulipwa kwa wanafunzi.

Inawezekana wanafunzi baada ya kuona longolongo hiyo na kujua kwamba Rais Dk. John Magufuli atatembelea chuoni hapo kuzindua jengo la maktaba, wakaamua kugoma ili kiongozi huyo wa nchi ajue kinachoendelea.

Kinachosikitisha ni kwamba mgomo huo wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar umetokea huku kukiwa na hali ya hewa mbaya katika Chuo Kikuu cha Dodoma baada ya wanafunzi 7802 waliokuwa wakisomea Diploma Maalum ya Elimu, Sayansi, Hisabati na Tehama wakirudishwa majumbani mwao.

Ilelezwa kuwa diploma hiyo ilikuwa ni mkakati mahususi wa serikali wa kupunguza tatizo la walimu wa sayansi katika shule za sekondari nchini. Kutimuliwa kwa wanafunzi hao kulileta taharuki kubwa katika Mji wa Dodoma na hata ndani ya Bunge kiasi cha kuathiri shughuli za chombo hicho cha wawakilishi wa wananchi ambacho kinaendelea na mikutano yake ya Bajeti ya Taifa.

Ninachotaka kusema hapa ni kwamba kufukuzwa kwa wanafunzi siyo jambo geni katika nchi yetu ingawa safari hii kwa hawa wa UDOM ni tofauti kwani hawakugoma wala kufanya kosa lolote kwani kuna sababu zimetolewa hasa hii ya walimu wao kugoma, hivyo wao kukosa elimu.

Hapa kuna tatizo; kwamba serikali badala ya kushughulikia tatizo la walimu wao, imeshughulikia wanafunzi na matokeo yake jambo hilo limetikisa nchi wakati lingeweza kumalizwa kwa majadiliano na pande husika badala yake limesababisha adha kubwa kwa wanafunzi na kuwafanya wabunge kuja juu hata kusababisha Bunge kuahirisha shughuli zake siku moja wiki iliyopita.

Ukweli ni kwamba mambo haya yanatafsirika kuwa kuna wanaopewa dhamana ya kusimamia ustawi wa maeneo yao lakini wanashindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo na kusababisha malalamiko na mitafaruku isiyo na tija kwa taifa.

Nasema hivyo kwa sababu hili la stahili za wanafunzi siyo jambo la dharura kwa sababu kuna utaratibu uliowekwa ambao unapaswa kufuatawa, sasa kwa nini haukufuatawa? Kama kulikuwa na tatizo kwa niniĀ  walengwa hawakuarifiwa?

Wakati umefika kwa serikali kupita Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako kuhakikisha haya matatizo ya vyuo vikuu yanatatuliwa mapema kuliko kusubiri migogoro.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave A Reply