The House of Favourite Newspapers

Mimba kutunga nje ya mfuko wa uzazi-4

1

MSOMAJI baada ya kuangalia dalili za tatizo hili la mimba kutunga nje ya mfumo wa uzazi ni vema tukajua njia za kugundua tatizo hili na njia za kuliepuka.

Ugunduzi wa Ectopic Pregnancy

Mimba iliyotungwa nje ya kizazi huweza kugunduliwa kwa;

Daktari kusikiliza historia ya mgonjwa na kufahamu dalili zake na kumfanyia uchunguzi wa mwili (Physical Examination).

 Kufanya vipimo kadhaa vinavyoonesha kuwepo kwa tatizo hilo. Vipimo hivyo ni pamoja na kupima damu kwa ajili ya kuangalia kiwango cha homoni ya ‘HCG’.

Kupima kiwango cha homoni ya Progesterone ambayo kwa mama mwenye Ectopic Pregnancy huwa chini (chini ya 15ng/mls), zaidi ya mwenye mimba ya kawaida.

 Ultrasound ambayo husaidia kutambua mimba ilipotungwa.

Matibabu ya Ectopic Pregnancy

Matibabu ya mimba iliyotunga nje ya kizazi yaweza kuwa ya aina mbili; yale yasiyohitaji upasuaji au yanayohitaji uangalizi na dawa na yale yanayohitaji upasuaji.

  1. Matibabu kwa kutumia dawa:

Faida kubwa ya kufanya uchunguzi mapema ni kuwa inaongeza uwezekano wa kuokoa maisha ya mama, kuokoa mirija isipasuke na hivyo kuongeza uwezekano wa kupata mimba kwa njia ya kawaida siku za usoni. Iwapo, mimba bado ni ndogo sana na kiwango cha HCG bado kipo chini mno, daktari anaweza kushauri kusubiri huku akimfuatilia mgonjwa kwa ukaribu sana. Wakati mwingine, mwili huwa na uwezo wa kuifyonza mimba changa ndani kwa ndani na hivyo kuondoa hatari ya kuwepo kwa Ectopic Pregnancy.

Hali kadhalika, mama anaweza kupewa dawa aina ya Methotrexate, ambayo ina uwezo wa kuzuia mimba kukua zaidi. Wakati dawa hii inapotolewa ni muhimu pia kufuatilia kiwango cha HCG ili kujiridhisha kuwa kimeshuka mpaka kufikia sifuri ili kuwa na uhakika mimba haipo tena.

Baadhi ya madaktari pia hutumia njia ya kuchoma dawa ya sumu ya Potassium Chloride kwenye mimba ili kuifanya isinyae na hatimaye kufyonzwa na mwili. Matibabu haya hufanyika chini ya uangalizi wa kipimo cha Ultrasound.

  1. Matibabu kwa kutumia upasuaji

Iwapo mrija tayari umepasuka, upasuaji wa dharura hufanyika kwa ajili ya kuzuia kupotea zaidi kwa damu. Sehemu ya mrija iliyopasuka huondolewa na mshipa wa damu uliopasuka hufungwa. Athari za matibabu kwa njia hii ni kuwa, huondoa uwezo wa mrija ulioathirika kupitisha yai tena maishani na hivyo kupunguza uwezekano wa mama kupata mimba siku za usoni.

Njia za kuzuia mimba kutunga nje ya kizazi

Yawezekana kupunguza uwezekano wa mimba kutunga nje ya kizazi kwa kuzuia na kujiepusha na vihatarishi vinavyosababisha hali hiyo. Njia hizo ni kama;

Kujikinga na maambukizi katika mfumo wa uzazi wa mwanamke kwa kujiepusha na ngono zembe, au kupunguza idadi ya wapenzi wa kufanya nao ngono.

Kuacha kutumia holela dawa za homoni bila kupata ushauri wa daktari.

Kujiepusha na uvutaji wa sigara

Kuna njia za kuepuka tatizo hili hivyo ni vema ukafuatilia makala haya.

Nikukumbushe kuwa Sigwa Herbal Clinic ni mabingwa wa kutatua matatizo mbalimbali katika mfumo wa uzazi wa mwanamke na mwanaume, unaweza ukawatembelea katika vituo vyao vilivyopo nchi nzima kwa maelezo na msaada usisite kupiga simu.

Itaendelea wiki ijayo.

1 Comment
  1. joseph john says

    ahsante gpl kwa elimu

Leave A Reply