The House of Favourite Newspapers

Mipango ya Mo, Okwi tishio CAF

LICHA ya mbwembwe zake na uzoefu wake, Kocha wa Mbabane Swallows ya Swaziland, Thabo ‘Koki’ Vilakati akisikia jina la Mohammed Dewji ‘Mo’ na Emmanuel Okwi wa Simba anashtuka paap!

 

Kocha huyo mzawa anayesi­fika kwa staili ya uchezaji ya 4-3-2-1 na uwezo mkubwa wa kuhamasisha, timu yake itacheza na Simba Novemba 27 jijini Dar es Salaam katika mechi ya kwanza ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Mbabane ambayo ni timu ya zamani ya Papy Tshishimbi wa Yanga na Asante Kwasi wa Simba, iliwaondoa Azam kwenye Kombe la Shirikisho msimu uliopita. Kama Simba ikiwaondoa Mbabane itaingia raundi ya kwanza kucheza na mshindi kati ya Nkana ya Zam­bia na UD Songo ya Msumbiji.

 

Thabo ambaye amekimbiwa na wachezaji kadhaa nyota waliokwenda kusaka masilahi nje, amezungumza na Cham­pioni Jumatano na kusema kwamba anajua mambo kadhaa kuhu­siana na Simba lakini tishio kubwa akataja ni ufundi wa Okwi na uwekezaji wa Mo.

 

Anasema kuwa anaelewa kuna ma­badiliko makubwa Simba am­bayo yametokana na uwekezaji wa Mo ambaye ana shauku ya mabadiliko na amefuatilia na kugundua anataka kufanya sapraizi msimu huu.

Kocha huyo ambaye yupo klabuni hapo tangu msimu wa 2016, ameweka wazi kwamba mchezaji anayemuumiza sana kichwa ni Okwi ambaye ame­kuwa kwenye fomu muda mre­fu huku akimtaja kama mche­zaji asiyekubali kushindwa.

 

Lakini akadadisi kujua nini kimemtokea au wapi alipo win­ga machachari ndani ya Simba, Shiza Kichuya kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Tunawafahamu. Tunajua nini wanafanya na kila kitu kinachoendelea kwao tumekuwa tukikifahamu.

“Tunafahamu kuwa Simba ni timu kubwa Afrika, na inatupa hofu zaidi sasa kwa kuwa ina mwekezaji bilionea Afrika, Mohammed Dewji, huyu amewekeza fedha nyingi na ni mtu maarufu sana.

 

“Tunafahamu anataka ma­fanikio makubwa kwenye timu yake, hivyo watakuja kamili sana, lakini pia Simba wanaye mmoja kati ya wachezaji mahiri Afrika Mashariki, Emmanuel Okwi, huyu kila mtu anaujua uwezo wake, hivyo lazima tuwe makini tunapocheza nao.

 

“Ila jambo moja ambalo si­jaelewa ni kwamba walikuwa na winga wao wa msimu uliopita (Shiza Kichuya) huyu alikuwa hatari sana lakini sasa haonekani, hivi yupo?” alisema kocha huyo mwenye mbwembwe nyingi.

 

Mpaka sasa kwenye ligi ya ndani, Mbabane wamecheza mechi nane na wako kwenye nafasi ya nne na pointi zao 16. Wameshapoteza mechi mbili, wakati msimu uliopita walitwaa ubingwa bila kupoteza mchezo hata mmoja zaidi ya sare tisa kwenye michezo 26 kwani ligi yao ina timu 14.

 

Kwa mujibu wa Mwenyeki­ti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Swedy Mkwabi wana­choangalia ni kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mab­ingwa tu na si vinginevyo na tayari wameanza kusaka video za Mbabane.

Ibrahim Mussa,  Dar es Salaam

Comments are closed.