The House of Favourite Newspapers

Mitandao ya Kijamii Inavyoweza Kutibua Penzi Lako! – 2

Na HASHIM AZIZ| GAZETI LA IJUMAA| LETS TALK ABOUT LOVE

WIKI iliyopita, tuliona mfano wa dada yetu Mwanahawa ambaye mpenzi wake ameamua kumuadhibu kwa kuposti picha zake za utupu, ambazo walipigana kimahaba enzi za mapenzi yao, lakini leo kwa sababu mapenzi yamefika mwisho ameamua kumdhalilisha.

Nakushukuru msomaji wangu ambaye umetumia muda wako kumshauri dada yetu huyu nini cha kufanya, naamini ushauri ataufanyia kazi kwa sababu ulikuwa ukimfikia kadiri ulivyokuwa ukiutuma. Jambo la msingi ambalo kila mmoja anapaswa kulijua ni kwamba kabla ya kuanza kuzungumzia suala la mitandao ya kijamii ni vizuri kwanza kuzungumzia suala la hifadhi au ‘privacy’ ya mtu.

Unampenda na yeye anakupenda, sawa. Unaamini hakuna kitu chochote kitakachowatenganisha kwenye huu ulimwengu, lakini kwa nini unaamua kuuweka utu wako rehani na kupiga picha zisizofaa? Yaani nini kinatokea mpaka unakubali mwenzi wako akupige picha ukiwa mtupu, au unaanzaje kumpiga picha mwenzi wako akiwa mtupu?

Nadhani kila mmoja akiwa makini kwenye suala hili, hakuna ambaye atakuja na kilio kama cha dada Mwanahawa. Wengine wanasingizia kwamba nililewa sana nikawa sijitambui. Ni ulevi wa namna gani ambao unakufanya mpaka ushindwe kujitambua?

Kama unalewa kiasi hicho, basi upo kwenye hatari ya kufanyiwa mambo mengine makubwa na mabaya zaidi ya hilo la kupigwa picha za utupu. Lazima kila mmoja, bila kujali kwamba ni mwanamke au mwanaume, ajue namna ya kujihifadhi.

Usiiamini simu yako kwa sababu inawezekana leo upo nayo, lakini kesho ukawa huna ikiwa tayari ina taarifa zako nyeti. Inawezekana simu yako au kompyuta yako ikaangukia kwenye mikono ya watu wasio na nia nzuri na wewe, matokeo yake ndiyo hayo, wengine wanafikia hata hatua za kuyakatisha maisha yao kwa sababu ya kukwepa aibu.

Kwa hiyo, pointi ya kwanza ya kuwa nayo makini, ni kutoruhusu mtu yeyote akupige picha zisizo na maadili, hata kama unampenda na kumuamini vipi kwa sababu rafiki wa leo anaweza kuwa adui wa kesho. Hata wewe mwenyewe pia, hutakiwi kujiamini kiasi cha kufikia hatua ya kujipiga picha chafu kwa sababu madhara yake ni makubwa sana.

Pili kwa wale wanaotumia mitandao ya kijamii kuumiza mioyo na hisia za wenzao, lazima utambue kwamba kufanya hivyo ni makosa kisheria yanayoweza kusababisha ukaishia pabaya. Huna sababu ya kumpiga mwenzi wako picha za utupu na hata kama unazo, huna sababu ya kuendelea kukaa nazo kwenye simu yako, zifute.

Kama shida yako ni kumuona, si unaweza kumuita na ukamuona mpaka roho yako ikaridhika? Wenzetu wanatumia mitandao ya kijamii kama jukwaa la kutangaza biashara, kupata elimu, kujadili mambo ya msingi na kufahamiana, imewaletea manufaa makubwa na kubadilisha maisha yao.

Na kwa wale ambao wamedhalilishwa au wanatishiwa kudhalilishwa, siku hizi sheria ipo wazi kabisa. Ikiwa kuna mtu ameposti picha zako za kukudhalilisha kwenye mtandao au anatishia kufanya hivyo, jambo la kwanza unalotakiwa kufanya ni kwenda kutoa ripoti kwenye kituo cha polisi na kufungua jalada.

Baada ya hapo, itakuwa ni kazi yako kufuatilia mwenendo wa kesi nzima kwa kushirikiana na polisi wa kitengo maalum cha makosa ya kimtandao na nakuhakikishia haki yako itapatikana kwa mtuhumiwa kupandishwa kizimbani na baadaye kuhukumiwa. Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

Comments are closed.