The House of Favourite Newspapers

Naibu Waziri Silinde: Mizani ya Kidigitali kuimarisha Mapato ya Wakulima Nchini

0
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo,  Mhe. David Silinde, amezindua matumizi ya Mizani za Kidigitali zilizounganishwa na Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU)  utakaoimarisha utendaji na uendeshwaji wa Vyama vya Ushirika Nchini.
Mhe. Silinde amesema sasa ni zama za Kidijitali hivyo   Vyama vyote vya Ushirika wa Mazao nchini vitumie  Mizani ya Kidijitali iliyounganishwa na Mfumo wa Upimaji wa Mazao katika kutekeleza majukumu yao.
Mhe. Silinde ameeleza hayo leo tarehe 5 Desemba, 2023 katika Wilayani Tandahimba Mkoani Mtwara alipokuwa akizindua mizani hizo na   kugawa mbegu za Mbaazi kwa wakulima wa Wilaya ya Tandahimba.
 Amesema baada ya uzinduzi ni kusimamia na kuhakikisha Viongozi na Watendaji wote wa Vyama vya Ushirika, wanasimamia matumizi sahihi ya Vipimo pamoja na matumizi ya Mizani ya Kidijitali iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo nchini.
Kwa upande wake Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amesema  Mkoa wa Mtwara una Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) 726 ambavyo  vinajishughulisha na mazao ya Korosho, Ufuta na Mbaazi pamoja na vituo vyake vya kukusanyia vipatavyo 2,236 inahitajika vituo vyote hivyo kutumia Mfumo wa Upimaji wa Mazao ya Wakulima uliounganishwa na mizani za kidijitali.
Dkt. Ndiege ameeleza kuwa, wanatarajia kusambaza kompyuta mpakato (Laptop) 726 kwa AMCOS zote zitakazofikishiwa Mizani kwa lengo la kuwezesha na kurahisisha utendaji kazi hususan katika kuwahudumia wakulima.
Amesema matarajio ya Serikali kuhusu matumizi ya Mifumo hii iliyounganishwa na Mizani ya Kidijitali, kwa kiwango kikubwa ni kuwa  itasaidia kupunguza malalamiko ya wakulima kupunjwa kilo za mazao yao  na kuwezesha upatikanaji wa taarifa na takwimu sahihi na kwa wakati.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika wa Mradi wa Pamoja wa Korosho Ltd,  Odas Mpunga, amesema mizani hizo zitasaidia kutatua changamoto kwa wakulima na amemuhakikishia Naibu Waziri kuwa watasimamia vyema na kwa uadilifu mkubwa mizani hizo kwa masilahi ya wakulima wanaowahudumia.
Leave A Reply