The House of Favourite Newspapers

Mizimu wa Mwamuziki wa Hip Hop Duniani 2PAC Kuitikisa Dunia

0
Mwamuziki wa Hip Hop duniani marehemu, Tupac Amaru Shakur ‘2Pac’.

YAPATA takriban miaka 20 sasa tangu rapa mwenye historia ndefu kwenye gemu la Muziki wa Hip Hop duniani, Tupac Amaru Shakur ‘2Pac’ afariki dunia Septemba 13, 1996 katika Hospitali ya University Medical Center Of Sourthern Nevada iliyopo huko Las Vegas, Marekani baada ya kupigwa risasi Septemba 7, mwaka huo.

2Pac alipigwa risasi wakati akitoka kwenye pambano la ngumi la Mike Tyson akiwa na meneja wake, Suge Knight ambaye alihusishwa na kifo hicho. Staa huyo wa dunia alipigwa risasi kadhaa kifuani zilizotokea kwenye gari moja lililowazuia kwa pembeni. Wengi walihusisha kifo chake na bifu alilokuwanalo na aliyekuwa mkali mwingine wa Hip Hop duniani, Christopher Wales ‘B.I.G Notorius’.

 

Kifo cha 2Pac hakikumuacha salama B.I.G kwani miezi sita baadaye naye aliuawa na watu waliodaiwa ni mashabiki wa 2Pac, walioamua kulipiza kisasi. Kifo cha 2Pac kiliibua mengi. Na ukweli ni kwamba kuna simulizi nyingi ambazo hazijawahi kuthibitishwa juu ya waliodaiwa kumuua rapa huyo aliyetamba na Ngoma ya California Love, Me Against The World, Dear Mama na nyingine kibao. Hata hivyo, kinachofurahisha zaidi ingawa 2Pac aliyefariki dunia akiwa amefanya zaidi ya ngoma za video 50 na muvi takriban 5 zikiwemo Justice iliyotoka mwaka 1992 na Poetic Justice ya mwaka 1993, amekuwa akikumbukwa na kazi zake zimekuwa zikiishi.

 

Mama mzazi wa 2Pac, Afeni Shakur ambaye pia ni marehemu, alifariki dunia mapema mwaka jana, alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha anatunza ‘legacy’ au 2PAC 2PAC heshima ya mwanaye huyo. Hilo lilijidhihirisha pale alipoanzisha kituo huko Georgia, Marekani mwaka 1997 kiitwacho The Tupac Amaru Shakur Centrer For The Arts ambacho malengo yake makubwa ilikuwa ni kuhakikisha kinatunza kazi za ‘legendary’ huyo na kuwasaidia vijana wadogo wenye vipaji. Ingawa kituo hicho kilifungwa mwaka 2015, kilikuwa alama kubwa ya kuonesha kuwa 2pac anaishi.

 

Kama haitoshi, kwa nyakati tofauti, 2pac amekuwa akiorodheshwa kuwania na kujizolea tuzo kutoka kwa waandaaji mbalimbali zikiwemo Grammy, Mobo, MTV Video Music na nyinginezo. Lakini pia Aprili, mwaka huu alichukua Tuzo ya Heshima ya Rock and Roll Hall Of Fame iliyopokelewa na mwanamuziki mwenzake, Snoop Dogg. Huyo ndiye 2pac ambaye kesho katika siku yake ya kuzaliwa kupitia Kampuni ya Morgan Creek na washirika wake inamtambulisha ‘mzimu’ wa rapa huyo kupitia Muvi ya All Eyes On Me, jina ambalo lilibeba albam ya nne ya 2pac aliyoitoa mwaka 1996.

 

MZIMU HUU HAPA

Mwigizaji wa Hollywood, Marekani ambaye ametumika kama 2pac katika muvi hiyo anaitwa Demetrius Shipp Jr. Ni mshkaji mwenye umri wa miaka 28 na amekulia katika Mitaa ya Carson huko California, Los Angeles.

 

KAMA ZALI TU

Akizungumza na Mtandao wa TMZ hivi karibuni, Shipp Jr ambaye kabla ya kupata zali hilo alikuwa ‘akiinstoo’ satelaiti kwenye madishi alisema kuwa, hakuwahi kabisa kuwaza wala kuwa na ndoto za kuwa mwigizaji.

 

Msikie: “Kiukweli ilikuwa ni kama zali. Baada ya mwaka 2011, Morgan Creek kutangaza kuwafanyia audition (usaili) watu wanaofikiri wanafanana na 2Pac, rafiki zangu walinishawishi kwenda kushiriki. “Ilikuwa ni kazi ngumu kwao kunishawishi maana nilikuwa ninakataa na nilifahamu siwezi kufanya lolote, lakini jambo la muujiza baada ya kwenda nilifanikiwa, nikashinda.

 

“Ilikuwa ni kazi ngumu kuwa 2Pac. Kufanya vitu alivyofanya. Kuongea alivyoongea na hata kutembea kama yeye. Kila siku mchana na usiku nilitazama ‘clips’ za video za mshkaji (2Pac). Muda wote nilisikiliza ngoma zake na kusoma vitabu alivyosoma.”

 

Shipp Jr anafunguka kuwa, katika kutimiza malengo yake hayo kwa namna moja au nyingine amesaidiwa pia na baba yake mzazi, Demetrius Shipp Sr ambaye alifanya kazi na 2Pac akiwa prodyuza. Aliprodyuzi Ngoma ya Toss It Up na alimsaidia kwa namna alivyokuwa anamfahamu 2Pac.

Hata hivyo, Shipp anaendelea kusema kuwa, baada ya kupata shavu la kuigiza filamu hiyo ambayo anaamini itakuwa na mapokezi mazuri, huo ndiyo mwanzo wake wa kukomaa kwenye tasnia ya filamu za Hoollywood na kutimiza malengo yake mapya ya kuwa mwigizaji mwenye mafanikio makubwa.

 

MUVI KUITEKA DUNIA

 

Binafsi ninaiona muvi hii ya All Eyes On Me ikifika mbali. Ni muvi bora ambayo imekuwa na maandalizi mazuri. Miaka sita ya maandalizi tangu 2011 hadi mwaka huu si mchezo. Lakini waandishi wa script yake, akina Jeremy Haft, Eddie Gonzalez na Steven Bagatourian ni waandishi bora na wenye uzoefu.

 

Ukiachana na waandishi hao, dairekta wa muvi hiyo iliyogharimu Dola za Kimarekani milioni 45 (zaidi ya Sh. bilioni 90 za Kibongo), Benny Boom ni mtu mzoefu na maarufu. Boom anakumbukwa alivyofanya vizuri katika Muvi za Next Day Air (2009) na S.W.A.T (2011). Lakini pia dairekta huyo amedairekti video nyingi za wanamuziki maarufu zilizofanya vizuri ikiwemo ya Wimbo wa Window Shopper wa 50 Cent, I Wanna Love You wa Akon, Toutch It wa Busta Rhymes na Out Of My Mind wa B.O.B aliomshirikisha Nicki Minaj.

NA BONIFACE NGUMIJE, AMANI, MAKALA

VIDEO: Wema Sepetu na Gabo Walivyozindua Filamu Mpya ya ‘KISOGO’, Tazama Kipande Hapa

Leave A Reply