The House of Favourite Newspapers

NI BALAA! MJAMZITO AKINUKISHA KWA MTABIRI

 

NI mkosi juu ya balaa! Mama mjamzito aliyetambulika kwa jina la Nuru Abdallah, mkazi wa Magomeni jijini Dar, amekinukisha kwa Mrithi wa Mnajimu na Mtabiri wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini, Marehemu Sheikh Yahya Hussein, Alhaj Maalim Hassan Yahya Hussein, Risasi Jumamosi lina kisa na mkasa.

 

Tukio hilo lililoshuhudiwa na gazeti hili lilijiri mapema wiki hii, majira ya saa 10:00 jioni ofisini kwa Maalim Hassan maeneo ya Magomeni, Mwembe-Chai jijini Dar ambapo nusura ujauzito wa mwanamke huyo uchoropoke kutokana na mshikemshike.

 

Nuru alitinga ofisini hapo huku akiangua kilio kuwa alipwe fedha zake kiasi cha shilingi laki nne ambazo alimpa mtaalam huyo, lasivyo atarudi kwenye Gereza la Segerea alipokuwa amewekwa mahabusu akidaiwa fedha hizo ambazo ndizo kisa cha yeye kukutana na Maalim Hassan.

 

Akielezea kisa kizima, Nuru alidai kwamba, anakumbuka ilikuwa Oktoba, mwaka jana ambapo alikwenda kwa mtabiri huyo ili amsaidie kurudisha fedha za ndugu yake alizokuwa akidaiwa kiasi cha shilingi milioni nne. Alidai kuwa, alifikia hatua ya kwenda kwa Maalim Hassan baada ya fedha hizo alizotumiwa na ndugu yake kutoka Uarabuni kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

 

MSIKIE NURU

Nuru aliendelea kudai kwamba, alitinga kwa Maalim Hassan baada ya kuona ndugu yake amerejea kutoka Uarabuni na anamdai fedha zake na maji yalikuwa yamemfika shingoni.

“Nilikwenda kwa mtabiri baada ya kuambiwa na rafiki yangu kuwa niende kwa watabiri maana wana uwezo wa kunirudishia fedha, lakini pia niangaliwe nyota yangu kwa nini ninapoteza fedha katika mazingira ya utata, ndipo nilipokwenda kwa mtabiri huyo, nikijua atanisaidia,” alidai Nuru akihema juujuu.

SAKATA LA LILIPOANZIA

Nuru ambaye ni mke wa mtu alisema kuwa, alifika kwa Maalim Hassan na kumweleza shida yake ambapo alimuahidi kwamba atamsaidia kwa kumsafisha kinyota kisha atampa fedha ili amrudishie ndugu yake. “Aliniamuru nimpe shilingi laki nne ndiyo nitaweza kupata hizo fedha za majini.“Siku ya kwanza nilipompelekea fedha, alinipa masharti flani niyatimize, nami nikayatimiza,” alisema Nuru.

Malim Hassan Yahya.

 

TIBA YAENDELEA

Alidai kuwa, baada ya kutekeleza masharti aliyopewa, tiba iliendelea ambapo alirudi kwa Maalim Hassan na kupewa tiba nyingine. Alidai kuwa, Maalim alimshikisha sanduku likiwa tupu kisha akafumba macho, alipofumbua, aliona fedha za majini.

“Nilipoona zile fedha nyingi, akaniambia hizo ndiyo fedha zangu ila nichukue shilingi elfu kumi nikatumie kwanza, nione kama zinafanya kazi kisha nitarudi siku nyingine ndiyo anipe zile ninazodaiwa,” alidai.

 

ALIPOZITUMIA

Mama huyo mjamzito aliendelea kudai kwamba, fedha hizo alizopewa alizitumia kwenye daladala kulipia nauli ambapo zilipokelewa vizuri. Alisema, alimpa majibu mtabiri huyo ambaye alimwambia arudi kesho yake akampatie zile nyingine, lakini kwa masharti ya kutoa fedha nyingine za mafuta.

“Aliniambia nirudi siku nyingine ili anipe fedha zote ninazodaiwa, lakini alinipa sharti la kutoa shilingi laki tatu ili yanunuliwe mafuta ya kuzimwagia fedha hizo,” aliendelea kudai.

 

ASUBIRI KUPEWA PESA

Alisema kuwa, baada ya kutoa laki nne ambazo alitoa kwa awamu, aliambiwa asubiri atapewa fedha zake, lakini alikaa siku nyingi bila kupewa fedha hizo huku mtaalam huyo akimzungusha kila siku hadi ndugu yake alipompeleka Segerea ambako alikaa siku tisa.

“Huwezi kuamini, sikuona fedha zozote. Aliniambia ataniita, lakini hadi ninapelekwa Segerea sikuona chochote. Kule gerezani niliteseka sana, nilipata mateso na hivi nilivyo mjamzito, sina hamu, nimebaki naumia tu,” alisema Nuru.

ATAKA LAKI NNE ZAKE

Baada ya kutoka Segerea na kwenda kuuliza lini atapewa fedha hizo na kueleza matatizo aliyoyapata, mtabiri huyo alimwambia kuwa hawezi tena kumpatia fedha kwani ‘walimu’ wanaotoa pesa za majini walikuwa wamegoma.

Baada ya waandishi wetu kuona timbwili zima la mjamzito huyo na Maalim Hassan, walizungumza na mtabiri huyo ambaye alifafanua kuwa, yeye siyo Mungu na kwamba tiba ilishindikana.

 

 

MSIKIE MAALIM HASSAN

Mtabiri huyo alikiri kuchukua fedha za Nuru kiasi cha shilingi laki nne kwa ajili ya kumsaidia mwenye fedha atulie kama ambavyo amekuwa akiwasaidia wenzake, lakini haikuwezekana na akamuahidi kumrudishia fedha hizo kwa kumuonea huruma tu, sasa anashangaa yeye anavyotumia nguvu.

“Ninamshangaa anavyotumia nguvu, mimi ninafanya kazi hizi kihalali kabisa. Siwezi kutapeli shilingi laki nne kwani ninakutana na watu wengi. Laki nne ni ndogo sana, alinipa fedha zake, kazi haikuwezekana na mimi siyo Mungu,” alisema Maalim Hassan.

 

AELEZA ALIVYOZITUMIA

Maalim Hassan alieleza kuwa, fedha hizo alizochukua kwa Nuru alizitumia kununulia vifaa hivyo anashangaa anavyodaiwa na kuongeza kuwa, yeye alimfanyia kazi yake hivyo awe mpole amrudishie fedha zake kwa kumsaidia tu, lakini si lazima.

 

“Hivi niwaulize waandishi, mgonjwa akienda hospitalini akitibiwa asipopona anadai fedha? Au mgonjwa akifariki dunia, mara ngapi ndugu huwa hawachukui maiti hadi walipie? Sasa ninaweza kumwambia sitamlipa kwani nilikuwa ninamsaidia tu na mimi sikuzitumia fedha zake kwa matakwa yangu, nilinunua vifaa vya kumsaidia yeye,” alisema Maalim.

 

NI FEDHA ZA MAJINI?

Mtaalam huyo alisisitiza kuwa, yeye hana fedha za majini na kwamba kama zingekuwepo, angejipa mwenyewe kwa kuwa naye ana shida ya fedha.

“Mimi sina fedha za majini, huyu alitaka nimsaidie kumpoza ndugu yake asimdai na ndiyo tiba niliyokuwa ninamfanyia, mengine siyajui,” alimaliza Maalim Hassan kwa maelezo kuwa atamrudishia fedha zake

 

STORI: Hamida Hassan na Gladness Mallya, Dar

 

 

 

 

Comments are closed.