Mjamzito Alia – “Askofu Aliniahidi Kunioa na Kulea Mimba Yangu, Kakimbia”-Video
ULISHAWAHI kusikia askofu wa kanisa amemtapeli mwanamke kindoa? Basi kama hujawahi kusikia utapeli wa aina hiyo tambua kuwa hilo limedaiwa kumtokea mwanadada mrembo Jackline Msele, Mkazi wa Kibamba jijini Dar es Salaam, AMANI linakupakulia ishu nzima.
Akizungumza wiki hii na Amani, Jackline amelia kutapeliwa kimapenzi huku akimtaja mwanaume huyo kwa jina lakini kutokana na sababu za kimaadili Amani linalazimika kuficha jina lake sambamba na kanisa analohudumu.
Jackline anasema Februari 20, mwaka huu alitaraji kufunga ndoa na askofu huyo baada ya kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi lakini mkasa aliokutana nao ulikuwa mzito, itoshe tu kusema kwamba ndoa iliota mbawa katika dakika za majeruhi.
HUYU HAPA JACKLINEA
Akizungumza na AMANI katika ofisi za Global Publishers, Jackline mwenye umri wa miaka 34, alianza kusimulia mkasa huo kwa kujitambulisha kuwa yeye ni Katibu wa Chama cha Usuluhishi na Maridhiano Tanzania wilaya ya Ubungo.
Alisema, ndani ya chama hicho kinachoongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum pia kinashirikisha viongozi wa madhehebu mbalimbali kutoka Uislamu na Ukiristo.
Alisema, akiwa kama mmoja wa viongozi wa ngazi ya wilaya ndani ya chama hicho, alikumbwa na mkasa wa aina yake katika ndoa yake ya kwanza aliyofunga na mwanaume mmoja aliyemtambulisha kwa jina la Mwanajeshi kutokana na kazi aliyokuwa akiifanya mwanaume huyo.Jackline alisema, baada ya kufunga ndoa ya Kiserikali, Septemba 18, mwaka jana walitofautiana na mumewe huyo na hivyo kuamua kuanza kutafuta usuluhishi kwa viongozi wenzie wa chama hicho ambacho anakitumikia.
Wakati akiendelea kujaribu kuinusuru ndoa yake na mjeshi isivunjie rafiki yake mmoja alimshauri aende akamuonea askofu huyo anayemtuhumu kwa maelezo kwamba ataweza kuwasuluhisha.“
Nilikutana na askofu na kumsimulia maumivu ninayopitia ndani ya ndoa yangu kwa sababu mume wangu huyu mwanajeshi (wakati huo) aliniacha na kwenda kuishi na hausigeli wangu katika nyumba nyingine aliyokwenda kupanga. “Baada ya kunisikiliza, akanishauri kuwa nimwache huyo mwanajeshi yaani mume mwangu na yeye atanioa ndoa ya kanisa kabisa.
“Mbali na kukataa nilimsisitiza kuwa tayari nina ujauzirto wa mume wangu, lakini askofu huyo alisisitiza kuwa yupo tayari kuilea mimba yangu, kunitunza na kufunga ndoa na mimi.“
Kwa kweli nilikataa kabisa ushauri wake, lakini aliendelea kunishawishi kwa zaidi ya mwezi, huku akisisitiza kuwa suala la kuprocess talaka kutoka kwa mwanajeshi huyo halitakuwa shida kwake kwa nafasi aliyonayo,” alisema.
Alisema baada ya kushawishiwa na askofu huyo kwa muda mrefu, alimkubalia na kuanzisha naye uhusiano wa kimapenzi kwa kuwa aliamini kuwa kwa nafasi aliyonayo ndani ya chama, sifa ya jina la askofu pamoja na kuwa mwanaume aliyemzidi umri pakubwa alimkubalia.
Akiendelea kusimulia Jackline alisema muda mfupi baadaye askofu huyo alikwenda kumtambulisha nyumbani kwao Mrangu – Moshi mkoani Kilimanjaro kisha na yeye akampeleka kwa wazazi wake Kibosho – Moshi mkoani humo.
Alisema, baada ya utambulisho huo, mipango ya ndoa ilianza ambapo askofu huyo alikwenda kuandikisha ndoa katika kanisa moja la kiroho huko Moshi, kisha kukamilisha taratibu za kukodi bendi ya polisi kutoka Chuo cha Polisi (TPC) Moshi.
“Kwa upande wangu niliendelea na maandalizi mengine kama vile kuchangisha michango, huku askofu akidai tayari ndoa ameandikisha kwenye kanisa la askofu mwenzake huko Moshi.
MAMBO YAENDA MRAMA
Alisema, baada ya kumaliza utambulisho na maandalizi yote ya ndoa huko Moshi walirejea Dar kisha askofu huyo akamwagiza kutafuta nyumba nyingine ya kuishi kwa kuwa aliyokuwa akiishi mwanadada huyo ilidaiwa kuwa ni ndogo.
Alisema, baada ya kuambiwa hivyo na mumewe huyo mtarajiwa, Februari mwanzoni mwaka huu alipata nyumba yenye thamani ya kodi ya Sh 500,000 kwa mwezi.
Lakini cha kushangaza ni kuwa baada ya kuipata askofu alianza kukwepa kuilipia kodi jambo lililomfanya aamue kulipa kwa kutumia fedha yake na kuhamia ambapo baadaye askofu naye akamfuata.
Alisema wakati tarehe za harusi yao zikikaribia, ilipofika Februari 15 mwaka huu, mwanaume huyo alibeba nguo zake na kumuaga mkewe huyo mtarajiwa kwamba anaelekea Chamwino Dodoma kwenye ziara Rais.
“Awali mbali na kuwa na cheo hicho cha uaskofu aliambia kuwa anafanya kazi serikalini na idara mbalimbali nyeti hivyo mara nyingi anakuwa kwenye misafara ya rais na mshahara wake kwa mwezi ni Sh milioni 1.2.
“Ilipofika tarehe 16 Februari nikamsisitiza ziara inaisha lini maana siku ya harusi yetu inakaribia, aliniambia nivute subira maana haweza kuacha ziara hiyo, pia aliniagiza niache kumpigia simu maana akiwa kazini anafuatiliwa, kwamba hatakiwi kutumia simu mara kwa mara,” alisema Jackline.
Alisema ilipofika Februari 18, zikiwa zimesalia siku mbili ndoa yao ifungwe, alimpompigia mumewe huyo mtarajiwa hakupokea, badala yake alimtumia ujumb mfupi wa maneno kuwa kila mtu aendelee na maisha yake.
“Niliishiwa nguvu, maana nikiwaza aibu inayonipata, nguo za harusi nilikuwa nimenunua mwenyewe tena gauni la Sh 700,000, michango nimepewa, nilianguka nikazimia na kupelekwa hospitali na wasamaria wema.
“Baada ya kukaa hospitalini siku moja nilirejea nyumbani, ile michango nikaomba ndugu zangu wairejeshe kwa sababu askofu alikuwa hapatikana, nilipozungumza na baba yake mdogo ambaye nilitambulishwa nilipokwenda Moshi naye pia alinieleza kuwa kila akimpigia hapokei simu,” alisema.
Alisema kwa kuwa nyumba aliyokuwa amehamia na Askofu huyo ilikuwa ya gharama kubwa ilibidi atafute ya gharama ndogo ili aweze kumudu gharama anazochangiwa na ndugu.
WITO WAKE KWA WASICHANA
Alisema kutokana na madhila aliyetendewa na askofu huyo anawaonya wasichana wanaotarajia kuingia kwenye ndoa na wale wanaotafuta wenzi wao, kutokurupuka kutafuta mwanaume wa kumuoa ili apate muda sahihi wa kumchunguza.“Pia nawaomba Watanzania waniombee, au hata nikipata mtaalaam wa saikolojia anisaidie namna ya kurejea hali yangu ya kawaida maana nimekumbwa na msongo wa mawazo,” alisema.
MAJIBU YA ASKOFU
Ingawa Amani lingali likitafuta vielelezo vya tuhuma hizo zito kwa askofu liliamua kumtafua ili angalau kupata picha ya tukio.
Akizungumza na AMANI kwa njia ya simu, askofu huyo, awali alikana kuwa siyo yeye lakini baadaye alikir na kusema hawezi kumuoana Jackline kwa vile ni mke wa mtu.“Huyo ni mke wa mtu, tena ana mimba ya miezi sita… sasa mimi nitamuoa vipi? Au hujui ndoa ni hiari, maridhiano kati ya mimi na yeye. Hebu muulize kama nimewahi kupeleka mahari kwao.“Suala la kumuahidi kumuoa, hata wewe unaweza kuwa na mtu usiporidhika naye unamuacha, kwani lazima kuoa,” alisema.
TUWEKE KIPORO CHA HABARI
Kutokana na mazingira tata kujitokeza kwenye habari hii Amani limeamua kuiweka habari hii kiporo na kwamba mengi yatafumuka baada ya kufanyiwa upelelezi wa kina.Hata hivyo, habari ambazo Amani limezinyaka ni kwamba, Sheikh Alhad naye analifahamu jambo hili na kwamba ameshakutana na Jackline na kumwelekeza cha kufanya.
⚫️ Kwa UPDATES zote, Download GLOBAL APP: ⚫️ ANDROID:http://bit.ly/38Lluc8 ⚫️ iOS:https://apple.co/38HjiCx

