The House of Favourite Newspapers

Mjane Auawa Kisa Mgogoro wa Mirathi

0

MWANAMKE mmoja aliyefahamika kwa jina la Emma Mfikwa umri (43) ameuawa kikatili kwa vitu vyenye ncha kali na mtoto wake wa kumzaa kutokana na kile kinachodaiwa ni migogoro ya kifamilia iliyotokana na kugombania mali.

 

Hayo yamesemwa leo Jumanne, Julai 27, 2021 na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, Hamis Issah wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi ya makao makuu ya jeshi hilo hapa mkoani Njombe.

 

Amesema tukio hilo la kutisha lilitokea siku ya Julai 24 mwaka huu majira ya saa mbili za asubuhi mtaa wa Lunguya wilayani Njombe. Amesema jeshi hilo baada ya kufanya uchunguzi linawashikilia watuhumiwa wanne wa familia moja ambao wametajwa kuhusika na tukio hilo.

 

Amesema awali mwanamke huyo aliolewa na mume wake ambae kwa sasa ni marehemu aliamua kujenga nyumba kwenye kiwanja chao baada ya mumewe kufariki kitendo ambacho familia ya mume wa mwanamke huyo haikupenda na kutengeneza mgogoro mkubwa.

 

“Kesi ipo mahakamani inayohusiana na umiliki wa hiyo nyumba ila kesi hiyo haijafikia mwishoni mwanamke huyo ameuawa,” amesema Issah.

 

Alisema jambo la kushangaza katika tukio hilo miongoni mwa watuhumiwa waliokamata yupo mtoto wa marehemu ambaye amehusika katika tukio hilo la kikatili la mauaji.

 

Amesema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi ili kuwasaka watuhumiwa wengine waliohusika na mauaji hayo ambao wataunganishwa na kupelekwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika ili sheria ifuate mkondo wake.

 

“Napenda kuwaambia wana-Njombe haki ya mwanamke ipo palepale ya kuishi na kumiliki mali katika familia na hata ya kutofanyiwa ukatili wa aina yoyote,” amesema Issah.

 

Katika hatua nyingine jeshi hilo linamtafuta mtu aliyehusika kumtupa mtoto mwenye umri wa miezi tisa katika bonde la mto usiku karibu na chuo cha maendeleo ya jamii kilichopo mkoani hapa na kusababisha kifo chake.

 

Amesema chanzo cha kifo cha mtoto huyo ni baridi kali licha kuwa aliokotwa akiwa amefunikwa nguo ambapo inaonyesha kuwa mzazi wa mtoto huyo alimtelekeza akiamini kuwa watu watamkuta akiwa hai na kumchukua.

 

“Mtoto huyu inaonyesha alifariki kutokana na mazingira aliyowekwa huu ni ukatili mkubwa dhidi ya mtoto kwani hata wanyama wakali wangeweza kumla,” amesema Issah.

Leave A Reply