The House of Favourite Newspapers

Mjane wa Mtikila Avaa Viatu vya Mumewe, Asisitiza Mumewe Kauawa, Ataja Sababu

mama MtikilaElvan Stambuli na Sifael Paul | Gazeti la Uwazi, Toleo la Desemba 27, 2016

TUNAWEZA kusema ni mpiganaji wa kike, anayetetea wanyonge, huyu si mwingine ila ni aliyekuwa mke wa marehemu Mchungaji Christopher Reuben Mtikila aliyefariki dunia Oktoba 4, mwaka huu, Georgina Mtikila.

Gazeti hili lilimtafuta na kumkuta akiwa Makao Makuu ya Democratic Party (DP), Mchikichini, Ilala Dar es Salaam na kufanya mahojiano naye kama ifutavyo:

Unaweza kuwaambia wasomaji wetu nini kuhusu DP mwaka mmoja baada ya Mwenyekiti Mtikila kufariki dunia?

Jibu: Chama kimepata pigo kwa kuondokewa na mwaasisi wake ambaye alikuwa pia mfadhili na msemaji wake. Tulishauriwa na ofisi ya msajili wa vyama kuchagua mwenyekiti baada ya kifo cha mpendwa wetu.

Nani alichaguliwa na lini nafasi hiyo ilizibwa?

Jibu: Mei 25, mwaka huu kikao husika cha chama kiliketi Zanzibar na kuniteua mimi kukaimu nafasi ya mchungaji.

Lini DP itaketi na kumchagua mwenyekiti wake?

Jibu: Tuliamua katika kikao hicho kuwa Mkutano Mkuu wa DP uitishwe Januari 26, mwaka 2017 kwa ajili ya kujaza nafasi zilizo wazi ndani ya chama chetu.

Baada ya kuteuliwa kukaimu uenyekiti wa DP, umekumbana na changamoto gani?

ChristopherMtikilaMchungaji Christopher Reuben Mtikila enzi za uhai wake.

Jibu: Changamoto ni nyingi lakini tunafuata katiba. Changamoto kubwa ni fedha za kuendeshea chama, chama chetu hakipati ruzuku, hivyo tunakamuana sisi kwa sisi, hasa wale wapenzi wa chama wa hapa na mikoani. Changamoto nyingine ni maandalizi ya chaguzi za madiwani sehemu mbalimbali nchini. Hapa ndipo tunapogundua kuwa kumpoteza mwenyekiti wetu kiutendaji ni pigo kubwa kwetu kitaifa na kimataifa kwani alikuwa akitoa neno kwa manufaa ya taifa, hili naweza kusema ni changamoto ya  kitaifa.

Je, DP inashirikiana na vyama vingine vya siasa?

Jibu: Kiitikadi tupo tofauti kidogo, sisi tunaidai Tanganyika yetu, vyama vingine haviongelei hilo. Sisi tunataka Serikali ya Tanganyika iwepo na ya Zanzibar ipo na iendelee. Ina wimbo wake wa taifa, rais wake, bunge lao na kadhalika. Kwa nini wao waje kwenye bunge letu na kupiga kura kuamua mambo yetu? Mbona sisi hatuwaingilii mambo yao?

Kwa maana hiyo ina maana DP mnataka serikali tatu?

Jibu: Hapana. Serikali ya tatu ya nini? Huu muungano ni wa aina gani? Mwaka 2015 Zanzibar walipotengeneza katiba yao tayari walikuwa wamejitenga na Muungano, hilo watu hawalioni kwa nini? Hili kabla ya uchaguzi mwaka jana Mchungaji Mtikila aliiandikia barua Tume ya Uchaguzi ya Taifa kuwauliza tunaingiaje kwenye uchaguzi wakati Zanzibar imejitenga? Hawakujibu. Viongozi wakumbuke kwamba neno la Mungu linasema: ‘ Amelaaniwa aongezaye mipaka ya nchi yake,’ DP inasema Tanganyika iwe Tanganyika na Zanzibar iwe Zanzibar.

Unadhani Rais Dk. John Magufuli anakwenda vizuri katika utawala wake?

Jibu: Inavyoonekana Magufuli ana maono, lakini nani ajuwaye anapotupeleka? Nchi hii ina mali nyingi lakini iligeuzwa shamba la bibi, watu wanapata shida wakati tuna dhahabu, makaa ya mawe, almasi, Tanzanite na kadhalika halafu nchi jirani inaongoza kwa kuuza Tanzanite, inakuwa best seller wakati haina hata machimbo, tuna akili kweli? Magufuli anaondoa mwiba kwenye mguu ndiyo maana watu wanapata maumivu japokuwa neno ‘kutumbua’ siyo zuri.

Unamzungumziaje rais kwa kitendo chake cha kuzuia mikutano ya hadhara?

Jibu: Kifupi kuzuia mikutano ya hadhara ya siasa ni kufunga siasa nchini, ni maono yake lakini ajue anavunja katiba na tunajiuliza tunakokwenda kukoje?

Vipi tuhuma kwamba Mchungaji Mtikila aliuawa, kuna kesi yoyote hadi sasa imefunguliwa? Kuna madai kuwa kuna ushirikina unafanyika pale alipofia, unasemaje kuhusu hilo?

Jibu: Hakuna kesi. Waliomuua mchungaji tunawajua lakini serikali imekaa kimya. Nimehangaika sana kuhusu suala hilo ili haki itendeke, nikakwamishwa. Nimeenda polisi, kwa msajili wa vyama na kuandika barua kwa Rais Kikwete (Jakaya) na hata kwa Magufuli, nimeshindwa kupata jawabu na sasa nimemuachia Mungu. Bado naomba na kusali kuhusu tukio hilo na naamini Mungu atajibu. Kuhusu ushirikina ile sehemu, nimesikia hilo pia namuachia Mungu japokuwa wananiumiza sana kwa vitendo hivyo wanavyofanya, waache, tupo kwenye maombi makali sana kuhusu kifo kile. Kuna mambo mengi sana kuhusu kifo kile, tuliiomba Mamlaka ya Mawasiliano yaani Tanzania Communications Regulatory Authority (TCRA) itusaidie mtu aliyeweka picha kwanza alfajiri kuonyesha mauti ya Mchungaji Mtikila alikuwa wapi? Kwenye tukio? Au ni hao wauaji walikuwa wanatoa taarifa kwa waajiri wao kuwa wamekamilisha kazi! Tuliuliza aliyeweka picha ya Dk. Jean-Bosco Ngendahimana kwenye mtandao kuwa ndiye anahusika na mauaji ya  Mch. Mtikila na kumsingizia kuwa amekamatwa na polisi akiwa anajiandaa kukimbia wakati siyo kweli. Sasa tunamtegemea Mungu baada ya serikali kushindwa kunisaidia kuwatafuta wauaji wa Mchungaji.

Nini mkakati wa DP sasa hivi?

Jibu: Mkakati wetu ni kuhakikisha tunafanya mkutano mkuu wa chama Mei 25, mwakani, kila mtendaji awajibike na wananchi wote wapenzi wa dekomrasia wanakaribishwa kutuchangia.

Msikie laivu hapa akizungumza mwenyewe

Comments are closed.