MKUU wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema amesema kuwa waendesha bodaboda wanathaminiwa na serikali kama walivyo wafanyabiashara wengine kwani wanaingiza kipato kupitia usafirishaji wao.
Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dar es Salaam kwenye Viwanja vya Mashujaa alipokuwa mgeni rasmi kwenye hafla fupi ya vijana waendesha bodaboda wa wilaya yake waliokutana kupongeza juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
Wakielezea katika hotuba yao, waendesha bodaboda hao wamesema kuwa Rais Magufuli anapaswa kuungwa mkono na kila mwananchi kutokana na utendaji kazi wake ambao umetukuka hasa anavyozuia rasilimali za nchi zisiibiwe na watu wachache wasiopenda maendeleo ya nchi.
Katika hotuba hiyo, wameelezea mambo mengi ambayo Rais Magufuli ameyafanya kwa kipindi kifupi na hivyo kuomba waendesha bodaboda kutoka mikoa mingine kumuunga mkono kwa maendeleo yanayoonekana.
Akijibu hotuba hiyo, Mjema amewapongeza waendesha bodaboda akiwaeleza kuwa hotuba yao itafanyiwa kazi na serikali kwa jumla iko pamoja nao na wanachopaswa kufanya ni kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Mjema amezitaka kampuni zinazofanya kazi ya kukamata bodaboda wanaoingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam, kuhakikisha wanawapatia risiti za kielektroniki ili fedha hizo ziweze kuingia katika mapato ya serikali na si vinginevyo na wazingatie sheria badala ya kuwakamata kwa kuwaonea kama wenyewe wanavyolalamika.
NA DENIS MTIMA/GPL.