The House of Favourite Newspapers

Mjue Bilionea wa Sudan ya Kusini Mwenye Utajiri Tata

BILIONEA tata wa Sudan ya Kusini,  Lawrence Lual Malong Yor Jnr, amezua sintofahamu miongoni mwa watu wa Kenya wiki hii baada ya kuzagaa habari kwamba ametoa misaada ya mamilioni ya fedha kwa mashirika mbalimbali nchini humo, habari ambazo zilikuja kujulikana kuwa ni za uongo.

Yor, anayejitambulisha kuwa ni “bilionea kijana zaidi Afrika” alidai majuzi katika video iliyozagaa mitandaoni kwamba ametoa Dola mil. 5 kwa Chama cha Msalaba Mwekundu cha Kenya na cha Sudan ya Kusini, akiongeza kwamba atausaidia Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Kenya (Kuso) na makanisa katika miji ya Juba na Nairobi.

Hata hivyo, vyama hivyo vimekanusa madai hayo, vikisema ni uwongo, kwa mujibu wa gazeti la Citizen Digital la Kenya.

Kilichowaudhi Wakenya wengi ni jinsi viongozi wa umoja huo wa wanafunzi unavyommwagia sifa Yor mwenye umri wa miaka 30, mtu anayejivuna kwamba huvaa viatu vya thamani ya Dola 10,000 (Sh. mil. 22) na kupanda ndege zinazotumiwa na marais duniani.

Kuna habari zinazosema Yor ni mtoto wa kambo wa Jenerali Paul Malong ambaye amedaiwa kutajirika kutokana na vita vya Sudan Kusini, ambapo utajiri huo ameuficha katika mabenki ya nchi za nje.

Jenerali Malong, alifukuzwa kazi mwaka 2017 na Rais wa Sudan ya Kusini, Salva Kiir, lakini amekana kuhusika na ukatili unaotokea nchini humo ambapo umewakosesha watu wapatao milioni mbili makazi yao tangu mwaka  2013.

Vilevile, Malong amekana kuhusika na “tajiri kijana” huyo akisema si mtoto wake wa kambo na ametishia kumchukulia hatua za kisheria yeyote anayesema ni mtoto wake.

Image result for Lawrence Lual Malong Yor Jnr

Yor alipoulizwa alivyoupata utajiri wake, alisema amebarikiwa tu na Bwana Yesu Kristo.

“Bwana wangu Yesu Kristo alinibariki; ninasafiri katika ndege za kifahari;  naishi katika nyumba wanazoishi marais, nimebarikiwa,” alisema.

Mara ya kwanza Yor alifahamika kwa watu wengi alipo-posti video katika mitandao ikimwonyesha amelala kwenye kitanda kilichotapakaa minoti ya Dola milioni moja aliyosema angeyatoa kama misaada kwa jamii.

Comments are closed.