Mjue Binti Wa Trump Ambaye Amekataa Kujiingiza Kwenye Siasa – Video

Ivanka Trump hana mpango wowote wa kurudi White House kumsaidia baba yake kuendesha nchi wakati wa muhula wake wa pili wa urais, akisema kwa uwazi kabisa: “Nachukia siasa.”
Binti mkubwa wa Rais Donald Trump, ambaye alikuwa mmoja wa washauri wake wa juu wakati wa muhula wake wa kwanza, hivi karibuni alisema kwenye podcast ya “Him & Her Show” kwamba kwa sasa hataki tena kushiriki siasa na ataepuka kabisa kurudi Washington DC.
“Napenda sera na athari chanya zake. Nachukia siasa. Na bahati mbaya, sera na siasa haviwezi kutenganishwa” alisema Ivanka, binti mwenye umri wa miaka 43.
Kwanini Ivanka Hataki Kurudi White House
Ivanka alielezea sababu kuu inayomfanya asikubali kurudi kwenye mazingira ya siasa kwa kusema, nanukuu:“Kuna mambo ya giza katika dunia hiyo ya siasa ambalo sitaki kulikaribisha kwenye maisha yangu.”
Aliongeza kwa kusema na nina nukuu:
“Kwa kiasi fulani, niko katikati ya dhoruba kwa sababu baba yangu sasa ni rais, lakini siasa ni biashara yenye giza. Watu wengine wanapenda maisha ya kupigana, vurugu — mimi sijawahi kuwa mmoja wao.” Mwisho wa kunukuu
Ivanka, ambaye amehamia jiji la Florida na mumewe Jared Kushner pamoja na watoto wao watatu baada ya kushindwa kwa uchaguzi wa baba yake mwaka 2020, alisema bado ataendelea kumuunga mkono baba yake kwa njia nyingine. Katika hili, Ivanka alinukuliwa akisema: Nanukuu
“Natarajia kuwa karibu naye kama binti, kuonyesha upendo wangu kwake na kumfariji, labda kwa kutizama filamu pamoja, au mechi ya mpira, ili tu kumtoa kwenye mawazo ya mambo mazito,” alisema.
Nani ni Ivanka Trump?
Ivanka, kwa jina lake kamili Ivana Marie Trump, alizaliwa Oktoba 30, 1981. Yeye ni binti mkubwa wa Rais Donald Trump na mtoto wa pili kati ya watoto watatu wa ndoa yake ya kwanza na marehemu mkewe wa zamani, Ivana Trump. Ivana alifariki Julai 2022 baada ya kuumia kwa ajali nyumbani kwake New York City.
Ivanka ana kaka zake wawili wa baba mmoja, mama mmoja, ambao ni:
Donald Trump Jr. (46)
Eric Trump (40)
Pia ana ndugu wengine waliochangia baba mmoja:
Tiffany Trump (31)
Barron Trump (18).
Elimu na Kazi za Awali za Ivanka
Ivanka alikulia Manhattan, ambako alisoma katika shule maarufu ya Chapin kabla ya kuhamia Choate Rosemary Hall kwa masomo ya sekondari. Aliendelea na masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Georgetown kabla ya kuhamia Chuo Kikuu cha Pennsylvania, ambapo alihitimu mwaka 2004 na shahada ya uchumi.
Kabla ya kuingia White House kama mshauri mwandamizi wa serikali ya baba yake, Ivanka alihudumu kama makamu wa rais mtendaji katika Shirika la Trump hadi Januari 2017. Pia alianzisha miradi yake ya kibunifu, ikiwa ni pamoja na lebo ya mitindo aliyofungua mwaka 2014 na kuifunga mwaka 2018.
Wakati wa utumishi wake Ikulu, Ivanka alihusika katika kuanzisha Women’s Global Development and Prosperity Initiative, ambayo inalenga kuongeza ushiriki wa kiuchumi wa wanawake duniani.
Baada ya kuacha nafasi yake rasmi serikalini Januari 2021, Ivanka amekuwa akiendelea kushiriki katika shughuli za kibiashara na za hisani.
Ivanka Trump na Jared Kushner
Ivanka aliolewa na Jared Kushner, mwekezaji maarufu wa majengo, mnamo Oktoba 2009 baada ya kuwa kwenye mahusiano kwa miaka miwili. Wawili hao walikutana wakiwa katika masuala ya kibiashara na kuanzisha urafiki ambao baadae uligeuka kuwa mapenzi.
Kushner nae alikuwa mmoja wa washauri wakuu wa Trump wakati wa muhula wake wa kwanza, lakini baada ya uchaguzi wa 2020, aliamua kujitenga na siasa.
Hivi sasa, Jared anaendesha mfuko wa uwekezaji binafsi wenye thamani ya dola bilioni 3 na anashirikiana na mataifa mbalimbali kama Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, na Qatar.
Kiburudani; Ivanka na Jared walionekana katika moja ya sehemu za kipindi maarufu cha televisheni, “Gossip Girl,” msimu wa nne.
Ivanka na Jared Wana watoto watatu pamoja, ambao ni:
Arabella Rose (13)
Joseph Frederick (11)
Theodore James (8).
Baada ya kuolewa Ivanka alijiunga na Uyahudi kama mumewe, ambaye familia yake ni wa Kanisa la Orthodox.
Huyu ndiye Ivanka Trump: Binti wa kwanza wa Rais wa 47 wa Marekani, Donald John Trump!